Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ruthu 2:1-23

Ruthu 2:1-23 Biblia Habari Njema (BHN)

Naomi alikuwa na ndugu aliyeitwa Boazi, wa ukoo wa Elimeleki mumewe. Huyo alikuwa mtu mashuhuri na tajiri. Siku moja, Ruthu Mmoabu alimwambia Naomi, “Niruhusu niende shambani kukusanya masalio ya mavuno. Nina hakika kumpata mtu ambaye ataniruhusu niokote nyuma yake.” Naomi akamwambia, “Haya, nenda binti yangu.” Basi Ruthu akaenda shambani, akawafuata wavunaji huku anayaokota masuke waliyoyaacha. Na kumbe akajikuta katika shamba la Boazi, yule wa ukoo wake Elimeleki. Baada ya muda, Boazi alifika kutoka Bethlehemu akawasalimu wavunaji, akasema, “Mwenyezi-Mungu awe nanyi.” Nao wakamjibu, “Mwenyezi-Mungu na akubariki.” Kisha Boazi akamwuliza msimamizi wa wavunaji, “Je, yule msichana ni nani?” Huyo kiongozi wa wavunaji akajibu, “Ni msichana Mmoabu aliyekuja pamoja na Naomi kutoka katika nchi ya Moabu. Aliniomba nimruhusu awafuate nyuma wavunaji huku akiokota masazo kati ya miganda. Basi alikuja na amefanya kazi tangu asubuhi na ni sasa tu amekwenda kupumzika kibandani.” Ndipo Boazi akamwambia Ruthu, “Hebu sikiliza binti yangu. Usiende kuokota masuke mahali pengine ila katika shamba hili tu. Fuatana na wanawake hawa; angalia mahali wavunapo ujiunge nao. Nimewaonya vijana hawa wasikusumbue. Na ukiona kiu, nenda kwenye mitungi na unywe maji waliyoyateka hao vijana.” Hapo Ruthu akamwinamia Boazi mpaka chini kwa unyenyekevu, akamwambia, “Nimepataje kibali chako? Mbona unanihurumia na hali mimi ni mgeni tu?” Lakini Boazi akamjibu, “Nimeyasikia yote uliyomfanyia mama mkwe wako tangu mumeo afariki. Ninajua jinsi ulivyowaacha wazazi wako, ukaiacha nchi yako, na jinsi ulivyokuja kuishi kati ya watu ambao hukuwajua hapo awali. Mwenyezi-Mungu akujaze kwa yote uliyoyafanya. Mwenyezi-Mungu wa Israeli uliyemkimbilia akulinde chini ya mabawa yake, akupe thawabu kamilifu.” Ruthu akamjibu, “Bwana, wewe umenifanyia wema mkubwa sana. Ingawa mimi si kama mmoja wa watumishi wako, nimeridhika kwa kuwa umenifariji sana na kuongea nami kwa ukarimu.” Wakati wa chakula, Boazi alimkaribisha Ruthu akamwambia, “Karibu hapa, njoo ule mkate pia na uuchovye ndani ya divai.” Kwa hiyo Ruthu akaketi pamoja na wavunaji, na Boazi akampa nafaka iliyokaangwa, akala akashiba hata akabakiza. Na ikawa Ruthu alipoendelea kuokota mavuno, Boazi aliwaambia wafanyakazi wake, “Mwacheni akusanye hata mahali miganda ilipo wala msimkemee. Zaidi ya hapo, vuteni masuke kutoka katika matita na mumwachie aokote bila kumkaripia.” Basi Ruthu aliendelea kuokota masuke mpaka jioni; na baada ya kupura hiyo shayiri alipata debe moja na zaidi. Kisha akachukua mavuno hayo hadi mjini na kumwonesha mama mkwe wake kiasi alichookota. Pia alikitoa kile chakula alichobakiza baada ya kushiba, akampa. Basi mkwewe akamwuliza, “Uliokota wapi haya yote? Je, ulikuwa katika shamba la nani? Heri huyo aliyekufadhili.” Hapo Ruthu akamwambia Naomi kwamba alikuwa amefanya kazi katika shamba la mtu aliyeitwa Boazi. Basi, Naomi akamwambia mkwewe, “Mwenyezi-Mungu ambariki Boazi! Mungu hutimiza daima ahadi zake kwa walio hai na waliokufa.” Kisha akaendelea kusema, “Huyo mtu ni ndugu yetu wa karibu na ni mmoja wa wale wenye wajibu wa kututunza.” Kisha Ruthu Mmoabu akasema, “Isitoshe, aliniambia nijiunge pamoja na wafanyakazi wake mpaka wamalize mavuno yote.” Basi, Naomi akamwambia Ruthu, “Naam binti yangu. Ni vyema kufanya kazi pamoja na wanawake wengine katika shamba la Boazi, kwa maana labda ungesumbuliwa kama ungekwenda katika shamba la mtu mwingine.” Kwa hiyo, Ruthu akafanya kazi nao, akaokota masuke mpaka mavuno ya ngano na shayiri yalipomalizika. Wakati huo wote alikuwa anakaa na mama mkwe wake.

Shirikisha
Soma Ruthu 2

Ruthu 2:1-23 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Basi huyo Naomi alikuwa na ndugu ya mumewe, mtu mkuu mwenye mali, wa jamaa yake Elimeleki, na jina lake aliitwa Boazi. Naye Ruthu Mmoabi akamwambia Naomi, Niruhusu niende shambani, niokote mabaki ya masuke nyuma yake yule ambaye nitaona kibali machoni pake. Akamwambia, Haya, mwanangu, nenda. Basi akaenda, akaja akaokota mabaki shambani nyuma ya wavunaji; na kwa bahati akafikia sehemu ya shamba la Boazi, ambaye alikuwa wa jamaa yake Elimeleki. Na tazama, Boazi akaja kutoka Bethlehemu na kuwaamkia wavunaji, akasema, BWANA akae nanyi. Nao wakamwitikia, BWANA na akubariki. Kisha Boazi akamwuliza mtumishi aliyewasimamia wavunaji, Na huyu je! Ni msichana wa nani? Yule msimamizi aliyewasimamia wavunaji akajibu, akasema, Ni yule msichana Mmoabi aliyerudi pamoja na Naomi, kutoka nchi ya Moabu; naye akasema, Tafadhali niruhusu kuokota mabaki, na kukusanya nyuma ya wavunaji kati ya miganda; basi akaja, naye ameshinda tangu asubuhi hadi sasa, isipokuwa alikaa nyumbani kitambo kidogo. Basi Boazi akamwambia Ruthu, Mwanangu, sikiliza; wewe usiende kuokota masazo katika shamba lingine, wala usiondoke hapa, lakini ukae papa hapa karibu na wasichana wangu. Macho yako na yaelekee shamba walivunalo, ufuatane nao; je! Sikuwaagiza vijana wasikusumbue? Tena, ukiona kiu, uende kwenye vyombo, nawe uyanywe waliyoyateka hao vijana. Ndipo aliposujudia, akainama mpaka nchi, akamwambia, Jinsi gani nimepata kibali machoni pako, hata ukanifahamu, mimi niliye mgeni? Naye Boazi akajibu, akamwambia, Nimeelezwa sana yote uliyomfanyia mkweo, tangu alipokufa mumeo; na jinsi ulivyowaacha baba yako na mama yako, na nchi yako uliyozaliwa, ukawafikia watu usiowajua tangu hapo. BWANA akujaze kwa kazi yako, nawe upewe thawabu kamili na BWANA, Mungu wa Israeli, ambaye umekuja kukimbilia chini ya mabawa yake. Ndipo aliposema, Bwana wangu, na nipate kibali machoni pako; kwa sababu wewe umeniburudisha moyo, na kumwambia mema mjakazi wako, ingawa mimi si kama mmojawapo wa wajakazi wako. Tena wakati wa chakula huyo Boazi akamwambia, Karibu kwetu, ule katika mkate wetu, na ulichovye tonge lako katika siki yetu. Basi akaketi pamoja na wavunaji, nao wakampitishia bisi, naye akala akashiba, hata akasaza. Naye alipoinuka tena ili aende kuokota masazo, huyo Boazi aliwaagiza vijana wake akisema, Mwacheni aokote hata kati ya miganda, wala msimkemee. Tena mtoleeni kidogo katika matita na kukiacha, na akiokote, wala msimkataze. Basi Ruthu akaokota mabaki shambani hadi jioni; kisha akazipura zile nafaka alizoziokota, zikawa yapata efa moja ya shayiri. Akajitwika, akaenda zake mjini. Akamwonesha mkwewe zile alizoziokota; akavitoa vile vyakula alivyovisaza alipokwisha kushiba, akampa. Basi mkwewe akamwuliza, Je! Umeokota wapi leo? Umefanya kazi wapi? Na abarikiwe yeye aliyekufahamu. Naye akamwarifu mkwewe ni nani ambaye alifanya kazi kwake, akasema, Yule mtu niliyefanya kazi kwake leo jina lake aitwa Boazi. Naye Naomi akamwambia mkwewe, Na abarikiwe huyo na BWANA, ambaye hakuuacha wema wake, wala kwa hao walio hai wala kwa waliokufa. Kisha Naomi akamwambia, Mtu huyu ni wa ukoo wetu, mmojawapo wa jamaa yetu aliye karibu. Naye Ruthu Mmoabi akasema, Naam, akaniambia, Ukae papa hapa karibu na watumishi wangu, hadi watakapomaliza mavuno yangu yote. Kisha Naomi akamwambia Ruthu mkwewe, Mwanangu, ni vizuri wewe ufuatane na wasichana wake, ili watu wasikusumbue katika shamba lingine lolote lile. Hivyo yeye akafuatana na wasichana wake Boazi na kuokota, hadi mwisho wa mavuno ya shayiri na mavuno ya ngano pia; naye alikuwa akikaa kwa mkwewe.

Shirikisha
Soma Ruthu 2

Ruthu 2:1-23 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Basi huyo Naomi alikuwa na ndugu ya mumewe, mtu mkuu mwenye mali, wa jamaa yake Elimeleki, na jina lake aliitwa Boazi. Naye Ruthu Mmoabi akamwambia Naomi, Sasa niende kondeni, niokote masazo ya masuke nyuma yake yule ambaye nitaona kibali machoni pake. Akamwambia, Haya, mwanangu, nenda. Basi akaenda, akaja akaokota masazo kondeni nyuma ya wavunaji; na bahati yake ikamtukia kwamba akaifika sehemu ya shamba iliyokuwa mali yake huyo Boazi, ambaye alikuwa wa jamaa yake Elimeleki. Na tazama, Boazi akaja kutoka Bethlehemu kawaamkia wavunaji, akasema, BWANA akae nanyi. Nao wakamwitikia, BWANA na akubariki. Kisha Boazi akamwuliza mtumishi aliyewasimamia wavunaji, Na huyu je! Ni msichana wa nani? Yule msimamizi aliyewasimamia wavunaji akajibu, akasema, Ni yule msichana Mmoabi aliyerudi pamoja na Naomi, kutoka nchi ya Moabu; naye akasema, Tafadhali niruhusu kuokota masazo, na kukusanya nyuma ya wavunaji kati ya miganda; basi akaja, naye ameshinda tangu asubuhi hata sasa, isipokuwa alikaa nyumbani kitambo kidogo. Basi Boazi akamwambia Ruthu, Mwanangu, sikiliza; wewe usiende kuokota masazo katika shamba lingine, wala usiondoke hapa, lakini ukae papa hapa karibu na wasichana wangu. Macho yako na yaelekee konde walivunalo, ufuatane nao; je! Sikuwaagiza vijana wasikuguse? Tena, ukiona kiu, uende kwenye vyombo, nawe uyanywe waliyoyateka hao vijana. Ndipo aliposujudia, akainama mpaka nchi, akamwambia, Jinsi gani nimepata kibali machoni pako, hata ukanifahamu, mimi niliye mgeni? Naye Boazi akajibu, akamwambia, Nimeelezwa sana yote uliyomfanyia mkweo, tangu alipokufa mumeo; na jinsi ulivyowaacha baba yako na mama yako, na nchi yako uliyozaliwa, ukawafikilia watu usiowajua tangu hapo. BWANA akujazi kwa kazi yako, nawe upewe thawabu kamili na BWANA, Mungu wa Israeli, ambaye umekuja kukimbilia chini ya mabawa yake. Ndipo aliposema, Bwana wangu, na nipate kibali machoni pako; kwa sababu wewe umeniburudisha moyo, na kumwambia mema mjakazi wako, ingawa mimi si kama mmojawapo wa wajakazi wako. Tena wakati wa chakula huyo Boazi akamwambia, Karibu kwetu, ule katika mkate wetu, na ulichovye tonge lako katika siki yetu. Basi akaketi pamoja na wavunaji, nao wakampitishia bisi, naye akala akashiba, hata akasaza. Naye alipoinuka tena ili aende kuokota masazo, huyo Boazi aliwaagiza vijana wake akisema, Mwacheni aokote hata kati ya miganda, wala msimkemee. Tena mtoleeni kidogo katika matita na kukiacha, na akiokote, wala msimkataze. Basi Ruthu akaokota masazo kondeni hata jioni; kisha akazipura zile nafaka alizoziokota, zikawa yapata efa moja ya shayiri. Akajitwika, akaenda zake mjini. Akamwonyesha mkwewe zile alizoziokota; akavitoa vile vyakula alivyovisaza alipokwisha kushiba, akampa. Basi mkwewe akamwuliza, Je! Umeokota wapi leo? Umefanya kazi wapi? Na abarikiwe yeye aliyekufahamu. Naye akamwarifu mkwewe ni nani ambaye alifanya kazi kwake, akasema, Yule mtu niliyefanya kazi kwake leo jina lake aitwa Boazi. Naye Naomi akamwambia mkwewe, Na abarikiwe huyo na BWANA, ambaye hakuuacha wema wake, wala kwa hao walio hai wala kwao waliokufa. Kisha Naomi akamwambia, Mtu huyu ni wa mbari yetu, mmojawapo wa jamaa yetu aliye karibu. Naye Ruthu Mmoabi akasema, Naam, akaniambia, Ukae papa hapa karibu na vijana wangu, hata watakapomaliza mavuno yangu yote. Kisha Naomi akamwambia Ruthu mkwewe, Mwanangu, ni vizuri wewe ufuatane na wasichana wake, wala watu wasikukute katika konde linginelo lote. Hivyo yeye akafuatana na wasichana wake Boazi na kuokota, hata mwisho wa mavuno ya shayiri na mavuno ya ngano pia; naye alikuwa akikaa kwa mkwewe.

Shirikisha
Soma Ruthu 2

Ruthu 2:1-23 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

Basi Naomi alikuwa na jamaa wa upande wa mume wake, kutoka ukoo wa Elimeleki, mtu maarufu ambaye aliitwa Boazi. Ruthu, Mmoabu, akamwambia Naomi, “Nitaenda mashambani nikaokote mabaki ya nafaka nyuma ya yule nitakayepata kibali machoni pake.” Naomi akamwambia, “Nenda, binti yangu.” Basi akaenda, akaokota mabaki ya nafaka mashambani nyuma ya wavunaji. Ikatokea kwamba alijikuta akifanya kazi kwenye shamba lililokuwa mali ya Boazi, ambaye alikuwa wa ukoo wa Elimeleki. Papo hapo Boazi akarudi kutoka Bethlehemu, akawasalimu wavunaji, akasema, “BWANA awe nanyi!” Nao wakamjibu, “BWANA akubariki.” Boazi akamuuliza msimamizi wa wavunaji, “Je, yule mwanamwali ni wa nani?” Msimamizi akamjibu, “Ni yule Mmoabu aliyerudi kutoka nchi ya Moabu pamoja na Naomi. Yeye aliomba, ‘Tafadhali niruhusu niokote na kukusanya miongoni mwa miganda nyuma ya wavunaji.’ Naye ameshinda shambani tangu asubuhi pasipo kupumzika, isipokuwa kwa muda mfupi kivulini.” Kisha Boazi akamwambia Ruthu, “Binti yangu, nisikilize. Usiende kuokota mabaki ya mavuno katika shamba lingine, na usiondoke hapa. Kaa hapa na hawa wajakazi wangu. Angalia shamba wanaume wanamovuna, ufuate nyuma yao. Nimewaamuru wanaume hawa wasikuguse. Wakati wowote ukiona kiu, nenda kwenye mitungi ukanywe maji waliyoyateka wanaume hawa.” Aliposikia hili, akasujudu, uso wake ukagusa chini, akamwambia, “Jinsi gani nimepata kibali machoni pako, hata ukanijali mimi mgeni?” Boazi akamjibu, “Nimeambiwa yote uliyomtendea mama mkwe wako tangu mume wako alipofariki, na jinsi ulivyomwacha baba yako na mama yako na nchi yako ulimozaliwa, ukaja kuishi na watu ambao hukuwafahamu awali. BWANA na akulipe kwa yale uliyoyatenda. Ubarikiwe kwa wingi na BWANA, Mungu wa Israeli, ambaye umekimbilia mabawani mwake.” Kisha Ruthu akasema, “Naomba niendelee kupata kibali machoni pako, bwana wangu. Kwa maana umenifariji na umezungumza kwa ukarimu na mjakazi wako, hata ingawa mimi si bora kama mmoja wa wajakazi wako.” Wakati wa chakula, Boazi akamwambia Ruthu, “Karibia hapa. Kula mkate na uchovye ndani ya siki.” Alipoketi pamoja na wavunaji, akampa nafaka zilizookwa. Akala kiasi alichotaka na kusaza. Alipoinuka ili kuokota mabaki ya nafaka, Boazi akawaagiza watu wake, “Hata kama atakusanya kati ya miganda, msimzuie. Badala yake, toeni masuke katika miganda, mwachieni ayaokote, na msimkemee.” Basi Ruthu akaokota masazo shambani hata jioni. Akatwanga ile shayiri aliyokusanya, ikajaa efa moja. Akaibeba na kuelekea mjini, naye mama mkwe wake akaona jinsi alivyoweza kuokota nafaka nyingi. Pia Ruthu akachukua kile alichobakiza baada ya kula na kushiba, akampa. Basi mkwewe akamuuliza, “Je, umeokota wapi leo? Umefanya kazi wapi? Abarikiwe mtu yule aliyekujali.” Ndipo Ruthu akamwambia mama mkwe wake kuhusu mtu ambaye alikuwa amemfanyia kazi katika shamba lake. Akasema, “Yule mtu niliyefanyia kazi kwake leo, anaitwa Boazi.” Naye Naomi akamwambia mkwewe, “BWANA ambariki! Hakuacha kuonesha fadhili zake kwa walio hai na kwa waliokufa.” Pia akamwambia, “Huyo mtu ni mmoja wa jamaa yetu wa karibu anayestahili kutukomboa.” Kisha Ruthu, Mmoabu, akasema, “Hata aliniambia, ‘Kaa pamoja na watumishi wangu hadi watakapomaliza kuvuna nafaka yangu yote.’ ” Kisha Naomi akamwambia Ruthu mkwewe, “Binti yangu, itakuwa vyema wewe ufuatane na wajakazi wake, kwa sababu katika shamba la mtu mwingine wanaweza kukudhuru.” Kwa hivyo Ruthu akafuatana na wajakazi wa Boazi, akaokota hadi mwisho wa mavuno ya shayiri na ya ngano. Naye aliishi na mama mkwe wake.

Shirikisha
Soma Ruthu 2