Wimbo Ulio Bora 2:4-16
Wimbo Ulio Bora 2:4-16 Biblia Habari Njema (BHN)
Alinichukua hadi ukumbi wa karamu, akatweka bendera ya mapenzi juu yangu. Nishibishe na zabibu kavu, niburudishe kwa matofaa, maana naugua kwa mapenzi! Mkono wake wa kushoto chini ya kichwa changu, mkono wake wa kulia wanikumbatia. Nawasihi enyi wanawake wa Yerusalemu, kama walivyo paa au swala wa porini, msiyachochee wala kuyaamsha mapenzi, hadi hapo wakati wake utakapofika. Hiyo ni sauti ya mpenzi wangu, yuaja mbio, anaruka milima, vilima anavipita kasi! Mpenzi wangu ni kama paa, ni kama swala mchanga. Amesimama karibu na ukuta wetu, achungulia dirishani, atazama kimiani. Mpenzi wangu aniambia: “Inuka basi, ewe mpenzi wangu, unipendezaye, njoo twende zetu. Tazama, majira ya baridi yamepita, nazo mvua zimekwisha koma; maua yamechanua kila mahali. Wakati wa kuimba umefika; sauti ya hua yasikika mashambani mwetu. Mitini imeanza kuzaa; na mizabibu imechanua; inatoa harufu nzuri. Njoo, basi, ewe mpenzi wangu unipendezaye, njoo twende. Ee hua wangu, uliyejificha miambani. Hebu niuone uso wako, hebu niisikie sauti yako, maana sauti yako yapendeza na uso wako wavutia. “Tukamatieni mbweha, wale mbweha wadogowadogo, wanaoiharibu mizabibu yetu inayochanua.” Mpenzi wangu ni wangu, nami ni wake. Yeye hulisha kondoo wake penye yungiyungi
Wimbo Ulio Bora 2:4-16 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Akanileta mpaka nyumba ya karamu, Na bendera yake juu yangu ni mapenzi. Nishibisheni zabibu, niburudisheni kwa mapera, Kwa maana nimezimia kwa mapenzi. Mkono wake wa kushoto uko chini ya kichwa changu, Nao wa kulia unanikumbatia! Nawasihi, enyi binti za Yerusalemu, Kwa paa na kwa ayala wa porini, Msiyachochee mapenzi, wala kuyaamsha, Hata yatakapoona vema yenyewe. Sikiliza! Ni mpendwa wangu! Tazama, anakuja, Akiruka milimani, akichachawa vilimani. Mpendwa wangu ni kama paa, au ayala. Tazama, asimama nyuma ya ukuta wetu, Achungulia dirishani, atazama kimiani. Mpendwa wangu alinena, akaniambia, Ondoka, mpenzi wangu, mzuri wangu, uje zako, Maana tazama, majira ya baridi yamepita, Masika imekwisha, imekwenda zake; Maua yatokea katika nchi, Wakati wa kuimba umefika, Na sauti ya mwigo husikiwa kwetu. Mtini wapevusha tini zake, Na mizabibu inachanua, Inatoa harufu yake nzuri; Ondoka, mpenzi wangu, mzuri wangu, uje zako. Hua wangu, mafichoni mwa jabali, Katika sitara za, magenge Nitazame uso wako, nisikie sauti yako, Maana sauti yako ni tamu na uso wako unapendeza. Tukamatie mbweha, Wale mbweha wadogo, Waiharibuo mizabibu, Maana mizabibu yetu yachanua. Mpendwa wangu ni wangu, na mimi ni wake; Hulisha kundi lake penye nyinyoro.
Wimbo Ulio Bora 2:4-16 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Akanileta mpaka nyumba ya karamu, Na bendera yake juu yangu ni mapenzi. Nishibisheni zabibu, niburudisheni kwa mapera, Kwa maana nimezimia kwa mapenzi. Mkono wake wa kushoto uko chini ya kichwa changu, Nao wa kuume unanikumbatia! Nawasihi, enyi binti za Yerusalemu, Kwa paa na kwa ayala wa porini, Msiyachochee mapenzi, wala kuyaamsha, Hata yatakapoona vema yenyewe. Sikiliza! Ni mpendwa wangu! Tazama, anakuja, Akiruka milimani, akichachawa vilimani. Mpendwa wangu ni kama paa, au ayala. Tazama, asimama nyuma ya ukuta wetu, Achungulia dirishani, atazama kimiani. Mpendwa wangu alinena, akaniambia, Ondoka, mpenzi wangu, mzuri wangu, uje zako, Maana tazama, kaskazi imepita, Masika imekwisha, imekwenda zake; Maua yatokea katika nchi, Wakati wa kupelea umefika, Na sauti ya mwigo husikiwa kwetu. Mtini wapevusha tini zake, Na mizabibu inachanua, Inatoa harufu yake nzuri; Ondoka, mpenzi wangu, mzuri wangu, uje zako. Hua wangu, mafichoni mwa jabali, Katika sitara za magenge, Nitazame uso wako, nisikie sauti yako, Maana sauti yako ni tamu na uso wako mzuri. Tukamatie mbweha, Wale mbweha wadogo, Waiharibuo mizabibu, Maana mizabibu yetu yachanua. Mpendwa wangu ni wangu, na mimi ni wake; Hulisha kundi lake penye nyinyoro.
Wimbo Ulio Bora 2:4-16 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Amenichukua hadi ukumbi wa karamu, na bendera ya huyu mwanaume juu yangu ni upendo. Nitie nguvu kwa zabibu kavu, niburudishe kwa matofaa, kwa maana ninazimia kwa mapenzi. Mkono wake wa kushoto uko chini ya kichwa changu, na mkono wake wa kuume unanikumbatia. Binti za Yerusalemu, ninawaagiza kwa paa na kwa ayala wa shambani: Msichochee wala kuamsha mapenzi hata yatakapotaka yenyewe. Sikiliza! Mpenzi wangu! Tazama! Huyu hapa anakuja, akirukaruka juu milimani akizunguka juu ya vilima. Mpenzi wangu ni kama paa au ayala mchanga. Tazama! Anasimama nyuma ya ukuta wetu, akitazama kupitia madirishani, akichungulia kimiani. Mpenzi wangu alizungumza na kuniambia, “Inuka, mpendwa wangu, mrembo wangu, tufuatane. Tazama! Wakati wa masika umepita, mvua imekwisha na ikapita. Maua yanatokea juu ya nchi; majira ya kuimba yamewadia, sauti za njiwa zinasikika katika nchi yetu. Mtini unatunga matunda yake ya mwanzoni, zabibu zinazochanua zaeneza harufu nzuri. Inuka, njoo mpenzi wangu. Mrembo wangu, tufuatane.” Hua wangu penye nyufa za majabali, mafichoni pembezoni mwa mlima, nioneshe uso wako, na niisikie sauti yako, kwa maana sauti yako ni tamu, na uso wako unapendeza. Tukamatie mbweha, mbweha wale wadogo wanaoharibu mashamba ya mizabibu, mashamba yetu ya mizabibu yaliyochanua. Mpenzi wangu ni wangu, nami ni wake, yeye hujilisha kati ya yungiyungi.