Waroma 2:1-29
Waroma 2:1-29 Biblia Habari Njema (BHN)
Basi, rafiki, kama unawahukumu wengine, huwezi kamwe kujitetea, hata kama wewe ni nani. Kwa maana, kwa kuwahukumu wengine, unajilaani wewe mwenyewe kwa vile nawe unayafanya mambo yaleyale unayohukumu. Tunajua kwamba hukumu ya Mungu kwa wale wanaofanya mambo kama hayo ni hukumu ya haki. Lakini wewe rafiki unayewahukumu wale wanaofanya mambo kama hayo hali wewe pia unayafanya, je unadhani utaiepa hukumu ya Mungu? Au labda unaudharau wema wake mkuu, uvumilivu wake na saburi yake, bila kutambua kwamba wema wake huo una shabaha ya kukuongoza upate kutubu? Lakini unao ugumu na ukaidi wa moyo, na hivyo unajirundikia adhabu kwa siku ile ya ghadhabu wakati hukumu ya haki ya Mungu itakapodhihirishwa. Siku hiyo Mungu atamlipa kila mmoja kufuatana na matendo yake. Wale wanaozingatia kutenda mema, kutafuta utukufu na heshima ya Mungu na kutokufa, watapata uhai wa milele. Lakini wale wengine wenye ubinafsi, wenye kukataa mambo ya haki na kufuata uovu, wataangukiwa na ghadhabu na hasira ya Mungu. Mateso na maumivu yatampata binadamu yeyote atendaye uovu. Yatawapata Wayahudi kwanza na watu wa mataifa mengine pia. Lakini Mungu atawapa utukufu, heshima na amani wale wanaotenda mema; Wayahudi kwanza, na watu wa mataifa mengine pia. Maana Mungu hambagui mtu yeyote. Wale wanaotenda dhambi bila kuijua sheria wataangamia ingawaje hawaijui sheria. Na wale wanaotenda dhambi wakiwa wanaijua sheria watahukumiwa kisheria. Maana sio wanaosikia sheria ndio walio waadilifu mbele ya Mungu, ila wenye kuitii sheria ndio watakaokubaliwa kuwa waadilifu. Mathalani: Watu wa mataifa mengine hawana sheria; lakini kila wanapotimiza matakwa ya sheria wakiongozwa na dhamiri zao, wao wenyewe wanakuwa kipimo cha sheria ingawa hawaijui sheria. Mwenendo wao unaonesha kwamba matakwa ya sheria yameandikwa mioyoni mwao. Dhamiri zao zinashuhudia pia jambo hilo, maana fikira zao mara nyingine huwashtaki, na mara nyingine huwatetea. Hivyo, kufuatana na hii Habari Njema ninayohubiri, ndivyo itakavyokuwa wakati Mungu atakapohukumu mambo ya siri ya binadamu kwa njia ya Yesu Kristo. Na wewe, je? Wewe mwenyewe unajiita Myahudi; unaitumainia sheria na kujivunia kuwa wa Mungu; kwa njia ya sheria unajua matakwa ya Mungu na unaweza kuchagua jambo jema; wewe unajiona kuwa kiongozi wa vipofu na mwanga kwa wale walio gizani; unajiona kuwa mkufunzi wa wajinga na mwalimu wa wale wasiokomaa bado. Unayo katika sheria picha kamili ya elimu na ukweli. Basi, wewe unawafundisha wengine; kwa nini hujifundishi wewe mwenyewe? Unawahubiria wengine wasiibe, lakini kumbe wewe mwenyewe unaiba. Unasema: “Msizini,” na huku wewe unazini; unachukia sanamu za miungu hali wewe unajitajirisha kwa kuiba katika nyumba za miungu. Kwa kujigamba ati unayo sheria ya Mungu, je huoni kwamba kwa kuivunja sheria unamdharau Mungu? Kama vile Maandiko Matakatifu yasemavyo: “Watu wa mataifa mengine wamelikufuru jina la Mungu kwa sababu yenu nyinyi Wayahudi!” Kutahiriwa kwako kutakuwa na maana kama ukiitii sheria. Lakini kama unaivunja sheria, basi, ni afadhali ungalibaki bila kutahiriwa. Kama mtu wa mataifa mengine ambaye hakutahiriwa akitimiza matakwa ya sheria, hakika atafikiriwa kana kwamba ametahiriwa. Watu wa mataifa mengine watakuhukumu wewe Myahudi kama ukiivunja sheria, ingawaje unayo maandishi ya sheria na umetahiriwa, hali wao wanaitii sheria ingawa hawakutahiriwa. Ndiyo kusema, si kila anayeonekana kwa nje kuwa Myahudi ni Myahudi wa kweli, wala mtu hawi Myahudi wa kweli ati kwa kuwa ametahiriwa kimwili. Myahudi wa kweli ni yule aliye Myahudi kwa ndani, yaani yule ambaye ametahiriwa moyoni. Hili ni jambo la Roho, na si jambo la maandishi ya sheria. Mtu wa namna hiyo anapata sifa, si kutoka kwa watu, bali kutoka kwa Mungu.
Waroma 2:1-29 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kwa hiyo, wewe mtu uwaye yote uhukumuye, huna udhuru; kwa maana katika hayo umhukumuyo mwingine wajihukumu mwenyewe kuwa na hatia; kwa maana wewe uhukumuye unafanya yale yale. Nasi tunajua ya kuwa hukumu ya Mungu ni ya kweli juu yao wafanyao hayo. Wewe binadamu, uwahukumuye wale wafanyao hayo na kutenda yayo hayo mwenyewe, je! Wadhani ya kwamba utajiepusha na hukumu ya Mungu? Au waudharau wingi wa wema wake na ustahimili wake na uvumilivu wake, usijue ya kuwa wema wa Mungu wakuvuta upate kutubu? Bali kwa kadiri ya ugumu wako, na kwa moyo wako usio na toba, wajiwekea akiba ya hasira kwa siku ile ya hasira na ufunuo wa hukumu ya haki ya Mungu, atakayemlipa kila mtu kwa kadiri ya matendo yake; wale ambao kwa subira katika kutenda mema wanatafuta utukufu na heshima na kutoharibika, watapewa uzima wa milele; na wale wenye fitina, wasioitii kweli, bali wakubalio dhuluma, watapata hasira na ghadhabu; dhiki na shida juu ya kila nafsi ya mwanadamu atendaye uovu, Myahudi kwanza na Mgiriki pia; bali utukufu na heshima na amani kwa kila mtu atendaye mema, Myahudi kwanza na Mgiriki pia; kwa maana hakuna upendeleo kwa Mungu. Kwa kuwa wote waliokosa pasipo sheria watapotea pasipo sheria, na wote waliokosa, wenye sheria, watahukumiwa kwa sheria. Kwa sababu sio wale waisikiao sheria walio wenye haki mbele za Mungu, bali ni wale waitendao sheria watakaohesabiwa haki. Kwa maana watu wa Mataifa wasio na sheria wafanyapo kwa tabia zao yaliyo ndani ya torati, hao wasio na sheria wamekuwa sheria kwa nafsi zao wenyewe. Hao waionesha kazi ya torati iliyoandikwa mioyoni mwao, dhamiri yao ikiwashuhudia, na mawazo yao, yenyewe kwa yenyewe, yakiwashitaki au kuwatetea; katika siku ile Mungu atakapozihukumu siri za wanadamu, sawasawa na Injili yangu, kwa Kristo Yesu. Lakini wewe, ukiwa unaitwa Myahudi na kuitegemea torati, na kujisifu katika Mungu, na kuyajua mapenzi yake, na kuyakubali mambo yaliyo bora, nawe umeelimishwa katika torati, na kujua hakika ya kuwa wewe mwenyewe u kiongozi wa vipofu, mwanga wao walio gizani, mkufunzi wa wajinga, mwalimu wa watoto wachanga, mwenye namna ya maarifa na ya kweli katika torati; basi wewe umfundishaye mwingine, je! Hujifundishi mwenyewe? Wewe uhubiriye kwamba mtu asiibe, waiba mwenyewe? Wewe usemaye kwamba mtu asizini, wazini mwenyewe? Wewe uchukiaye sanamu, wayaibia mahekalu? Wewe ujisifuye katika torati, wamvunjia Mungu heshima kwa kuiasi torati? Kwa maana jina la Mungu latukanwa katika Mataifa kwa ajili yenu, kama ilivyoandikwa. Kwa maana kutahiriwa kwafaa kama ukiwa mtendaji wa sheria, lakini ukiwa mvunjaji wa sheria kutahiriwa kwako kumekuwa kutotahiriwa. Basi ikiwa yeye asiyetahiriwa huyashika maagizo ya torati, je! Kutotahiriwa kwake hakutahesabiwa kuwa kutahiriwa? Na yeye asiyetahiriwa kwa asili, aishikaye torati, je! Hatakuhukumu wewe, uliye na kutahiriwa, ukaivunja torati? Maana yeye si Myahudi aliye Myahudi kwa nje tu, wala tohara siyo ile ya nje tu katika mwili; bali yeye ni Myahudi aliye Myahudi kwa ndani, na tohara ni ya moyo, katika roho, si katika andiko; ambaye sifa yake haitoki kwa wanadamu bali kwa Mungu.
Waroma 2:1-29 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Kwa hiyo, wewe mtu uwaye yote uhukumuye, huna udhuru; kwa maana katika hayo umhukumuyo mwingine wajihukumu mwenyewe kuwa na hatia; kwa maana wewe uhukumuye unafanya yale yale. Nasi twajua ya kuwa hukumu ya Mungu ni ya kweli juu yao wafanyao hayo. Wewe binadamu, uwahukumuye wale wafanyao hayo na kutenda yayo hayo mwenyewe, je! Wadhani ya kwamba utajiepusha na hukumu ya Mungu? Au waudharau wingi wa wema wake na ustahimili wake na uvumilivu wake, usijue ya kuwa wema wa Mungu wakuvuta upate kutubu? Bali kwa kadiri ya ugumu wako, na kwa moyo wako usio na toba, wajiwekea akiba ya hasira kwa siku ile ya hasira na ufunuo wa hukumu ya haki ya Mungu, atakayemlipa kila mtu kwa kadiri ya matendo yake; wale ambao kwa saburi katika kutenda mema wanatafuta utukufu na heshima na kutokuharibika, watapewa uzima wa milele; na wale wenye fitina, wasioitii kweli, bali wakubalio dhuluma, watapata hasira na ghadhabu; dhiki na shida juu ya kila nafsi ya mwanadamu atendaye uovu, Myahudi kwanza na Myunani pia; bali utukufu na heshima na amani kwa kila mtu atendaye mema, Myahudi kwanza na Myunani pia; kwa maana hakuna upendeleo kwa Mungu. Kwa kuwa wote waliokosa pasipo sheria watapotea pasipo sheria, na wote waliokosa, wenye sheria, watahukumiwa kwa sheria. Kwa sababu sio wale waisikiao sheria walio wenye haki mbele za Mungu, bali ni wale waitendao sheria watakaohesabiwa haki. Kwa maana watu wa Mataifa wasio na sheria wafanyapo kwa tabia zao yaliyo ndani ya torati, hao wasio na sheria wamekuwa sheria kwa nafsi zao wenyewe. Hao waionyesha kazi ya torati iliyoandikwa mioyoni mwao, dhamiri yao ikiwashuhudia, na mawazo yao, yenyewe kwa yenyewe, yakiwashitaki au kuwatetea; katika siku ile Mungu atakapozihukumu siri za wanadamu, sawasawa na injili yangu, kwa Kristo Yesu. Lakini wewe, ukiwa unaitwa Myahudi na kuitegemea torati, na kujisifu katika Mungu, na kuyajua mapenzi yake, na kuyakubali mambo yaliyo bora, nawe umeelimishwa katika torati, na kujua hakika ya kuwa wewe mwenyewe u kiongozi wa vipofu, mwanga wao walio gizani, mkufunzi wa wajinga, mwalimu wa watoto wachanga, mwenye namna ya maarifa na ya kweli katika torati; basi wewe umfundishaye mwingine, je! Hujifundishi mwenyewe? Wewe uhubiriye kwamba mtu asiibe, waiba mwenyewe? Wewe usemaye kwamba mtu asizini, wazini mwenyewe? Wewe uchukiaye sanamu, wateka mahekalu? Wewe ujisifuye katika torati, wamvunjia Mungu heshima kwa kuiasi torati? Kwa maana jina la Mungu latukanwa katika Mataifa kwa ajili yenu, kama ilivyoandikwa. Kwa maana kutahiriwa kwafaa kama ukiwa mtendaji wa sheria, lakini ukiwa mvunjaji wa sheria kutahiriwa kwako kumekuwa kutokutahiriwa. Basi ikiwa yeye asiyetahiriwa huyashika maagizo ya torati, je! Kutokutahiriwa kwake hakutahesabiwa kuwa kutahiriwa? Na yeye asiyetahiriwa kwa asili, aishikaye torati, je! Hatakuhukumu wewe, uliye na kutahiriwa, ukaihalifu torati? Maana yeye si Myahudi aliye Myahudi kwa nje tu, wala tohara siyo ile ya nje tu katika mwili; bali yeye ni Myahudi aliye Myahudi kwa ndani, na tohara ni ya moyo, katika roho, si katika andiko; ambaye sifa yake haitoki kwa wanadamu bali kwa Mungu.
Waroma 2:1-29 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Kwa hiyo huna udhuru wowote, wewe utoaye hukumu kwa mwingine, kwa maana katika jambo lolote unalowahukumu wengine, unajihukumu wewe mwenyewe kwa sababu wewe unayehukumu unafanya mambo hayo hayo. Basi tunajua kwamba hukumu ya Mungu dhidi ya wale wafanyao mambo kama hayo ni ya kweli. Hivyo wewe mwanadamu, unapotoa hukumu juu yao na bado unafanya mambo yale yale, unadhani utaepuka hukumu ya Mungu? Au waudharau wingi wa wema, ustahimili na uvumilivu wake, bila kujua kuwa wema wa Mungu wakuelekeza kwenye toba? Lakini kwa sababu ya ukaidi wenu na mioyo yenu isiyotaka kutubu, mnajiwekea akiba ya ghadhabu dhidi yenu wenyewe kwa siku ile ya ghadhabu ya Mungu, wakati hukumu yake ya haki itakapodhihirishwa. Kwa maana Mungu atamlipa kila mtu kulingana na matendo yake. Wale ambao kwa kuvumilia katika kutenda mema hutafuta utukufu, heshima na maisha yasiyoharibika, Mungu atawapa uzima wa milele. Lakini kwa wale wanaotafuta mambo yao wenyewe na wale wanaokataa kweli na kuzifuata njia mbaya, kutakuwa na ghadhabu na hasira ya Mungu. Kutakuwa na taabu na dhiki kwa kila mmoja atendaye maovu, Myahudi kwanza na mtu wa Mataifa pia, bali utukufu, heshima na amani kwa ajili ya kila mmoja atendaye mema, kwa Myahudi kwanza, kisha kwa mtu wa Mataifa. Kwa maana Mungu hana upendeleo. Watu wote waliotenda dhambi pasipo sheria wataangamia pasipo sheria, nao wote waliotenda dhambi chini ya sheria watahukumiwa kwa sheria. Kwa maana si wale wanaoisikia sheria ambao ni wenye haki mbele za Mungu, bali ni wale wanaoitii sheria ndio watakaohesabiwa haki. (Naam, wakati wa watu wa Mataifa, ambao hawana sheria, wanapofanya kwa asili mambo yatakiwayo na sheria, wao ni sheria kwa nafsi zao wenyewe, hata ingawa hawana sheria. Wao wanaonesha kwamba lile linalotakiwa na sheria limeandikwa kwenye mioyo yao, ambayo pia dhamiri zao zikiwashuhudia, nayo mawazo yao yenye kupingana yatawashtaki au kuwatetea.) Hili litatukia siku hiyo Mungu atakapozihukumu siri za wanadamu kupitia kwa Yesu Kristo, kama isemavyo Injili yangu. Tazama, wewe ukiwa unajiita Myahudi na kuitegemea sheria na kujisifia uhusiano wako na Mungu, kama unajua mapenzi ya Mungu na kukubali lililo bora kwa sababu umefundishwa na hiyo sheria, kama unatambua kuwa wewe ni kiongozi wa vipofu, na mwanga kwa wale walio gizani, mkufunzi wa wajinga na mwalimu wa watoto wachanga, kwa kuwa una maarifa ya kweli katika hiyo sheria, basi wewe, uwafundishaye wengine, mbona hujifunzi mwenyewe? Wewe uhubiriye kwamba mtu asiibe, wewe mwenyewe waiba? Wewe usemaye mtu asizini, wewe mwenyewe wazini? Wewe uchukiaye miungu ya sanamu, wafanya jambo la kumchukiza katika mahekalu? Wewe ujivuniaye sheria, wamwaibisha Mungu kwa kuvunja sheria? Kama ilivyoandikwa, “Kwa ajili yenu ninyi, Jina la Mungu linatukanwa miongoni mwa watu wa Mataifa.” Kutahiriwa kuna thamani ikiwa unatii sheria, lakini kama unavunja sheria, kutahiriwa kwako kumekuwa kutokutahiriwa. Hivyo, ikiwa wale wasiotahiriwa wanatimiza mambo ambayo sheria inataka, je, kutokutahiriwa kwao hakutahesabiwa kuwa sawa na kutahiriwa? Ndipo wale ambao hawakutahiriwa kimwili lakini wanaitii sheria watawahukumu ninyi, ambao ingawa mmetahiriwa na kuijua sana sheria ya Mungu iliyoandikwa, lakini mwaivunja. Kwa maana mtu si Myahudi kwa vile alivyo kwa nje, wala tohara ya kweli si kitu cha nje au cha kimwili. Lakini mtu ni Myahudi alivyo ndani, nayo tohara ya kweli ni jambo la moyoni, ni la Roho, wala si la sheria iliyoandikwa. Mtu kama huyo hapokei sifa kutoka kwa wanadamu bali kwa Mungu.