Ruthu 2:8-16
Ruthu 2:8-16 Biblia Habari Njema (BHN)
Ndipo Boazi akamwambia Ruthu, “Hebu sikiliza binti yangu. Usiende kuokota masuke mahali pengine ila katika shamba hili tu. Fuatana na wanawake hawa; angalia mahali wavunapo ujiunge nao. Nimewaonya vijana hawa wasikusumbue. Na ukiona kiu, nenda kwenye mitungi na unywe maji waliyoyateka hao vijana.” Hapo Ruthu akamwinamia Boazi mpaka chini kwa unyenyekevu, akamwambia, “Nimepataje kibali chako? Mbona unanihurumia na hali mimi ni mgeni tu?” Lakini Boazi akamjibu, “Nimeyasikia yote uliyomfanyia mama mkwe wako tangu mumeo afariki. Ninajua jinsi ulivyowaacha wazazi wako, ukaiacha nchi yako, na jinsi ulivyokuja kuishi kati ya watu ambao hukuwajua hapo awali. Mwenyezi-Mungu akujaze kwa yote uliyoyafanya. Mwenyezi-Mungu wa Israeli uliyemkimbilia akulinde chini ya mabawa yake, akupe thawabu kamilifu.” Ruthu akamjibu, “Bwana, wewe umenifanyia wema mkubwa sana. Ingawa mimi si kama mmoja wa watumishi wako, nimeridhika kwa kuwa umenifariji sana na kuongea nami kwa ukarimu.” Wakati wa chakula, Boazi alimkaribisha Ruthu akamwambia, “Karibu hapa, njoo ule mkate pia na uuchovye ndani ya divai.” Kwa hiyo Ruthu akaketi pamoja na wavunaji, na Boazi akampa nafaka iliyokaangwa, akala akashiba hata akabakiza. Na ikawa Ruthu alipoendelea kuokota mavuno, Boazi aliwaambia wafanyakazi wake, “Mwacheni akusanye hata mahali miganda ilipo wala msimkemee. Zaidi ya hapo, vuteni masuke kutoka katika matita na mumwachie aokote bila kumkaripia.”
Ruthu 2:8-16 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi Boazi akamwambia Ruthu, Mwanangu, sikiliza; wewe usiende kuokota masazo katika shamba lingine, wala usiondoke hapa, lakini ukae papa hapa karibu na wasichana wangu. Macho yako na yaelekee shamba walivunalo, ufuatane nao; je! Sikuwaagiza vijana wasikusumbue? Tena, ukiona kiu, uende kwenye vyombo, nawe uyanywe waliyoyateka hao vijana. Ndipo aliposujudia, akainama mpaka nchi, akamwambia, Jinsi gani nimepata kibali machoni pako, hata ukanifahamu, mimi niliye mgeni? Naye Boazi akajibu, akamwambia, Nimeelezwa sana yote uliyomfanyia mkweo, tangu alipokufa mumeo; na jinsi ulivyowaacha baba yako na mama yako, na nchi yako uliyozaliwa, ukawafikia watu usiowajua tangu hapo. BWANA akujaze kwa kazi yako, nawe upewe thawabu kamili na BWANA, Mungu wa Israeli, ambaye umekuja kukimbilia chini ya mabawa yake. Ndipo aliposema, Bwana wangu, na nipate kibali machoni pako; kwa sababu wewe umeniburudisha moyo, na kumwambia mema mjakazi wako, ingawa mimi si kama mmojawapo wa wajakazi wako. Tena wakati wa chakula huyo Boazi akamwambia, Karibu kwetu, ule katika mkate wetu, na ulichovye tonge lako katika siki yetu. Basi akaketi pamoja na wavunaji, nao wakampitishia bisi, naye akala akashiba, hata akasaza. Naye alipoinuka tena ili aende kuokota masazo, huyo Boazi aliwaagiza vijana wake akisema, Mwacheni aokote hata kati ya miganda, wala msimkemee. Tena mtoleeni kidogo katika matita na kukiacha, na akiokote, wala msimkataze.
Ruthu 2:8-16 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi Boazi akamwambia Ruthu, Mwanangu, sikiliza; wewe usiende kuokota masazo katika shamba lingine, wala usiondoke hapa, lakini ukae papa hapa karibu na wasichana wangu. Macho yako na yaelekee konde walivunalo, ufuatane nao; je! Sikuwaagiza vijana wasikuguse? Tena, ukiona kiu, uende kwenye vyombo, nawe uyanywe waliyoyateka hao vijana. Ndipo aliposujudia, akainama mpaka nchi, akamwambia, Jinsi gani nimepata kibali machoni pako, hata ukanifahamu, mimi niliye mgeni? Naye Boazi akajibu, akamwambia, Nimeelezwa sana yote uliyomfanyia mkweo, tangu alipokufa mumeo; na jinsi ulivyowaacha baba yako na mama yako, na nchi yako uliyozaliwa, ukawafikilia watu usiowajua tangu hapo. BWANA akujazi kwa kazi yako, nawe upewe thawabu kamili na BWANA, Mungu wa Israeli, ambaye umekuja kukimbilia chini ya mabawa yake. Ndipo aliposema, Bwana wangu, na nipate kibali machoni pako; kwa sababu wewe umeniburudisha moyo, na kumwambia mema mjakazi wako, ingawa mimi si kama mmojawapo wa wajakazi wako. Tena wakati wa chakula huyo Boazi akamwambia, Karibu kwetu, ule katika mkate wetu, na ulichovye tonge lako katika siki yetu. Basi akaketi pamoja na wavunaji, nao wakampitishia bisi, naye akala akashiba, hata akasaza. Naye alipoinuka tena ili aende kuokota masazo, huyo Boazi aliwaagiza vijana wake akisema, Mwacheni aokote hata kati ya miganda, wala msimkemee. Tena mtoleeni kidogo katika matita na kukiacha, na akiokote, wala msimkataze.
Ruthu 2:8-16 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Kisha Boazi akamwambia Ruthu, “Binti yangu, nisikilize. Usiende kuokota mabaki ya mavuno katika shamba lingine, na usiondoke hapa. Kaa hapa na hawa wajakazi wangu. Angalia shamba wanaume wanamovuna, ufuate nyuma yao. Nimewaamuru wanaume hawa wasikuguse. Wakati wowote ukiona kiu, nenda kwenye mitungi ukanywe maji waliyoyateka wanaume hawa.” Aliposikia hili, akasujudu, uso wake ukagusa chini, akamwambia, “Jinsi gani nimepata kibali machoni pako, hata ukanijali mimi mgeni?” Boazi akamjibu, “Nimeambiwa yote uliyomtendea mama mkwe wako tangu mume wako alipofariki, na jinsi ulivyomwacha baba yako na mama yako na nchi yako ulimozaliwa, ukaja kuishi na watu ambao hukuwafahamu awali. BWANA na akulipe kwa yale uliyoyatenda. Ubarikiwe kwa wingi na BWANA, Mungu wa Israeli, ambaye umekimbilia mabawani mwake.” Kisha Ruthu akasema, “Naomba niendelee kupata kibali machoni pako, bwana wangu. Kwa maana umenifariji na umezungumza kwa ukarimu na mjakazi wako, hata ingawa mimi si bora kama mmoja wa wajakazi wako.” Wakati wa chakula, Boazi akamwambia Ruthu, “Karibia hapa. Kula mkate na uchovye ndani ya siki.” Alipoketi pamoja na wavunaji, akampa nafaka zilizookwa. Akala kiasi alichotaka na kusaza. Alipoinuka ili kuokota mabaki ya nafaka, Boazi akawaagiza watu wake, “Hata kama atakusanya kati ya miganda, msimzuie. Badala yake, toeni masuke katika miganda, mwachieni ayaokote, na msimkemee.”