Waroma 7:1-25
Waroma 7:1-25 Biblia Habari Njema (BHN)
Ndugu zangu, bila shaka mtaelewa yafuatayo, maana ninawazungumzia watu wanaojua sheria. Sheria humtawala mtu wakati akiwa hai. Mathalani: Mwanamke aliyeolewa anafungwa na sheria muda wote mumewe anapokuwa hai; lakini mumewe akifa, hiyo sheria haimtawali tena huyo mwanamke. Hivyo mwanamke huyo akiishi na mwanamume mwingine wakati mumewe yungali hai, ataitwa mzinzi; lakini mumewe akifa, mwanamke huyo yu huru kisheria, na akiolewa na mwanamume mwingine, yeye si mzinzi. Hali kadhalika nyinyi ndugu zangu: Nyinyi pia mmekufa kuhusu sheria kwa kuwa nyinyi ni sehemu ya mwili wa Kristo; sasa mmekuwa wake yeye aliyefufuliwa kutoka kwa wafu ili tupate kuzaa matunda mema kwa ajili ya Mungu. Maana, tulipokuwa tukiishi kimaumbile tu, tamaa mbaya zikichochewa na sheria, zilifanya kazi katika miili yetu, na kuchuma pato la kifo. Lakini sasa tumekuwa huru kutoka vifungo vya sheria, kwa sababu tumekufa kuhusu lile jambo lililotufanya sisi watumwa. Sasa tunatumikia kufuatana na maisha mapya ya Roho, na si kufuatana na hali ile ya kale ya sheria iliyoandikwa. Je, tuseme basi, kwamba sheria ni dhambi? Hata kidogo! Lakini bila sheria, mimi nisingalijua dhambi ni kitu gani. Maana, nisingalijua ni nini hasa kutamani mabaya, kama sheria isingalikuwa imesema: “Usitamani.” Kwa kuitumia hiyo amri, dhambi ilipata fursa ya kuamsha kila aina ya tamaa mbaya ndani yangu. Maana, bila sheria dhambi ni kitu kilichokufa. Wakati mmoja mimi nilikuwa hai mbali na sheria; lakini amri ilipokuja, dhambi ilifufuka, nami nikafa. Hiyo amri ambayo shabaha yake ilikuwa kuleta uhai, kwangu imeleta kifo. Maana, dhambi ilichukua fursa iliyopatiwa na amri hiyo, ikanidanganya na kuniua. Basi, sheria yenyewe ni takatifu, na amri yenyewe ni takatifu, ni ya haki na nzuri. Je, hii inamaanisha kwamba kile kilicho kizuri kimesababisha kifo changu? Hata kidogo! Ilivyo ni kwamba, dhambi, ili ionekane dhahiri kuwa ni dhambi, imekitumia kile kilicho kizuri na kusababisha kifo changu. Hivyo dhambi, kwa njia ya ile amri, ilijionesha kikamilifu jinsi ilivyo mbaya mno. Tunajua kwamba sheria ni ya kiroho, lakini mimi ni wa kidunia, mimi nimeuzwa kuwa mtumwa wa dhambi. Sielewi nifanyacho, maana kile ninachotaka sikifanyi, bali kile ninachokichukia ndicho nikifanyacho. Ikiwa basi, ninatenda kinyume cha matakwa yangu, hii inamaanisha kwamba nakubali kuwa ile sheria ni nzuri. Basi, si mimi hasa ninayefanya kitu hicho, bali ile dhambi inayokaa ndani yangu. Najua kwamba hamna jema lolote ndani yangu mimi, kadiri ya ubinadamu wangu. Kwa maana, ingawa nataka kufanya jambo jema, siwezi kulitekeleza. Yaani, badala ya kufanya lile jambo jema ninalotaka, nafanya lile baya nisilotaka. Basi, kama ninafanya kinyume cha matakwa yangu, hii inamaanisha kwamba si mimi ninayefanya hayo, bali ni ile dhambi inayokaa ndani yangu. Basi, nimegundua kanuni hii: Ninataka kufanya jema, lakini najikuta kwamba lile lililo baya ndilo ninalochagua. Ndani kabisa katika moyo wangu naifurahia sheria ya Mungu. Lakini naona kwamba kuna sheria nyingine inayofanya kazi mwilini mwangu, sheria ambayo inapingana na ile inayokubaliwa na akili yangu. Hiyo inanifanya niwe mtumwa wa sheria ya dhambi ifanyayo kazi mwilini mwangu. Maskini miye! Nani atakayeniokoa kutoka mwili huu unaonipeleka kifoni? Shukrani kwa Mungu afanyaye hivyo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo! Hii basi, ndiyo hali yangu: Mimi binafsi, kwa akili yangu, ninaitumikia sheria ya Mungu, lakini kwa mwili wangu ninaitumikia sheria ya dhambi.
Waroma 7:1-25 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ndugu zangu, hamjui (maana nasema na hao waijuao sheria) ya kuwa torati humtawala mtu wakati anapokuwa yu hai? Kwa maana mwanamke aliye na mume amefungwa na sheria kwa yule mume wakati anapokuwa yu hai; bali yule mume akifa, amefunguliwa ile sheria ya mume. Basi wakati mumewe awapo hai, kama akiwa na mume mwingine huitwa mzinzi. Ila mumewe akifa, amekuwa huru, hafungwi na sheria hiyo, hata yeye si mzinzi, ajapoolewa na mume mwingine. Kadhalika, ndugu zangu, ninyi pia mmeifia torati, kwa njia ya mwili wa Kristo, mpate kuwa mali ya mwingine, yeye aliyefufuka katika wafu, kusudi tumzalie Mungu matunda. Kwa maana tulipokuwa katika hali ya mwili, tamaa za dhambi, zilizokuwako kwa sababu ya torati, zilitenda kazi katika viungo vyetu hata mkaizalia mauti mazao. Bali sasa tumefunguliwa katika torati, tumeifia hali ile iliyotupinga, ili sisi tupate kutumika katika hali mpya ya roho, si katika hali ya zamani, ya andiko. Tusemeje, basi? Torati ni dhambi? La hasha! Lakini singalitambua dhambi ila kwa sheria; kwa kuwa singalijua kutamani, kama torati isingalisema, Usitamani. Lakini dhambi ilipata nafasi kwa ile amri, ikafanya ndani yangu kila namna ya kutamani. Kwa maana dhambi bila sheria imekufa. Nami nilikuwa hai hapo kwanza bila sheria; ila ilipokuja ile amri, dhambi ilihuika, nami nikafa. Nikaona ya kuwa ile amri iletayo uzima kwangu mimi ilileta mauti. Kwa maana dhambi, kwa kupata nafasi kwa ile amri, ilinidanganya, na kwa hiyo ikaniua. Basi torati ni takatifu, na ile amri ni takatifu, na ya haki, na njema. Basi je! Ile iliyo njema ilikuwa mauti kwangu mimi? La hasha! Bali dhambi, ili ionekane kuwa ni dhambi hasa, ilifanya mauti ndani yangu kwa njia ya ile njema, kusudi kwa ile amri dhambi izidi kuwa mbaya mno. Kwa maana twajua ya kuwa torati asili yake ni ya rohoni; bali mimi ni mtu wa mwilini, nimeuzwa chini ya dhambi. Maana sijui nifanyalo, kwa sababu lile nilipendalo, silitendi; bali lile nilichukialo ndilo ninalolitenda. Lakini kama nikilitenda lile nisilolipenda, naikiri ile sheria ya kuwa ni njema. Basi sasa si mimi nafsi yangu ninayetenda hilo, bali ni ile dhambi ikaayo ndani yangu Kwa maana najua ya kuwa ndani yangu, yaani, ndani ya mwili wangu, halikai neno jema; kwa kuwa kutaka nataka, bali kutenda lililo jema siwezi. Kwa maana lile jema nilipendalo, silitendi; bali lile baya nisilolipenda ndilo nilitendalo. Basi kama lile nisilolipenda ndilo nilitendalo, si mimi nafsi yangu nilitendaye, bali ni ile dhambi ikaayo ndani yangu. Basi nimeona sheria hii, ya kuwa kwangu mimi nitakaye kutenda lililo jema, lipo lililo baya. Kwa maana naifurahia sheria ya Mungu kwa utu wa ndani, lakini katika viungo vyangu naona sheria iliyo mbali, inapiga vita na ile sheria ya akili zangu, na kunifanya mateka wa ile sheria ya dhambi iliyo katika viungo vyangu. Ole wangu, maskini mimi! Ni nani atakayeniokoa na mwili huu wa mauti? Namshukuru Mungu, kwa Yesu Kristo Bwana wetu. Basi, kama ni hivyo, mimi mwenyewe kwa akili zangu naitumikia sheria ya Mungu, bali kwa mwili wangu sheria ya dhambi.
Waroma 7:1-25 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ndugu zangu, hamjui (maana nasema na hao waijuao sheria) ya kuwa torati humtawala mtu wakati anapokuwa yu hai? Kwa maana mwanamke aliye na mume amefungwa na sheria kwa yule mume wakati anapokuwa yu hai; bali akifa yule mume, amefunguliwa ile sheria ya mume. Basi wakati awapo hai mumewe, kama akiwa na mume mwingine huitwa mzinzi. Ila mumewe akifa, amekuwa huru, hafungwi na sheria hiyo, hata yeye si mzinzi, ajapoolewa na mume mwingine. Kadhalika, ndugu zangu, ninyi pia mmeifia torati, kwa njia ya mwili wa Kristo, mpate kuwa mali ya mwingine, yeye aliyefufuka katika wafu, kusudi tumzalie Mungu matunda. Kwa maana tulipokuwa katika hali ya mwili, tamaa za dhambi, zilizokuwako kwa sababu ya torati, zilitenda kazi katika viungo vyetu hata mkaizalia mauti mazao. Bali sasa tumefunguliwa katika torati, tumeifia hali ile iliyotupinga, ili sisi tupate kutumika katika hali mpya ya roho, si katika hali ya zamani, ya andiko. Tusemeje, basi? Torati ni dhambi? Hasha! Walakini singalitambua dhambi ila kwa sheria; kwa kuwa singalijua kutamani, kama torati isingalisema, Usitamani. Lakini dhambi ilipata nafasi kwa ile amri, ikafanya ndani yangu kila namna ya kutamani. Kwa maana dhambi bila sheria imekufa. Nami nalikuwa hai hapo kwanza bila sheria; ila ilipokuja ile amri, dhambi ilihuika, nami nikafa. Nikaona ile amri iletayo uzima ya kuwa kwangu mimi ilileta mauti. Kwa maana dhambi, kwa kupata nafasi kwa ile amri, ilinidanganya, na kwa hiyo ikaniua. Basi torati ni takatifu, na ile amri ni takatifu, na ya haki, na njema. Basi je! Ile iliyo njema ilikuwa mauti kwangu mimi? Hasha! Bali dhambi, ili ionekane kuwa ni dhambi hasa, ilifanya mauti ndani yangu kwa njia ya ile njema, kusudi kwa ile amri dhambi izidi kuwa mbaya mno. Kwa maana twajua ya kuwa torati asili yake ni ya rohoni; bali mimi ni mtu wa mwilini, nimeuzwa chini ya dhambi. Maana sijui nifanyalo, kwa sababu lile nilipendalo, silitendi; bali lile nilichukialo ndilo ninalolitenda. Lakini kama nikilitenda lile nisilolipenda, naikiri ile sheria ya kuwa ni njema. Basi sasa si mimi nafsi yangu ninayetenda hilo, bali ni ile dhambi ikaayo ndani yangu Kwa maana najua ya kuwa ndani yangu, yaani, ndani ya mwili wangu, halikai neno jema; kwa kuwa kutaka nataka, bali kutenda lililo jema sipati. Kwa maana lile jema nilipendalo, silitendi; bali lile baya nisilolipenda ndilo nilitendalo. Basi kama lile nisilolipenda ndilo nilitendalo, si mimi nafsi yangu nilitendaye, bali ni ile dhambi ikaayo ndani yangu. Basi nimeona sheria hii, ya kuwa kwangu mimi nitakaye kutenda lililo jema, lipo lililo baya. Kwa maana naifurahia sheria ya Mungu kwa utu wa ndani, lakini katika viungo vyangu naona sheria iliyo mbali, inapiga vita na ile sheria ya akili zangu, na kunifanya mateka ya ile sheria ya dhambi iliyo katika viungo vyangu. Ole wangu, maskini mimi! Ni nani atakayeniokoa na mwili huu wa mauti? Namshukuru Mungu, kwa Yesu Kristo Bwana wetu. Basi, kama ni hivyo, mimi mwenyewe kwa akili zangu naitumikia sheria ya Mungu, bali kwa mwili wangu sheria ya dhambi.
Waroma 7:1-25 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Ndugu zangu, sasa ninasema na wale wanaoijua sheria: Je, hamjui kwamba sheria ina mamlaka juu ya mtu wakati akiwa hai tu? Kwa mfano, mwanamke aliyeolewa amefungwa kwa mumewe wakati akiwa hai, lakini yule mume akifa, yule mwanamke amefunguliwa kutoka sheria ya ndoa. Hivyo basi, kama huyo mwanamke ataolewa na mwanaume mwingine wakati mumewe akiwa bado yuko hai, ataitwa mzinzi. Lakini kama mumewe akifa, mwanamke huyo hafungwi tena na sheria ya ndoa, naye akiolewa na mtu mwingine haitwi mzinzi. Vivyo hivyo, ndugu zangu, ninyi mmeifia sheria kupitia kwa mwili wa Kristo, ili mweze kuwa mali ya mwingine, yeye ambaye alifufuliwa kutoka kwa wafu, ili tupate kuzaa matunda kwa Mungu. Kwa maana tulipokuwa tunatawaliwa na asili ya dhambi, tamaa za dhambi zilizochochewa na sheria zilikuwa zikitenda kazi katika miili yetu, hivyo tulizaa matunda ya mauti. Lakini sasa, kwa kufia kile kilichokuwa kimetufunga kwanza, tumewekwa huru kutokana na sheria ili tutumike katika njia mpya ya Roho, wala si katika njia ya zamani ya sheria iliyoandikwa. Tuseme nini basi? Kwamba sheria ni dhambi? La, hasha! Lakini singejua dhambi isipokuwa kwa sababu ya sheria. Singejua kutamani ni nini kama sheria haikusema, “Usitamani.” Lakini dhambi ilipata nafasi katika amri, nayo ikazaa kila aina ya tamaa ndani yangu. Kwa maana pasipo sheria, dhambi imekufa. Mwanzoni nilikuwa hai pasipo sheria; lakini amri ilipokuja, dhambi ikawa hai, nami nikafa. Nikaona kwamba ile amri iliyokusudiwa kuleta uzima, ilileta mauti. Kwa maana dhambi kwa kupata nafasi katika amri, ilinidanganya, na kupitia katika hiyo amri, ikaniua. Hivyo basi, sheria yenyewe ni takatifu, na amri ni takatifu na ya haki, tena ni njema. Je, kile kilicho chema basi kilikuwa mauti kwangu? La, hasha! Lakini ili dhambi itambuliwe kuwa ni dhambi, ilileta mauti ndani yangu kupitia kile kilichokuwa chema, ili kupitia kwa amri dhambi izidi kuwa mbaya kupita kiasi. Kwa maana tunajua kwamba sheria ni ya kiroho, lakini mimi ni wa kimwili nikiwa nimeuzwa kwenye utumwa wa dhambi. Sielewi nitendalo, kwa maana lile ninalotaka kulitenda, silitendi, lakini ninatenda lile ninalolichukia. Basi kama ninatenda lile nisilotaka kutenda, ni kwamba ninakubali kuwa sheria ni njema. Lakini, kwa kweli si mimi tena nitendaye lile nisilotaka bali ni ile dhambi inayokaa ndani yangu. Kwa maana ninafahamu kwamba hakuna jema lolote linalokaa ndani yangu, yaani katika asili yangu ya dhambi. Kwa kuwa nina shauku ya kutenda lililo jema, lakini siwezi kulitenda. Sitendi lile jema nitakalo kutenda, bali lile baya nisilolitaka, ndilo nitendalo. Basi kama ninatenda lile nisilotaka kutenda, si mimi tena nifanyaye hivyo, bali ni ile dhambi inayokaa ndani yangu. Hivyo naiona sheria ikitenda kazi. Ninapotaka kutenda jema, jambo baya liko papo hapo. Kwa maana katika utu wangu wa ndani naifurahia sheria ya Mungu. Lakini ninaona kuna sheria nyingine inayotenda kazi katika viungo vya mwili wangu inayopigana vita dhidi ya ile sheria ya akili yangu. Sheria hii inanifanya mateka wa ile sheria ya dhambi inayofanya kazi katika viungo vya mwili wangu. Ole wangu, mimi maskini! Ni nani atakayeniokoa na mwili huu wa mauti? Namshukuru Mungu anayeniokoa kupitia kwa Yesu Kristo Bwana wetu! Hivyo basi, mimi mwenyewe kwa akili zangu ni mtumwa wa sheria ya Mungu, lakini katika asili ya dhambi ni mtumwa wa sheria ya dhambi.