Ruthu 3:12-18
Ruthu 3:12-18 Biblia Habari Njema (BHN)
Ni kweli kwamba ni jukumu langu kukutunza, lakini kuna pia mwenye jukumu la kukutunza na ambaye yu karibu zaidi kuliko mimi. Kwa hiyo, kaa hapa usiku wote, na kesho asubuhi tutaona kama atakubali kukutunza au la. Ikiwa atakutunza ni vyema. Akikataa, kwa jina la Mwenyezi-Mungu aliye hai mimi nitakutunza. Lala hapa mpaka asubuhi.” Basi Ruthu akalala hapo miguuni pake mpaka asubuhi, lakini aliamka alfajiri ili asionekane, kwa kuwa Boazi hakutaka mtu ajue kuwa Ruthu alikuwa mahali pa kupuria. Boazi akamwambia, “Tandika nguo yako chini.” Ruthu akafanya hivyo. Boazi akamwaga shayiri ipatayo vipimo sita, akamtwika, naye akarudi mjini. Alipofika mjini, mkwewe akamwuliza, “Ilikuwaje binti yangu?” Ruthu akamweleza yote ambayo Boazi alimtendea. Halafu akaendelea kusema, “Aliniambia nisirudi nyumbani kwa mkwe wangu mikono mitupu na kwa hiyo alinipa shayiri hii ipatayo vipimo sita.” Naye Naomi akasema, “Sasa tulia binti yangu Ruthu, mpaka uone litakalotokea. Boazi hatatulia leo mpaka ameyatimiza yote.”
Ruthu 3:12-18 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Tena ni kweli kuwa mimi ni jamaa yako aliye karibu; lakini kuna mtu wa jamaa aliye karibu kuliko mimi. Wewe ungoje usiku huu; kisha, asubuhi, kama akikubali kukufanyia impasavyo jamaa, haya, na akufanyie; lakini ikiwa hataki yeye, basi mimi nitakufanyia impasavyo jamaa; BWANA aishivyo. Ulale wewe hadi asubuhi. Hivyo huyo mwanamke akalala miguuni pake hata asubuhi; akaondoka mapema asijaweza mtu kumtambua mwenziwe; maana Boazi amesema, Isijulikane kabisa ya kuwa mwanamke alifika penye uga. Tena alisema, Lete hapa shela yako uliyoivaa, uishike; naye akaishika; naye akampimia vipimo sita vya shayiri akamtwika; kisha huyo mwanamke akaenda zake mjini. Basi alipofika kwa mkwewe, huyo akamwuliza, Je! Mwanangu, imekuwaje? Akamwambia yote yule mtu aliyomfanyia. Akasema, Na vipimo hivi sita vya shayiri amenipa; maana aliniambia, Usiende kwa mkweo mikono mitupu. Naye mkwewe akasema, Basi, mwanangu, tulia; hadi utakapojua jinsi litakavyotukia jambo hili; kwa sababu mtu huyu hataridhika, asipolimaliza jambo hilo leo.
Ruthu 3:12-18 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Tena ndiyo kweli ya kuwa mimi ni wa jamaa yako aliye karibu; lakini kuna mtu wa jamaa aliye karibu kuliko mimi. Wewe ungoje usiku huu; kisha, asubuhi, kama akikubali kukufanyia impasavyo jamaa, haya, na akufanyie; lakini ikiwa hataki yeye, basi mimi nitakufanyia impasavyo jamaa; BWANA aishivyo. Ulale wewe hata asubuhi. Hivyo huyo mwanamke akalala miguuni pake hata asubuhi; akaondoka mapema asijaweza mtu kumtambua mwenziwe; maana Boazi amesema, Isijulikane kabisa ya kuwa mwanamke alifika penye uga. Tena alisema, Lete hapa shela yako uliyoivaa, uishike; naye akaishika; naye akampimia vipimo sita vya shayiri akamtwika; kisha huyo mwanamke akaenda zake mjini. Basi alipofika kwa mkwewe, huyo akamwuliza, Je! Mwanangu, imekuwaje? Akamwambia yote yule mtu aliyomfanyia. Akasema, Na vipimo hivi sita vya shayiri amenipa; maana akaniambia, Usiende kwa mkweo mikono mitupu. Naye mkwewe akasema, Basi, mwanangu, tulia; hata utakapojua jinsi litakavyotukia jambo hili; kwa sababu mtu huyu hataridhika, asipolimaliza jambo hilo leo.
Ruthu 3:12-18 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Ingawa ni kweli kwamba mimi ndiye jamaa aliye karibu, bado kuna mtu mwingine wa jamaa aliye karibu zaidi wa kukomboa kuliko mimi. Wewe kaa hapa usiku huu, kisha asubuhi akikubali kukukomboa, vyema, na akomboe. La sivyo, kama hayuko tayari, hakika kama BWANA aishivyo nitafanya hivyo. Lala hapa hadi asubuhi.” Hivyo huyo mwanamke akalala miguuni pake hadi asubuhi, akaondoka mapema pasipo mtu kuweza kumtambua mwenzake, maana Boazi alisema, “Isijulikane kabisa ya kuwa mwanamke alifika kwenye sakafu ya kupuria.” Pia akamwambia, “Leta shela yako uliyoivaa, uitandaze.” Naye alipoitandaza, akamimina vipimo sita vya shayiri, akamtwika. Kisha Ruthu akarudi zake mjini. Basi Ruthu alipofika kwa mama mkwe wake Naomi, akamuuliza, “Je, binti yangu, ilikuwaje huko?” Ndipo akamwelezea kila kitu Boazi alichomfanyia. Akaendelea kusema, “Amenipa shayiri vipimo sita, akaniambia, ‘Usiende kwa mama mkwe wako mikono mitupu.’ ” Kisha Naomi akasema, “Subiri binti yangu, hadi utakapojua kwamba hili jambo limeendaje. Kwa sababu mtu huyu hatatulia hadi akamilishe jambo hili leo.”