Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Waroma 3:1-26

Waroma 3:1-26 Biblia Habari Njema (BHN)

Basi, Myahudi ana nini zaidi kuliko watu wengine? Au kutahiriwa kuna faida gani? Naam, iko faida kwa kila upande. Kwanza, Mungu aliwakabidhi Wayahudi ujumbe wake. Lakini itakuwaje iwapo baadhi yao hawakuwa waaminifu? Je, jambo hilo litaondoa uaminifu wa Mungu? Hata kidogo! Mungu hubaki mwaminifu daima, ingawaje kila binadamu ni mwongo. Kama Maandiko Matakatifu yasemavyo: “Kila usemapo, maneno yako ni ya kweli; na katika hukumu, wewe hushinda.” Lakini, ikiwa uovu wetu unathibitisha kwamba Mungu anatenda kwa haki, tutasema nini? Je, tutasema kwamba anakosa haki akituadhibu? (Hapa naongea kibinadamu). Hata kidogo! Ingekuwa hivyo, Mungu angewezaje kuuhukumu ulimwengu? Labda utasema: “Ikiwa ukosefu wa uaminifu kwa upande wangu unamdhihirisha Mungu kuwa mwaminifu zaidi na hivyo kumpatia utukufu, basi singepaswa kuhukumiwa kuwa mwenye dhambi!” Ni sawa na kusema: Tufanye maovu ili tupate mema! Ndivyo wengine walivyotukashifu kwa kutushtaki kwamba tumefundisha hivyo. Watahukumiwa wanavyostahili! Tuseme nini, basi? Je, sisi Wayahudi ni bora kuliko wengine? Hata kidogo! Kwa maana nimekwisha bainisha hapo mwanzoni kwamba Wayahudi na watu wa mataifa mengine wote wako chini ya utawala wa dhambi. Kama Maandiko Matakatifu yasemavyo: “Hakuna hata mmoja aliye mwadilifu! Hakuna mtu anayeelewa, wala anayemtafuta Mungu. Wote wamepotoka wote wamekosa; hakuna atendaye mema, hakuna hata mmoja. Makoo yao ni kama kaburi wazi, ndimi zao zimejaa udanganyifu, midomoni mwao mwatoka maneno yenye sumu kama ya nyoka. Vinywa vyao vimejaa laana chungu. Miguu yao iko mbioni kumwaga damu, popote waendapo husababisha maafa na mateso; njia ya amani hawaijui. Hawajali kabisa kumcha Mungu.” Tunajua kwamba sheria huwahusu walio chini ya sheria hiyo, hata hawawezi kuwa na kisingizio chochote, na ulimwengu wote uko chini ya hukumu ya Mungu. Maana hakuna binadamu yeyote anayekubaliwa kuwa mwadilifu mbele yake Mungu kwa kushika sheria; kazi ya sheria ni kumwonesha tu mtu kwamba ametenda dhambi. Lakini sasa, njia ya Mungu ya kuwakubali watu kuwa waadilifu imekwisha dhihirishwa, tena bila kutegemea sheria. Sheria na manabii hushuhudia jambo hili. Mungu huwakubali watu kuwa waadilifu kwa njia ya imani yao kwa Yesu Kristo; Mungu hufanya hivyo kwa wote wanaoamini; hakuna ubaguzi wowote. Watu wote wametenda dhambi na wametindikiwa utukufu wa Mungu. Lakini kwa zawadi ya neema ya Mungu, watu wote hukubaliwa kuwa waadilifu kwa njia ya Yesu Kristo anayewakomboa. Mungu alimtoa Yesu kusudi, kwa damu yake, awe njia ya kuwaondolea watu dhambi zao kwa imani yao kwake. Alifanya hivyo ili apate kuonesha kwamba yeye ni mwadilifu. Hapo zamani Mungu alikuwa mvumilivu bila kuzijali dhambi za watu; sasa, wakati huu, anazikabili dhambi za watu apate kuonesha uadilifu wake. Kwa namna hiyo Mungu mwenyewe huonesha kwamba yeye ni mwadilifu na kwamba humfanya kuwa mwadilifu mtu yeyote anayemwamini Yesu.

Shirikisha
Soma Waroma 3

Waroma 3:1-26 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Basi Myahudi ana nini zaidi? Na kutahiriwa kwafaa nini? Kwafaa sana kwa kila njia. Kwanza kwa kuwa wamekabidhiwa mausia ya Mungu. Ni nini, basi, ikiwa baadhi yao hawakuamini? Je! Kutoamini kwao kutaubatili uaminifu wa Mungu? La hasha! Mungu aonekane kuwa kweli japo kila mtu ni mwongo; kama ilivyoandikwa, Ili ujulikane kuwa una haki katika maneno yako, Ukashinde uingiapo katika hukumu. Lakini, ikiwa udhalimu wetu waithibitisha haki ya Mungu, tuseme nini? Je! Mungu ni dhalimu aletaye ghadhabu? (Nasema kwa jinsi ya kibinadamu.) Hasha! Kwa maana hapo Mungu atawezaje kuuhukumu ulimwengu? Lakini, ikiwa kweli ya Mungu imezidi kudhihirisha utukufu wake kwa sababu ya uongo wangu, mbona mimi ningali nahukumiwa kuwa ni mwenye dhambi? Kwa nini tusiseme (kama tulivyosingiziwa, na kama wengine wanavyokaza kusema ya kwamba twasema hivyo), Na tufanye mabaya, ili yaje mema? Ambao kuhukumiwa kwao kuna haki. Ni nini basi? Tu bora kuliko wengine? La! Hata kidogo. Kwa maana tumekwisha kuwashitaki Wayahudi na Wagiriki ya kwamba pia wamekuwa chini ya dhambi; kama ilivyoandikwa, ya kwamba, Hakuna mwenye haki hata mmoja. Hakuna afahamuye; Hakuna amtafutaye Mungu. Wote wamepotoka, wameoza wote pia; Hakuna mtenda mema, la! Hata mmoja. Koo lao ni kaburi wazi, Kwa ndimi zao wametumia hila. Sumu ya fira iko chini ya midomo yao. Vinywa vyao vimejaa laana na uchungu. Miguu yao ina mbio kumwaga damu. Uharibifu na mashaka yamo njiani mwao. Wala njia ya amani hawakuijua. Kumcha Mungu hakupo machoni pao. Basi twajua ya kuwa mambo yote inenayo torati huyanena kwa hao walio chini ya torati, ili kila kinywa kifumbwe, na ulimwengu wote uwe chini ya hukumu ya Mungu; kwa sababu hakuna mwenye mwili atakayehesabiwa haki mbele zake kwa matendo ya sheria; kwa maana kutambua dhambi huja kwa njia ya sheria. Lakini sasa, haki ya Mungu imedhihirika pasipo sheria; inashuhudiwa na Torati na Manabii; ni haki ya Mungu iliyo kwa njia ya imani katika Yesu Kristo kwa wote waaminio. Maana hakuna tofauti; kwa sababu wote wamefanya dhambi, na kupungukiwa na utukufu wa Mungu; wanahesabiwa haki bure kwa neema yake, kwa njia ya ukombozi ulio katika Kristo Yesu; ambaye Mungu amekwisha kumweka awe upatanisho kwa njia ya imani katika damu yake, ili aoneshe haki yake, kwa sababu ya kuziachilia katika ustahimili wa Mungu dhambi zote zilizotangulia kufanywa; apate kuonesha haki yake wakati huu, ili awe mwenye haki na mwenye kumhesabia haki yeye amwaminiye Yesu.

Shirikisha
Soma Waroma 3

Waroma 3:1-26 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Basi Myahudi ana ziada gani? Na kutahiriwa kwafaa nini? Kwafaa sana kwa kila njia. Kwanza kwa kuwa wamekabidhiwa mausia ya Mungu. Ni nini, basi, ikiwa baadhi yao hawakuamini? Je! Kutokuamini kwao kutaubatili uaminifu wa Mungu? Hasha! Mungu aonekane kuwa amini na kila mtu mwongo; kama ilivyoandikwa, Ili ujulike kuwa una haki katika maneno yako, Ukashinde uingiapo katika hukumu. Lakini, ikiwa udhalimu wetu waithibitisha haki ya Mungu, tuseme nini? Je! Mungu ni dhalimu aletaye ghadhabu? (Nasema kwa jinsi ya kibinadamu.) Hasha! Kwa maana hapo Mungu atawezaje kuuhukumu ulimwengu? Lakini, ikiwa kweli ya Mungu imezidi kudhihirisha utukufu wake kwa sababu ya uongo wangu, mbona mimi ningali nahukumiwa kuwa ni mwenye dhambi? Kwa nini tusiseme (kama tulivyosingiziwa, na kama wengine wanavyokaza kusema ya kwamba twasema hivyo), Na tufanye mabaya, ili yaje mema? Ambao kuhukumiwa kwao kuna haki. Ni nini basi? Tu bora kuliko wengine? La! Hata kidogo. Kwa maana tumekwisha kuwashitaki Wayahudi na Wayunani ya kwamba pia wamekuwa chini ya dhambi; kama ilivyoandikwa, ya kwamba, Hakuna mwenye haki hata mmoja. Hakuna afahamuye; Hakuna amtafutaye Mungu. Wote wamepotoka, wameoza wote pia; Hakuna mtenda mema, la! Hata mmoja. Koo lao ni kaburi wazi, Kwa ndimi zao wametumia hila. Sumu ya fira i chini ya midomo yao. Vinywa vyao vimejaa laana na uchungu. Miguu yao ina mbio kumwaga damu. Uharibifu na mashaka yamo njiani mwao. Wala njia ya amani hawakuijua. Kumcha Mungu hakupo machoni pao. Basi twajua ya kuwa mambo yote inenayo torati huyanena kwa hao walio chini ya torati, ili kila kinywa kifumbwe, na ulimwengu wote uwe chini ya hukumu ya Mungu; kwa sababu hakuna mwenye mwili atakayehesabiwa haki mbele zake kwa matendo ya sheria; kwa maana kutambua dhambi huja kwa njia ya sheria. Lakini sasa, haki ya Mungu imedhihirika pasipo sheria; inashuhudiwa na torati na manabii; ni haki ya Mungu iliyo kwa njia ya imani katika Yesu Kristo kwa wote waaminio. Maana hakuna tofauti; kwa sababu wote wamefanya dhambi, na kupungukiwa na utukufu wa Mungu; wanahesabiwa haki bure kwa neema yake, kwa njia ya ukombozi ulio katika Kristo Yesu; ambaye Mungu amekwisha kumweka awe upatanisho kwa njia ya imani katika damu yake, ili aonyeshe haki yake, kwa sababu ya kuziachilia katika ustahimili wa Mungu dhambi zote zilizotangulia kufanywa; apate kuonyesha haki yake wakati huu, ili awe mwenye haki na mwenye kumhesabu haki yeye amwaminiye Yesu.

Shirikisha
Soma Waroma 3

Waroma 3:1-26 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

Basi kuna faida gani kuwa Myahudi? Au kuna thamani gani katika tohara? Kuna faida kubwa kwa kila namna! Kwanza kabisa, Wayahudi wamekabidhiwa maneno halisi ya Mungu. Ingekuwaje kama wengine hawakuwa na imani? Je, kutokuamini kwao kungebatilisha uaminifu wa Mungu? La hasha! Mungu na aonekane mwenye haki, na kila mwanadamu kuwa mwongo, kama ilivyoandikwa: “Ili uthibitike kuwa wa kweli unaponena, na ukashinde unapotoa hukumu.” Lakini ikiwa uovu wetu unathibitisha haki ya Mungu waziwazi, tuseme nini basi? Je, Mungu kuileta ghadhabu yake juu yetu ni kwamba yeye si mwenye haki? (Nanena kibinadamu.) La hasha! Kama hivyo ndivyo ilivyo, Mungu angewezaje kuhukumu ulimwengu? Mtu aweza kuuliza, “Kama uongo wangu unasaidia kuonesha kweli ya Mungu na kuzidisha utukufu wake, kwa nini basi mimi nahukumiwa kuwa mwenye dhambi?” Nasi kwa nini tusiseme, kama wengine wanavyotusingizia kuwa tunasema, “Tutende maovu ili mema yapate kuja”? Wao wanastahili hukumu yao. Tusemeje basi? Je, sisi ni bora kuliko wao? La hasha! Kwa maana tumekwisha kuhakikisha kwa vyovyote kwamba Wayahudi na watu wa Mataifa wote wako chini ya nguvu ya dhambi. Kama ilivyoandikwa: “Hakuna mwenye haki, hakuna hata mmoja. Hakuna hata mmoja mwenye ufahamu, hakuna hata mmoja amtafutaye Mungu. Wote wamepotoka, wote wameoza pamoja; hakuna atendaye mema, naam, hakuna hata mmoja.” “Makoo yao ni makaburi wazi; kwa ndimi zao wao hufanya udanganyifu.” “Sumu ya nyoka iko midomoni mwao.” “Vinywa vyao vimejaa laana na uchungu.” “Miguu yao ina haraka kumwaga damu; maangamizi na taabu viko katika njia zao, wala njia ya amani hawaijui.” “Hakuna hofu ya Mungu machoni pao.” Basi tunajua kwamba chochote sheria inachosema, inawaambia wale walio chini ya sheria ili kila kinywa kinyamazishwe na ulimwengu wote uwajibike kwa Mungu. Kwa hiyo hakuna binadamu hata mmoja atakayehesabiwa haki mbele za Mungu kwa matendo ya sheria, kwa maana sheria hutufanya tuitambue dhambi. Lakini sasa, haki ya Mungu imedhihirishwa pasipo sheria, ambayo Sheria na Manabii wanaishuhudia. Haki hii inayotoka kwa Mungu hupatikana kwa Yesu Kristo kwa wote wanaomwamini. Kwa maana hapo hakuna tofauti, kwa kuwa wote wametenda dhambi na kupungukiwa na utukufu wa Mungu, wanahesabiwa haki bure kwa neema yake kupitia kwa ukombozi ulio katika Kristo Yesu. Mungu alimtoa awe dhabihu ya upatanisho kupitia kwa imani katika damu yake. Alifanya hivi ili kuonesha haki yake, kwa sababu kwa ustahimili wake, Mungu aliziachilia bila adhabu zile dhambi zilizotangulia kufanywa. Alifanya hivyo ili kuonesha haki yake wakati huu, ili yeye awe mwenye haki na mwenye kumhesabia haki yule anayemwamini Yesu.

Shirikisha
Soma Waroma 3