Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ruthu 2:1-12

Ruthu 2:1-12 Biblia Habari Njema (BHN)

Naomi alikuwa na ndugu aliyeitwa Boazi, wa ukoo wa Elimeleki mumewe. Huyo alikuwa mtu mashuhuri na tajiri. Siku moja, Ruthu Mmoabu alimwambia Naomi, “Niruhusu niende shambani kukusanya masalio ya mavuno. Nina hakika kumpata mtu ambaye ataniruhusu niokote nyuma yake.” Naomi akamwambia, “Haya, nenda binti yangu.” Basi Ruthu akaenda shambani, akawafuata wavunaji huku anayaokota masuke waliyoyaacha. Na kumbe akajikuta katika shamba la Boazi, yule wa ukoo wake Elimeleki. Baada ya muda, Boazi alifika kutoka Bethlehemu akawasalimu wavunaji, akasema, “Mwenyezi-Mungu awe nanyi.” Nao wakamjibu, “Mwenyezi-Mungu na akubariki.” Kisha Boazi akamwuliza msimamizi wa wavunaji, “Je, yule msichana ni nani?” Huyo kiongozi wa wavunaji akajibu, “Ni msichana Mmoabu aliyekuja pamoja na Naomi kutoka katika nchi ya Moabu. Aliniomba nimruhusu awafuate nyuma wavunaji huku akiokota masazo kati ya miganda. Basi alikuja na amefanya kazi tangu asubuhi na ni sasa tu amekwenda kupumzika kibandani.” Ndipo Boazi akamwambia Ruthu, “Hebu sikiliza binti yangu. Usiende kuokota masuke mahali pengine ila katika shamba hili tu. Fuatana na wanawake hawa; angalia mahali wavunapo ujiunge nao. Nimewaonya vijana hawa wasikusumbue. Na ukiona kiu, nenda kwenye mitungi na unywe maji waliyoyateka hao vijana.” Hapo Ruthu akamwinamia Boazi mpaka chini kwa unyenyekevu, akamwambia, “Nimepataje kibali chako? Mbona unanihurumia na hali mimi ni mgeni tu?” Lakini Boazi akamjibu, “Nimeyasikia yote uliyomfanyia mama mkwe wako tangu mumeo afariki. Ninajua jinsi ulivyowaacha wazazi wako, ukaiacha nchi yako, na jinsi ulivyokuja kuishi kati ya watu ambao hukuwajua hapo awali. Mwenyezi-Mungu akujaze kwa yote uliyoyafanya. Mwenyezi-Mungu wa Israeli uliyemkimbilia akulinde chini ya mabawa yake, akupe thawabu kamilifu.”

Shirikisha
Soma Ruthu 2

Ruthu 2:1-12 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Basi huyo Naomi alikuwa na ndugu ya mumewe, mtu mkuu mwenye mali, wa jamaa yake Elimeleki, na jina lake aliitwa Boazi. Naye Ruthu Mmoabi akamwambia Naomi, Niruhusu niende shambani, niokote mabaki ya masuke nyuma yake yule ambaye nitaona kibali machoni pake. Akamwambia, Haya, mwanangu, nenda. Basi akaenda, akaja akaokota mabaki shambani nyuma ya wavunaji; na kwa bahati akafikia sehemu ya shamba la Boazi, ambaye alikuwa wa jamaa yake Elimeleki. Na tazama, Boazi akaja kutoka Bethlehemu na kuwaamkia wavunaji, akasema, BWANA akae nanyi. Nao wakamwitikia, BWANA na akubariki. Kisha Boazi akamwuliza mtumishi aliyewasimamia wavunaji, Na huyu je! Ni msichana wa nani? Yule msimamizi aliyewasimamia wavunaji akajibu, akasema, Ni yule msichana Mmoabi aliyerudi pamoja na Naomi, kutoka nchi ya Moabu; naye akasema, Tafadhali niruhusu kuokota mabaki, na kukusanya nyuma ya wavunaji kati ya miganda; basi akaja, naye ameshinda tangu asubuhi hadi sasa, isipokuwa alikaa nyumbani kitambo kidogo. Basi Boazi akamwambia Ruthu, Mwanangu, sikiliza; wewe usiende kuokota masazo katika shamba lingine, wala usiondoke hapa, lakini ukae papa hapa karibu na wasichana wangu. Macho yako na yaelekee shamba walivunalo, ufuatane nao; je! Sikuwaagiza vijana wasikusumbue? Tena, ukiona kiu, uende kwenye vyombo, nawe uyanywe waliyoyateka hao vijana. Ndipo aliposujudia, akainama mpaka nchi, akamwambia, Jinsi gani nimepata kibali machoni pako, hata ukanifahamu, mimi niliye mgeni? Naye Boazi akajibu, akamwambia, Nimeelezwa sana yote uliyomfanyia mkweo, tangu alipokufa mumeo; na jinsi ulivyowaacha baba yako na mama yako, na nchi yako uliyozaliwa, ukawafikia watu usiowajua tangu hapo. BWANA akujaze kwa kazi yako, nawe upewe thawabu kamili na BWANA, Mungu wa Israeli, ambaye umekuja kukimbilia chini ya mabawa yake.

Shirikisha
Soma Ruthu 2

Ruthu 2:1-12 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Basi huyo Naomi alikuwa na ndugu ya mumewe, mtu mkuu mwenye mali, wa jamaa yake Elimeleki, na jina lake aliitwa Boazi. Naye Ruthu Mmoabi akamwambia Naomi, Sasa niende kondeni, niokote masazo ya masuke nyuma yake yule ambaye nitaona kibali machoni pake. Akamwambia, Haya, mwanangu, nenda. Basi akaenda, akaja akaokota masazo kondeni nyuma ya wavunaji; na bahati yake ikamtukia kwamba akaifika sehemu ya shamba iliyokuwa mali yake huyo Boazi, ambaye alikuwa wa jamaa yake Elimeleki. Na tazama, Boazi akaja kutoka Bethlehemu kawaamkia wavunaji, akasema, BWANA akae nanyi. Nao wakamwitikia, BWANA na akubariki. Kisha Boazi akamwuliza mtumishi aliyewasimamia wavunaji, Na huyu je! Ni msichana wa nani? Yule msimamizi aliyewasimamia wavunaji akajibu, akasema, Ni yule msichana Mmoabi aliyerudi pamoja na Naomi, kutoka nchi ya Moabu; naye akasema, Tafadhali niruhusu kuokota masazo, na kukusanya nyuma ya wavunaji kati ya miganda; basi akaja, naye ameshinda tangu asubuhi hata sasa, isipokuwa alikaa nyumbani kitambo kidogo. Basi Boazi akamwambia Ruthu, Mwanangu, sikiliza; wewe usiende kuokota masazo katika shamba lingine, wala usiondoke hapa, lakini ukae papa hapa karibu na wasichana wangu. Macho yako na yaelekee konde walivunalo, ufuatane nao; je! Sikuwaagiza vijana wasikuguse? Tena, ukiona kiu, uende kwenye vyombo, nawe uyanywe waliyoyateka hao vijana. Ndipo aliposujudia, akainama mpaka nchi, akamwambia, Jinsi gani nimepata kibali machoni pako, hata ukanifahamu, mimi niliye mgeni? Naye Boazi akajibu, akamwambia, Nimeelezwa sana yote uliyomfanyia mkweo, tangu alipokufa mumeo; na jinsi ulivyowaacha baba yako na mama yako, na nchi yako uliyozaliwa, ukawafikilia watu usiowajua tangu hapo. BWANA akujazi kwa kazi yako, nawe upewe thawabu kamili na BWANA, Mungu wa Israeli, ambaye umekuja kukimbilia chini ya mabawa yake.

Shirikisha
Soma Ruthu 2

Ruthu 2:1-12 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

Basi Naomi alikuwa na jamaa wa upande wa mume wake, kutoka ukoo wa Elimeleki, mtu maarufu ambaye aliitwa Boazi. Ruthu, Mmoabu, akamwambia Naomi, “Nitaenda mashambani nikaokote mabaki ya nafaka nyuma ya yule nitakayepata kibali machoni pake.” Naomi akamwambia, “Nenda, binti yangu.” Basi akaenda, akaokota mabaki ya nafaka mashambani nyuma ya wavunaji. Ikatokea kwamba alijikuta akifanya kazi kwenye shamba lililokuwa mali ya Boazi, ambaye alikuwa wa ukoo wa Elimeleki. Papo hapo Boazi akarudi kutoka Bethlehemu, akawasalimu wavunaji, akasema, “BWANA awe nanyi!” Nao wakamjibu, “BWANA akubariki.” Boazi akamuuliza msimamizi wa wavunaji, “Je, yule mwanamwali ni wa nani?” Msimamizi akamjibu, “Ni yule Mmoabu aliyerudi kutoka nchi ya Moabu pamoja na Naomi. Yeye aliomba, ‘Tafadhali niruhusu niokote na kukusanya miongoni mwa miganda nyuma ya wavunaji.’ Naye ameshinda shambani tangu asubuhi pasipo kupumzika, isipokuwa kwa muda mfupi kivulini.” Kisha Boazi akamwambia Ruthu, “Binti yangu, nisikilize. Usiende kuokota mabaki ya mavuno katika shamba lingine, na usiondoke hapa. Kaa hapa na hawa wajakazi wangu. Angalia shamba wanaume wanamovuna, ufuate nyuma yao. Nimewaamuru wanaume hawa wasikuguse. Wakati wowote ukiona kiu, nenda kwenye mitungi ukanywe maji waliyoyateka wanaume hawa.” Aliposikia hili, akasujudu, uso wake ukagusa chini, akamwambia, “Jinsi gani nimepata kibali machoni pako, hata ukanijali mimi mgeni?” Boazi akamjibu, “Nimeambiwa yote uliyomtendea mama mkwe wako tangu mume wako alipofariki, na jinsi ulivyomwacha baba yako na mama yako na nchi yako ulimozaliwa, ukaja kuishi na watu ambao hukuwafahamu awali. BWANA na akulipe kwa yale uliyoyatenda. Ubarikiwe kwa wingi na BWANA, Mungu wa Israeli, ambaye umekimbilia mabawani mwake.”

Shirikisha
Soma Ruthu 2