Waroma 8:24-28
Waroma 8:24-28 Biblia Habari Njema (BHN)
Maana kwa matumaini hayo sisi tumekombolewa. Lakini tumaini halina maana ikiwa tunakiona kile tunachotumainia. Maana ni nani anayetumaini kile ambacho tayari anakiona? Kama tunakitumaini kile ambacho hatujakiona bado, basi, tunakingojea kwa uvumilivu. Hali kadhalika, naye Roho anatusaidia katika udhaifu wetu. Maana hatujui inavyotupasa kuomba; lakini Roho mwenyewe anatuombea kwa Mungu kwa mlio wa huzuni usioelezeka. Naye Mungu aonaye mpaka ndani ya mioyo ya watu, anajua fikira ya huyo Roho; kwani huyo Roho huwaombea watu wa Mungu kufuatana na mapenzi ya Mungu. Tunajua kwamba, katika mambo yote, Mungu hufanya kazi na kuifanikisha pamoja na wote wampendao, yaani wale aliowaita kadiri ya kusudi lake.
Waroma 8:24-28 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kwa maana tuliokolewa kwa tumaini; lakini kitu kilichotumainiwa kikionekana, hakiwi tumaini tena. Kwa maana ni nani anayekitumainia kile akionacho? Bali tukikitumainia kitu tusichokiona, twakingojea kwa subira. Kadhalika Roho naye hutusaidia udhaifu wetu, kwa maana hatujui kuomba jinsi itupasavyo, lakini Roho mwenyewe hutuombea kwa kuugua kusikoweza kutamkwa. Na yeye aichunguzaye mioyo aijua nia ya Roho ilivyo, kwa kuwa huwaombea watakatifu kama apendavyo Mungu. Nasi twajua ya kuwa katika mambo yote Mungu hufanya kazi pamoja na wale wampendao katika kuwapatia mema, yaani, wale walioitwa kwa kusudi lake.
Waroma 8:24-28 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Kwa maana tuliokolewa kwa taraja; lakini kitu kilichotarajiwa kikionekana, hakuna taraja tena. Kwa maana ni nani anayekitarajia kile akionacho? Bali tukikitarajia kitu tusichokiona, twakingojea kwa saburi. Kadhalika Roho naye hutusaidia udhaifu wetu, kwa maana hatujui kuomba jinsi itupasavyo, lakini Roho mwenyewe hutuombea kwa kuugua kusikoweza kutamkwa. Na yeye aichunguzaye mioyo aijua nia ya Roho ilivyo, kwa kuwa huwaombea watakatifu kama apendavyo Mungu. Nasi twajua ya kuwa katika mambo yote Mungu hufanya kazi pamoja na wale wampendao katika kuwapatia mema, yaani, wale walioitwa kwa kusudi lake.
Waroma 8:24-28 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Kwa kuwa tuliokolewa kwa tumaini hili. Lakini kama kinachotumainiwa kikionekana, basi hakiwi tumaini tena. Je, kuna mtu anayetumaini kupata kitu alicho nacho tayari? Lakini tunapotumaini kupata kitu ambacho hatuna, basi twakingojea kwa saburi. Vivyo hivyo, Roho hutusaidia katika udhaifu wetu, kwa sababu hatujui kuomba ipasavyo. Lakini Roho mwenyewe hutuombea kwa uchungu usioweza kutamkwa. Naye Mungu aichunguzaye mioyo, anaijua nia ya Roho, kwa sababu Roho huwaombea watakatifu sawasawa na mapenzi ya Mungu. Nasi tunajua ya kuwa katika mambo yote Mungu hutenda kazi pamoja na wote wanaompenda, yaani wale walioitwa kwa kusudi lake, ili kuwaletea mema.