Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Wimbo Ulio Bora 4:1-16

Wimbo Ulio Bora 4:1-16 Biblia Habari Njema (BHN)

Hakika u mzuri ewe mpenzi wangu, hakika u mzuri! Macho yako ni kama ya hua nyuma ya shela lako, nywele zako ni kama kundi la mbuzi washukao katika milima ya Gileadi. Meno yako ni kama kondoo majike waliokatwa manyoya wanaoteremka baada ya kuogeshwa. Kila mmoja amezaa mapacha, na hakuna yeyote aliyefiwa. Midomo yako ni kama utepe mwekundu, kinywa chako chavutia kweli. Nyuma ya shela lako, mashavu yako ni kama nusu mbili za komamanga. Shingo yako ni kama mnara wa Daudi, uliojengwa ili kuhifadhia silaha, ambako zimetundikwa ngao elfu moja zote zikiwa za mashujaa. Matiti yako ni kama paa mapacha, ambao huchungwa penye yungiyungi. Nitakaa kwenye mlima wa manemane, na kwenye kilima cha ubani, hadi hapo kutakapopambazuka, na giza kutoweka. Tazama ulivyo mzuri ee mpenzi wangu, wewe huna kasoro yoyote. Njoo, bibiarusi wangu tuondoke Lebanoni; na tuiachilie mbali Lebanoni. Shuka toka kilele cha mlima Amana, toka kilele cha Seniri na Hermoni, toka mapango ya simba, toka milima ya chui. Umefurahisha moyo wangu, dada yangu, bi arusi, umefurahisha moyo wangu, kwa kunitupia jicho mara moja tu, na kwa huo mkufu wako shingoni. Dada yangu, bi arusi; pendo lako ni tamu ajabu. Ni bora kuliko divai, marashi yako yanukia kuliko viungo vyote. Midomo yako yadondosha asali, ee bibiarusi wangu; ulimi wako una asali na maziwa. Harufu nzuri ya mavazi yako ni kama ya Lebanoni. Dada yangu, naam, bi arusi, ni bustani iliyofichika, bustani iliyosetiriwa; chemchemi iliyotiwa mhuri. Machipukizi yako ni bustani ya mikomamanga pamoja na matunda bora kuliko yote, hina na nardo. Nardo na zafarani, mchai na mdalasini manemane na udi, na mimea mingineyo yenye harufu nzuri. U chemchemi ya bustani, kisima cha maji yaliyo hai, vijito vitiririkavyo kutoka Lebanoni. Vuma, ewe upepo wa kaskazi, njoo, ewe upepo wa kusi; vumeni juu ya bustani yangu, mlijaze anga kwa manukato yake. Mpenzi wangu na aje bustanini mwake, ale matunda yake bora kuliko yote.

Wimbo Ulio Bora 4:1-16 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Tazama, u mzuri, mpenzi wangu, U mzuri, macho yako ni kama ya hua, Nyuma ya barakoa yako. Nywele zako ni kama kundi la mbuzi, Wakijilaza mbavuni pa mlima Gileadi. Meno yako ni kama kundi waliokatwa manyoya, Wakipanda kutoka kuoshwa, Ambao kila mmoja amezaa mapacha, Wala hakuna aliyefiwa kati yao. Midomo yako ni kama uzi mwekundu, Na kinywa chako ni kizuri; Mashavu yako ni kama nusu kipande cha komamanga, Nyuma ya barakoa yako. Shingo yako ni kama mnara wa Daudi, Uliojengwa pa kuwekea silaha; Ngao elfu zimetungikwa juu yake, Zote ni ngao za mashujaa. Matiti yako mawili ni kama wanapaa wawili, Nyuma ya barakoa yako. Ambao ni mapacha ya paa; Wakilisha penye nyinyoro. Hata jua lipunge, na vivuli vikimbie, Nitakwenda kwenye mlima wa manemane, Na kwenye kilima cha ubani. Mpenzi wangu, u mzuri kwa ujumla, Wala ndani yako hamna kasoro. Bibi arusi, njoo pamoja nami toka Lebanoni, Pamoja nami toka Lebanoni. Shuka kutoka kilele cha Amana, Kutoka vilele vya Seniri na Hermoni; Kutoka mapangoni mwa simba, Kutoka milimani mwa chui. Umenishangaza moyo, dada yangu, Bibi arusi, umenishangaza moyo, Kwa mtupo mmoja wa macho yako, Kwa mkufu mmoja wa shingo yako. Jinsi pendo lako lilivyo nzuri, dada yangu, Bibi arusi, ni nzuri kupita divai; Na harufu ya marhamu yako Yapita manukato ya kila namna. Bibi arusi, midomo yako yadondosha asali, Asali na maziwa viko chini ya ulimi wako; Na harufu ya mavazi yako Ni kama harufu ya Lebanoni. Bustani iliyofungwa ni dada yangu, bibi arusi, Kijito kilichofungwa, chemchemi iliyotiwa mhuri. Machipuko yako ni bustani ya komamanga, Yenye matunda mazuri, hina na nardo, Nardo na zafarani, mchai na mdalasini, Na miti yote iletayo ubani, Manemane na udi, na kolezi kuu zote. Wewe ndiwe chemchemi ya bustani yangu, Kisima cha maji yaliyo hai, Vijito vya Lebanoni viendavyo kasi. Amka, kaskazi; nawe uje, kusi; Vumeni juu ya bustani yangu, Manukato ya bustani yatokee. Mpendwa wangu na aingie bustanini mwake, Akayale matunda yake mazuri.

Wimbo Ulio Bora 4:1-16 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Tazama, u mzuri, mpenzi wangu, U mzuri, macho yako ni kama ya hua, Nyuma ya barakoa yako. Nywele zako ni kama kundi la mbuzi, Wakijilaza mbavuni pa mlima Gileadi. Meno yako ni kama kundi waliokatwa manyoya, Wakipanda kutoka kuoshwa, Ambao kila mmoja amezaa mapacha, Wala hakuna aliyefiwa kati yao. Midomo yako ni kama uzi mwekundu, Na kinywa chako ni kizuri; Mashavu yako ni kama kipande cha komamanga, Nyuma ya barakoa yako. Shingo yako ni kama mnara wa Daudi, Uliojengwa pa kuwekea silaha; Ngao elfu zimetungikwa juu yake, Zote ni ngao za mashujaa. Maziwa yako mawili ni kama wana-paa wawili, Nyuma ya barakoa yako. Ambao ni mapacha ya paa; Wakilisha penye nyinyoro. Hata jua lipunge, na vivuli vikimbie, Nitakwenda kwenye mlima wa manemane, Na kwenye kilima cha ubani. Mpenzi wangu, u mzuri pia pia, Wala ndani yako hamna ila. Bibi arusi, njoo pamoja nami toka Lebanoni, Pamoja nami toka Lebanoni. Shuka kutoka kilele cha Amana, Kutoka vilele vya Seniri na Hermoni; Kutoka mapangoni mwa simba, Kutoka milimani mwa chui. Umenishangaza moyo, umbu langu, Bibi arusi, umenishangaza moyo, Kwa mtupo mmoja wa macho yako, Kwa mkufu mmoja wa shingo yako. Jinsi zilivyo nzuri pambaja zako, umbu langu, Bibi arusi, ni nzuri kupita divai; Na harufu ya marhamu yako Yapita manukato ya kila namna. Bibi arusi, midomo yako yadondoza asali, Asali na maziwa vi chini ya ulimi wako; Na harufu ya mavazi yako Ni kama harufu ya Lebanoni. Bustani iliyofungwa ni umbu langu, bibi arusi, Kijito kilichofungwa, chemchemi iliyotiwa muhuri. Machipuko yako ni bustani ya komamanga, Yenye matunda mazuri, hina na nardo, Nardo na zafarani, mchai na mdalasini, Na miti yote iletayo ubani, Manemane na udi, na kolezi kuu zote. Wewe ndiwe chemchemi ya bustani yangu, Kisima cha maji yaliyo hai, Vijito vya Lebanoni viendavyo kasi. Amka, kaskazi; nawe uje, kusi; Vumeni juu ya bustani yangu, Manukato ya bustani yatokee. Mpendwa wangu na aingie bustanini mwake, Akayale matunda yake mazuri.

Wimbo Ulio Bora 4:1-16 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

Tazama jinsi ulivyo mzuri, mpendwa wangu! Ee, jinsi ulivyo mzuri! Macho yako nyuma ya shela yako ni kama ya hua. Nywele zako ni kama kundi la mbuzi wakishuka kutoka Mlima Gileadi. Meno yako ni kama kundi la kondoo waliokatwa manyoya sasa hivi, wanaotoka kuogeshwa. Kila jino lina pacha lake; hakuna hata moja lililo pekee. Midomo yako ni kama uzi mwekundu, kinywa chako kinapendeza. Mashavu yako nyuma ya shela yako ni kama vipande viwili vya komamanga. Shingo yako ni kama mnara wa Daudi, uliojengwa kwa madaha, juu yake zimetundikwa ngao elfu, zote ni ngao za mashujaa. Matiti yako mawili ni kama wana-paa wawili, kama wana-paa mapacha wajilishao kati ya yungiyungi. Hata kupambazuke na vivuli vikimbie, nitaenda kwenye mlima wa manemane na kwenye kilima cha uvumba. Wewe ni mzuri kote, mpendwa wangu, hakuna hitilafu ndani yako. Nenda nami kutoka Lebanoni, bibi arusi wangu, nenda nami kutoka Lebanoni. Shuka kutoka ncha ya Amana, kutoka juu ya Seniri, kilele cha Hermoni, kutoka mapango ya simba na kutoka mlima wapendapo kukaa chui. Umeiba moyo wangu, dada yangu, bibi arusi wangu; umeiba moyo wangu kwa mtazamo mmoja wa macho yako, kwa kito kimoja cha mkufu wako. Tazama jinsi pendo lako linavyofurahisha, dada yangu, bibi arusi wangu! Pendo lako linafurahisha aje zaidi ya divai, na harufu ya marhamu yako zaidi ya manukato yoyote! Midomo yako inadondosha utamu kama sega la asali, bibi arusi wangu; maziwa na asali viko chini ya ulimi wako. Harufu nzuri ya mavazi yako ni kama ile ya Lebanoni. Wewe ni bustani iliyofungwa, dada yangu, bibi arusi wangu; wewe ni chanzo cha maji kilichozungushiwa kabisa, chemchemi yangu peke yangu. Mimea yako ni bustani ya mikomamanga yenye matunda mazuri sana, yenye hina na nardo, nardo na zafarani, mchai na mdalasini, pamoja na kila aina ya mti wa uvumba, manemane na udi, na aina zote za vikolezo bora kuliko vyote. Wewe ni chemchemi ya bustani, kisima cha maji yanayotiririka, yakitiririka kutoka Lebanoni. Amka, upepo wa kaskazini, na uje, upepo wa kusini! Vuma juu ya bustani yangu, ili harufu yake nzuri iweze kuenea mpaka ngʼambo. Mpenzi wangu na aje bustanini mwake na kuonja matunda mazuri sana.