Waroma 3:9-18
Waroma 3:9-18 Biblia Habari Njema (BHN)
Tuseme nini, basi? Je, sisi Wayahudi ni bora kuliko wengine? Hata kidogo! Kwa maana nimekwisha bainisha hapo mwanzoni kwamba Wayahudi na watu wa mataifa mengine wote wako chini ya utawala wa dhambi. Kama Maandiko Matakatifu yasemavyo: “Hakuna hata mmoja aliye mwadilifu! Hakuna mtu anayeelewa, wala anayemtafuta Mungu. Wote wamepotoka wote wamekosa; hakuna atendaye mema, hakuna hata mmoja. Makoo yao ni kama kaburi wazi, ndimi zao zimejaa udanganyifu, midomoni mwao mwatoka maneno yenye sumu kama ya nyoka. Vinywa vyao vimejaa laana chungu. Miguu yao iko mbioni kumwaga damu, popote waendapo husababisha maafa na mateso; njia ya amani hawaijui. Hawajali kabisa kumcha Mungu.”
Waroma 3:9-18 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ni nini basi? Tu bora kuliko wengine? La! Hata kidogo. Kwa maana tumekwisha kuwashitaki Wayahudi na Wagiriki ya kwamba pia wamekuwa chini ya dhambi; kama ilivyoandikwa, ya kwamba, Hakuna mwenye haki hata mmoja. Hakuna afahamuye; Hakuna amtafutaye Mungu. Wote wamepotoka, wameoza wote pia; Hakuna mtenda mema, la! Hata mmoja. Koo lao ni kaburi wazi, Kwa ndimi zao wametumia hila. Sumu ya fira iko chini ya midomo yao. Vinywa vyao vimejaa laana na uchungu. Miguu yao ina mbio kumwaga damu. Uharibifu na mashaka yamo njiani mwao. Wala njia ya amani hawakuijua. Kumcha Mungu hakupo machoni pao.
Waroma 3:9-18 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ni nini basi? Tu bora kuliko wengine? La! Hata kidogo. Kwa maana tumekwisha kuwashitaki Wayahudi na Wayunani ya kwamba pia wamekuwa chini ya dhambi; kama ilivyoandikwa, ya kwamba, Hakuna mwenye haki hata mmoja. Hakuna afahamuye; Hakuna amtafutaye Mungu. Wote wamepotoka, wameoza wote pia; Hakuna mtenda mema, la! Hata mmoja. Koo lao ni kaburi wazi, Kwa ndimi zao wametumia hila. Sumu ya fira i chini ya midomo yao. Vinywa vyao vimejaa laana na uchungu. Miguu yao ina mbio kumwaga damu. Uharibifu na mashaka yamo njiani mwao. Wala njia ya amani hawakuijua. Kumcha Mungu hakupo machoni pao.
Waroma 3:9-18 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Tusemeje basi? Je, sisi ni bora kuliko wao? La hasha! Kwa maana tumekwisha kuhakikisha kwa vyovyote kwamba Wayahudi na watu wa Mataifa wote wako chini ya nguvu ya dhambi. Kama ilivyoandikwa: “Hakuna mwenye haki, hakuna hata mmoja. Hakuna hata mmoja mwenye ufahamu, hakuna hata mmoja amtafutaye Mungu. Wote wamepotoka, wote wameoza pamoja; hakuna atendaye mema, naam, hakuna hata mmoja.” “Makoo yao ni makaburi wazi; kwa ndimi zao wao hufanya udanganyifu.” “Sumu ya nyoka iko midomoni mwao.” “Vinywa vyao vimejaa laana na uchungu.” “Miguu yao ina haraka kumwaga damu; maangamizi na taabu viko katika njia zao, wala njia ya amani hawaijui.” “Hakuna hofu ya Mungu machoni pao.”