Waroma 15:23-29
Waroma 15:23-29 Biblia Habari Njema (BHN)
Lakini maadamu sasa nimemaliza kazi yangu pande hizi, na kwa kuwa kwa miaka mingi nimekuwa na nia kubwa ya kuja kwenu, natumaini kufanya hivyo sasa. Ningependa kuwaoneni nikiwa safarini kwenda Spania na kupata msaada wenu kwa safari hiyo baada ya kufurahia kuwa kwa muda pamoja nanyi. Lakini, kwa sasa nakwenda kuwahudumia watu wa Mungu kule Yerusalemu. Maana makanisa ya Makedonia na Akaya yemeamua kutoa mchango wao kuwasaidia watu wa Mungu walio maskini huko Yerusalemu. Wao wenyewe wameamua kufanya hivyo; lakini, kwa kweli, hilo ni jukumu lao kwa hao. Maana, ikiwa watu wa mataifa mengine wameshiriki baraka za kiroho za Wayahudi, wanapaswa nao pia kuwahudumia Wayahudi katika mahitaji yao ya kidunia. Nitakapokwisha tekeleza kazi hiyo na kuwakabidhi mchango huo uliokusanywa kwa ajili yao, nitawatembeleeni nyinyi nikiwa safarini kwenda Spania. Najua ya kuwa nikija kwenu nitawaletea wingi wa baraka za Kristo.
Waroma 15:23-29 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Lakini sasa, kwa kuwa sina wasaa tena pande hizi, tena kwa miaka mingi nimekuwa nikitamani kuja kwenu; wakati wowote nitakaosafiri kwenda Spania [nitakuja kwenu.] Kwa maana natarajia kuwaona ninyi nikiwa katika safari, na kusafirishwa nanyi, baada ya kukaa kwenu kwa muda. Ila sasa ninakwenda Yerusalemu, nikiwahudumia watakatifu; maana imewapendeza watu wa Makedonia na Akaya kutoa mchango kwa ajili ya watakatifu walio maskini huko Yerusalemu. Naam, imewapendeza, tena wamekuwa wadeni wao. Kwa maana ikiwa Mataifa wameyashiriki mambo yao ya roho, imewabidi kuwahudumia kwa mambo yao ya mwili. Basi nikiisha kuimaliza kazi hiyo, na kuwatilia mhuri tunda hilo, nitapitia kwenu, kwenda Spania. Nami najua ya kuwa nikija kwenu nitakuja kwa utimilifu wa baraka ya Kristo.
Waroma 15:23-29 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Lakini sasa, kwa kuwa sina wasaa tena pande hizi, tena tangu miaka mingi nina shauku kuja kwenu; wakati wo wote nitakaosafiri kwenda Spania [nitakuja kwenu.] Kwa maana nataraji kuwaona ninyi katika kusafiri kwangu, na kusafirishwa nanyi, moyo wangu ushibe kwenu kidogo. Ila sasa ninakwenda Yerusalemu, nikiwahudumu watakatifu; maana imewapendeza watu wa Makedonia na Akaya kufanya changizo kwa ajili ya watakatifu huko Yerusalemu walio maskini. Naam, imewapendeza, tena wamekuwa wadeni wao. Kwa maana ikiwa Mataifa wameyashiriki mambo yao ya roho, imewabidi kuwahudumu kwa mambo yao ya mwili. Basi nikiisha kuimaliza kazi hiyo, na kuwatilia muhuri tunda hilo, nitapitia kwenu, kwenda Spania. Nami najua ya kuwa nikija kwenu nitakuja kwa utimilifu wa baraka ya Kristo.
Waroma 15:23-29 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Lakini sasa kwa kuwa hakuna nafasi zaidi kwa ajili yangu katika sehemu hii, ninatamani kuja kwenu kama ambavyo nimekuwa na shauku kwa miaka mingi. Nimekusudia kufanya hivyo nitakapokuwa njiani kwenda Hispania. Natarajia kuwaona katika safari yangu na kusafirishwa nanyi hadi huko, baada ya kufurahia ushirika wenu kwa kitambo kidogo. Ila sasa niko njiani kuelekea Yerusalemu kwa ajili ya kuwahudumia watakatifu huko. Kwa kuwa imewapendeza watu wa Makedonia na Akaya kufanya changizo kwa ajili ya maskini walio miongoni mwa watakatifu huko Yerusalemu. Imewapendeza kufanya hivyo, naam, kwani ni wadeni wao. Kwa maana ikiwa watu wa Mataifa wameshiriki baraka za rohoni za Wayahudi, wao ni wadeni wa Wayahudi, ili Wayahudi nao washiriki baraka zao za mambo ya mwilini. Kwa hiyo baada ya kukamilisha kazi hii na kuhakikisha kuwa wamepokea kila kitu kilichokusanywa, nitapitia kwenu nikiwa njiani kwenda Hispania. Ninajua kwamba nitakapokuja kwenu, nitakuja na wingi wa baraka za Kristo.