Waroma 3:10-26
Waroma 3:10-26 Biblia Habari Njema (BHN)
Kama Maandiko Matakatifu yasemavyo: “Hakuna hata mmoja aliye mwadilifu! Hakuna mtu anayeelewa, wala anayemtafuta Mungu. Wote wamepotoka wote wamekosa; hakuna atendaye mema, hakuna hata mmoja. Makoo yao ni kama kaburi wazi, ndimi zao zimejaa udanganyifu, midomoni mwao mwatoka maneno yenye sumu kama ya nyoka. Vinywa vyao vimejaa laana chungu. Miguu yao iko mbioni kumwaga damu, popote waendapo husababisha maafa na mateso; njia ya amani hawaijui. Hawajali kabisa kumcha Mungu.” Tunajua kwamba sheria huwahusu walio chini ya sheria hiyo, hata hawawezi kuwa na kisingizio chochote, na ulimwengu wote uko chini ya hukumu ya Mungu. Maana hakuna binadamu yeyote anayekubaliwa kuwa mwadilifu mbele yake Mungu kwa kushika sheria; kazi ya sheria ni kumwonesha tu mtu kwamba ametenda dhambi. Lakini sasa, njia ya Mungu ya kuwakubali watu kuwa waadilifu imekwisha dhihirishwa, tena bila kutegemea sheria. Sheria na manabii hushuhudia jambo hili. Mungu huwakubali watu kuwa waadilifu kwa njia ya imani yao kwa Yesu Kristo; Mungu hufanya hivyo kwa wote wanaoamini; hakuna ubaguzi wowote. Watu wote wametenda dhambi na wametindikiwa utukufu wa Mungu. Lakini kwa zawadi ya neema ya Mungu, watu wote hukubaliwa kuwa waadilifu kwa njia ya Yesu Kristo anayewakomboa. Mungu alimtoa Yesu kusudi, kwa damu yake, awe njia ya kuwaondolea watu dhambi zao kwa imani yao kwake. Alifanya hivyo ili apate kuonesha kwamba yeye ni mwadilifu. Hapo zamani Mungu alikuwa mvumilivu bila kuzijali dhambi za watu; sasa, wakati huu, anazikabili dhambi za watu apate kuonesha uadilifu wake. Kwa namna hiyo Mungu mwenyewe huonesha kwamba yeye ni mwadilifu na kwamba humfanya kuwa mwadilifu mtu yeyote anayemwamini Yesu.
Waroma 3:10-26 Swahili Revised Union Version (SRUV)
kama ilivyoandikwa, ya kwamba, Hakuna mwenye haki hata mmoja. Hakuna afahamuye; Hakuna amtafutaye Mungu. Wote wamepotoka, wameoza wote pia; Hakuna mtenda mema, la! Hata mmoja. Koo lao ni kaburi wazi, Kwa ndimi zao wametumia hila. Sumu ya fira iko chini ya midomo yao. Vinywa vyao vimejaa laana na uchungu. Miguu yao ina mbio kumwaga damu. Uharibifu na mashaka yamo njiani mwao. Wala njia ya amani hawakuijua. Kumcha Mungu hakupo machoni pao. Basi twajua ya kuwa mambo yote inenayo torati huyanena kwa hao walio chini ya torati, ili kila kinywa kifumbwe, na ulimwengu wote uwe chini ya hukumu ya Mungu; kwa sababu hakuna mwenye mwili atakayehesabiwa haki mbele zake kwa matendo ya sheria; kwa maana kutambua dhambi huja kwa njia ya sheria. Lakini sasa, haki ya Mungu imedhihirika pasipo sheria; inashuhudiwa na Torati na Manabii; ni haki ya Mungu iliyo kwa njia ya imani katika Yesu Kristo kwa wote waaminio. Maana hakuna tofauti; kwa sababu wote wamefanya dhambi, na kupungukiwa na utukufu wa Mungu; wanahesabiwa haki bure kwa neema yake, kwa njia ya ukombozi ulio katika Kristo Yesu; ambaye Mungu amekwisha kumweka awe upatanisho kwa njia ya imani katika damu yake, ili aoneshe haki yake, kwa sababu ya kuziachilia katika ustahimili wa Mungu dhambi zote zilizotangulia kufanywa; apate kuonesha haki yake wakati huu, ili awe mwenye haki na mwenye kumhesabia haki yeye amwaminiye Yesu.
Waroma 3:10-26 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
kama ilivyoandikwa, ya kwamba, Hakuna mwenye haki hata mmoja. Hakuna afahamuye; Hakuna amtafutaye Mungu. Wote wamepotoka, wameoza wote pia; Hakuna mtenda mema, la! Hata mmoja. Koo lao ni kaburi wazi, Kwa ndimi zao wametumia hila. Sumu ya fira i chini ya midomo yao. Vinywa vyao vimejaa laana na uchungu. Miguu yao ina mbio kumwaga damu. Uharibifu na mashaka yamo njiani mwao. Wala njia ya amani hawakuijua. Kumcha Mungu hakupo machoni pao. Basi twajua ya kuwa mambo yote inenayo torati huyanena kwa hao walio chini ya torati, ili kila kinywa kifumbwe, na ulimwengu wote uwe chini ya hukumu ya Mungu; kwa sababu hakuna mwenye mwili atakayehesabiwa haki mbele zake kwa matendo ya sheria; kwa maana kutambua dhambi huja kwa njia ya sheria. Lakini sasa, haki ya Mungu imedhihirika pasipo sheria; inashuhudiwa na torati na manabii; ni haki ya Mungu iliyo kwa njia ya imani katika Yesu Kristo kwa wote waaminio. Maana hakuna tofauti; kwa sababu wote wamefanya dhambi, na kupungukiwa na utukufu wa Mungu; wanahesabiwa haki bure kwa neema yake, kwa njia ya ukombozi ulio katika Kristo Yesu; ambaye Mungu amekwisha kumweka awe upatanisho kwa njia ya imani katika damu yake, ili aonyeshe haki yake, kwa sababu ya kuziachilia katika ustahimili wa Mungu dhambi zote zilizotangulia kufanywa; apate kuonyesha haki yake wakati huu, ili awe mwenye haki na mwenye kumhesabu haki yeye amwaminiye Yesu.
Waroma 3:10-26 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Kama ilivyoandikwa: “Hakuna mwenye haki, hakuna hata mmoja. Hakuna hata mmoja mwenye ufahamu, hakuna hata mmoja amtafutaye Mungu. Wote wamepotoka, wote wameoza pamoja; hakuna atendaye mema, naam, hakuna hata mmoja.” “Makoo yao ni makaburi wazi; kwa ndimi zao wao hufanya udanganyifu.” “Sumu ya nyoka iko midomoni mwao.” “Vinywa vyao vimejaa laana na uchungu.” “Miguu yao ina haraka kumwaga damu; maangamizi na taabu viko katika njia zao, wala njia ya amani hawaijui.” “Hakuna hofu ya Mungu machoni pao.” Basi tunajua kwamba chochote sheria inachosema, inawaambia wale walio chini ya sheria ili kila kinywa kinyamazishwe na ulimwengu wote uwajibike kwa Mungu. Kwa hiyo hakuna binadamu hata mmoja atakayehesabiwa haki mbele za Mungu kwa matendo ya sheria, kwa maana sheria hutufanya tuitambue dhambi. Lakini sasa, haki ya Mungu imedhihirishwa pasipo sheria, ambayo Sheria na Manabii wanaishuhudia. Haki hii inayotoka kwa Mungu hupatikana kwa Yesu Kristo kwa wote wanaomwamini. Kwa maana hapo hakuna tofauti, kwa kuwa wote wametenda dhambi na kupungukiwa na utukufu wa Mungu, wanahesabiwa haki bure kwa neema yake kupitia kwa ukombozi ulio katika Kristo Yesu. Mungu alimtoa awe dhabihu ya upatanisho kupitia kwa imani katika damu yake. Alifanya hivi ili kuonesha haki yake, kwa sababu kwa ustahimili wake, Mungu aliziachilia bila adhabu zile dhambi zilizotangulia kufanywa. Alifanya hivyo ili kuonesha haki yake wakati huu, ili yeye awe mwenye haki na mwenye kumhesabia haki yule anayemwamini Yesu.