Waroma 7:1-6
Waroma 7:1-6 Biblia Habari Njema (BHN)
Ndugu zangu, bila shaka mtaelewa yafuatayo, maana ninawazungumzia watu wanaojua sheria. Sheria humtawala mtu wakati akiwa hai. Mathalani: Mwanamke aliyeolewa anafungwa na sheria muda wote mumewe anapokuwa hai; lakini mumewe akifa, hiyo sheria haimtawali tena huyo mwanamke. Hivyo mwanamke huyo akiishi na mwanamume mwingine wakati mumewe yungali hai, ataitwa mzinzi; lakini mumewe akifa, mwanamke huyo yu huru kisheria, na akiolewa na mwanamume mwingine, yeye si mzinzi. Hali kadhalika nyinyi ndugu zangu: Nyinyi pia mmekufa kuhusu sheria kwa kuwa nyinyi ni sehemu ya mwili wa Kristo; sasa mmekuwa wake yeye aliyefufuliwa kutoka kwa wafu ili tupate kuzaa matunda mema kwa ajili ya Mungu. Maana, tulipokuwa tukiishi kimaumbile tu, tamaa mbaya zikichochewa na sheria, zilifanya kazi katika miili yetu, na kuchuma pato la kifo. Lakini sasa tumekuwa huru kutoka vifungo vya sheria, kwa sababu tumekufa kuhusu lile jambo lililotufanya sisi watumwa. Sasa tunatumikia kufuatana na maisha mapya ya Roho, na si kufuatana na hali ile ya kale ya sheria iliyoandikwa.
Waroma 7:1-6 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ndugu zangu, hamjui (maana nasema na hao waijuao sheria) ya kuwa torati humtawala mtu wakati anapokuwa yu hai? Kwa maana mwanamke aliye na mume amefungwa na sheria kwa yule mume wakati anapokuwa yu hai; bali yule mume akifa, amefunguliwa ile sheria ya mume. Basi wakati mumewe awapo hai, kama akiwa na mume mwingine huitwa mzinzi. Ila mumewe akifa, amekuwa huru, hafungwi na sheria hiyo, hata yeye si mzinzi, ajapoolewa na mume mwingine. Kadhalika, ndugu zangu, ninyi pia mmeifia torati, kwa njia ya mwili wa Kristo, mpate kuwa mali ya mwingine, yeye aliyefufuka katika wafu, kusudi tumzalie Mungu matunda. Kwa maana tulipokuwa katika hali ya mwili, tamaa za dhambi, zilizokuwako kwa sababu ya torati, zilitenda kazi katika viungo vyetu hata mkaizalia mauti mazao. Bali sasa tumefunguliwa katika torati, tumeifia hali ile iliyotupinga, ili sisi tupate kutumika katika hali mpya ya roho, si katika hali ya zamani, ya andiko.
Waroma 7:1-6 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ndugu zangu, hamjui (maana nasema na hao waijuao sheria) ya kuwa torati humtawala mtu wakati anapokuwa yu hai? Kwa maana mwanamke aliye na mume amefungwa na sheria kwa yule mume wakati anapokuwa yu hai; bali akifa yule mume, amefunguliwa ile sheria ya mume. Basi wakati awapo hai mumewe, kama akiwa na mume mwingine huitwa mzinzi. Ila mumewe akifa, amekuwa huru, hafungwi na sheria hiyo, hata yeye si mzinzi, ajapoolewa na mume mwingine. Kadhalika, ndugu zangu, ninyi pia mmeifia torati, kwa njia ya mwili wa Kristo, mpate kuwa mali ya mwingine, yeye aliyefufuka katika wafu, kusudi tumzalie Mungu matunda. Kwa maana tulipokuwa katika hali ya mwili, tamaa za dhambi, zilizokuwako kwa sababu ya torati, zilitenda kazi katika viungo vyetu hata mkaizalia mauti mazao. Bali sasa tumefunguliwa katika torati, tumeifia hali ile iliyotupinga, ili sisi tupate kutumika katika hali mpya ya roho, si katika hali ya zamani, ya andiko.
Waroma 7:1-6 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Ndugu zangu, sasa ninasema na wale wanaoijua sheria: Je, hamjui kwamba sheria ina mamlaka juu ya mtu wakati akiwa hai tu? Kwa mfano, mwanamke aliyeolewa amefungwa kwa mumewe wakati akiwa hai, lakini yule mume akifa, yule mwanamke amefunguliwa kutoka sheria ya ndoa. Hivyo basi, kama huyo mwanamke ataolewa na mwanaume mwingine wakati mumewe akiwa bado yuko hai, ataitwa mzinzi. Lakini kama mumewe akifa, mwanamke huyo hafungwi tena na sheria ya ndoa, naye akiolewa na mtu mwingine haitwi mzinzi. Vivyo hivyo, ndugu zangu, ninyi mmeifia sheria kupitia kwa mwili wa Kristo, ili mweze kuwa mali ya mwingine, yeye ambaye alifufuliwa kutoka kwa wafu, ili tupate kuzaa matunda kwa Mungu. Kwa maana tulipokuwa tunatawaliwa na asili ya dhambi, tamaa za dhambi zilizochochewa na sheria zilikuwa zikitenda kazi katika miili yetu, hivyo tulizaa matunda ya mauti. Lakini sasa, kwa kufia kile kilichokuwa kimetufunga kwanza, tumewekwa huru kutokana na sheria ili tutumike katika njia mpya ya Roho, wala si katika njia ya zamani ya sheria iliyoandikwa.