Waroma 15:13-33
Waroma 15:13-33 Biblia Habari Njema (BHN)
Basi, Mungu aliye msingi wa matumaini, awajazeni furaha yote na amani kutokana na imani yenu; tumaini lenu lipate kuongezeka kwa nguvu ya Roho Mtakatifu. Ndugu zangu, mimi binafsi nina hakika kwamba nyinyi pia mmejaa wema, elimu yote, na mnaweza kushauriana nyinyi kwa nyinyi. Lakini nimewaandikia hapa na pale katika barua hii bila woga, nipate kuwakumbusheni juu ya mambo fulani. Nimefanya hivyo kwa sababu ya neema aliyonijalia Mungu ya kuwa mtumishi wa Yesu Kristo kwa watu wa mataifa. Ni jukumu langu la kikuhani kuihubiri Habari Njema ya Mungu ili watu wa mataifa mengine wapate kuwa tambiko inayokubaliwa na Mungu, tambiko iliyotakaswa na Roho Mtakatifu. Kwa hiyo, nikiwa nimeungana na Kristo Yesu, naweza kujivunia huduma yangu kwa ajili ya Mungu. Sithubutu kusema kitu kingine chochote isipokuwa tu kile ambacho Kristo Yesu amekifanya kwa kunitumia mimi ili watu wa mataifa wapate kutii. Amefanya hivyo kwa maneno na vitendo, kwa nguvu ya miujiza na maajabu, na kwa nguvu ya Roho wa Mungu. Basi, kwa kusafiri kila mahali, tangu kule Yerusalemu mpaka Iluriko, nimeihubiri kikamilifu Habari Njema ya Kristo. Nia yangu imekuwa daima kuihubiri Habari Njema popote pale ambapo jina la Kristo halijapata kusikika, nisije nikajenga juu ya msingi wa mtu mwingine. Kama yasemavyo Maandiko Matakatifu: “Watu wote ambao hawakuambiwa habari zake wataona; nao wale ambao hawajapata kusikia, wataelewa.” Kwa sababu hiyo nilizuiwa mara nyingi kuja kwenu. Lakini maadamu sasa nimemaliza kazi yangu pande hizi, na kwa kuwa kwa miaka mingi nimekuwa na nia kubwa ya kuja kwenu, natumaini kufanya hivyo sasa. Ningependa kuwaoneni nikiwa safarini kwenda Spania na kupata msaada wenu kwa safari hiyo baada ya kufurahia kuwa kwa muda pamoja nanyi. Lakini, kwa sasa nakwenda kuwahudumia watu wa Mungu kule Yerusalemu. Maana makanisa ya Makedonia na Akaya yemeamua kutoa mchango wao kuwasaidia watu wa Mungu walio maskini huko Yerusalemu. Wao wenyewe wameamua kufanya hivyo; lakini, kwa kweli, hilo ni jukumu lao kwa hao. Maana, ikiwa watu wa mataifa mengine wameshiriki baraka za kiroho za Wayahudi, wanapaswa nao pia kuwahudumia Wayahudi katika mahitaji yao ya kidunia. Nitakapokwisha tekeleza kazi hiyo na kuwakabidhi mchango huo uliokusanywa kwa ajili yao, nitawatembeleeni nyinyi nikiwa safarini kwenda Spania. Najua ya kuwa nikija kwenu nitawaletea wingi wa baraka za Kristo. Basi, ndugu zangu, nawasihi kwa Bwana wetu Yesu Kristo na kwa upendo uletwao na Roho, mniunge mkono kwa kuniombea kwa Mungu. Ombeni nipate kutoka salama miongoni mwa wale wasioamini walioko Uyahudi, nayo huduma yangu huko Yerusalemu ipate kukubaliwa na watu wa Mungu walioko huko. Hivyo, Mungu akipenda, nitaweza kuja kwenu na moyo wa furaha, nikapumzike pamoja nanyi. Mungu aliye chanzo cha amani na awe nanyi nyote! Amina!
Waroma 15:13-33 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi Mungu wa tumaini na awajaze ninyi furaha yote na amani katika kuamini, mpate kuzidi sana kuwa na tumaini, katika nguvu za Roho Mtakatifu. Ndugu zangu, mimi mwenyewe nina hakika juu yenu, kuwa ninyi mmejaa wema, na mmejazwa ujuzi wote, tena mnaweza kuonyana. Lakini nawaandikia, kwa ujasiri zaidi katika sehemu za waraka huu, kana kwamba kuwakumbusha, kwa neema ile niliyopewa na Mungu, ili niwe mhudumu wa Kristo Yesu kati ya watu wa Mataifa, niifanyie Injili ya Mungu kazi ya ukuhani, kusudi Mataifa wawe sadaka yenye kibali, ikiisha kutakaswa na Roho Mtakatifu. Basi, nina sababu ya kuona fahari katika Kristo Yesu mbele za Mungu. Maana sitathubutu kutaja neno asilolitenda Kristo kwa kazi yangu, Mataifa wapate kutii, kwa neno au kwa tendo, kwa nguvu za ishara na maajabu, katika nguvu za Roho Mtakatifu; hata ikawa tangu Yerusalemu, na kandokando yake, mpaka Iliriko nimekwisha kuihubiri Injili ya Kristo kwa utimilifu; kadhalika nikijitahidi kuihubiri Injili, nisihubiri hapo ambapo jina la Kristo limekwisha kutajwa, nisije nikajenga juu ya msingi wa mtu mwingine; bali kama ilivyoandikwa, Wale wasiowahi kuhubiriwa habari zake wataona, Na wale wasiowahi kusikia habari zake watafahamu. Ndiyo sababu nilizuiwa mara nyingi nisije kwenu. Lakini sasa, kwa kuwa sina wasaa tena pande hizi, tena kwa miaka mingi nimekuwa nikitamani kuja kwenu; wakati wowote nitakaosafiri kwenda Spania [nitakuja kwenu.] Kwa maana natarajia kuwaona ninyi nikiwa katika safari, na kusafirishwa nanyi, baada ya kukaa kwenu kwa muda. Ila sasa ninakwenda Yerusalemu, nikiwahudumia watakatifu; maana imewapendeza watu wa Makedonia na Akaya kutoa mchango kwa ajili ya watakatifu walio maskini huko Yerusalemu. Naam, imewapendeza, tena wamekuwa wadeni wao. Kwa maana ikiwa Mataifa wameyashiriki mambo yao ya roho, imewabidi kuwahudumia kwa mambo yao ya mwili. Basi nikiisha kuimaliza kazi hiyo, na kuwatilia mhuri tunda hilo, nitapitia kwenu, kwenda Spania. Nami najua ya kuwa nikija kwenu nitakuja kwa utimilifu wa baraka ya Kristo. Ndugu zangu, nawasihi kwa Bwana wetu Yesu Kristo, na kwa upendo wa Roho, jitahidini pamoja nami katika maombi yenu kwa ajili yangu mbele za Mungu; kwamba niokolewe kutoka kwa wale wasioamini katika Yudea, na tena huduma yangu niliyo nayo huko Yerusalemu ikubalike kwa watakatifu; nipate kufika kwenu kwa furaha, kama apendavyo Mungu, nikapate kupumzika pamoja nanyi. Mungu wa amani na awe pamoja nanyi nyote. Amina.
Waroma 15:13-33 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi Mungu wa tumaini na awajaze ninyi furaha yote na amani katika kuamini, mpate kuzidi sana kuwa na tumaini, katika nguvu za Roho Mtakatifu. Ndugu zangu, nimehakikishwa mimi mwenyewe kwa habari zenu ya kuwa ninyi nanyi mmejaa wema, mmejazwa elimu yote, tena mwaweza kuonyana. Lakini nawaandikia, kwa ujasiri zaidi katika sehemu za waraka huu, kana kwamba kuwakumbusha, kwa neema ile niliyopewa na Mungu, ili niwe mhudumu wa Kristo Yesu kati ya watu wa Mataifa, niifanyie Injili ya Mungu kazi ya ukuhani, kusudi Mataifa wawe sadaka yenye kibali, ikiisha kutakaswa na Roho Mtakatifu. Basi, nina sababu ya kuona fahari katika Kristo Yesu mbele za Mungu. Maana sitathubutu kutaja neno asilolitenda Kristo kwa kazi yangu, Mataifa wapate kutii, kwa neno au kwa tendo, kwa nguvu za ishara na maajabu, katika nguvu za Roho Mtakatifu; hata ikawa tangu Yerusalemu, na kando kando yake, mpaka Iliriko nimekwisha kuihubiri Injili ya Kristo kwa utimilifu; kadhalika nikijitahidi kuihubiri Injili, nisihubiri hapo ambapo jina la Kristo limekwisha kutajwa, nisije nikajenga juu ya msingi wa mtu mwingine; bali kama ilivyoandikwa, Wale wasiohubiriwa habari zake wataona, Na wale wasiojasikia watafahamu. Ndiyo sababu nalizuiwa mara nyingi nisije kwenu. Lakini sasa, kwa kuwa sina wasaa tena pande hizi, tena tangu miaka mingi nina shauku kuja kwenu; wakati wo wote nitakaosafiri kwenda Spania [nitakuja kwenu.] Kwa maana nataraji kuwaona ninyi katika kusafiri kwangu, na kusafirishwa nanyi, moyo wangu ushibe kwenu kidogo. Ila sasa ninakwenda Yerusalemu, nikiwahudumu watakatifu; maana imewapendeza watu wa Makedonia na Akaya kufanya changizo kwa ajili ya watakatifu huko Yerusalemu walio maskini. Naam, imewapendeza, tena wamekuwa wadeni wao. Kwa maana ikiwa Mataifa wameyashiriki mambo yao ya roho, imewabidi kuwahudumu kwa mambo yao ya mwili. Basi nikiisha kuimaliza kazi hiyo, na kuwatilia muhuri tunda hilo, nitapitia kwenu, kwenda Spania. Nami najua ya kuwa nikija kwenu nitakuja kwa utimilifu wa baraka ya Kristo. Ndugu zangu, nawasihi kwa Bwana wetu Yesu Kristo, na kwa upendo wa Roho, jitahidini pamoja nami katika maombi yenu kwa ajili yangu mbele za Mungu; kwamba niokolewe na wale wasioamini katika Uyahudi, na tena huduma yangu niliyo nayo huko Yerusalemu ikubalike kwa watakatifu; nipate kufika kwenu kwa furaha, kama apendavyo Mungu, nikapate kupumzika pamoja nanyi. Mungu wa amani na awe pamoja nanyi nyote. Amina.
Waroma 15:13-33 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Mungu wa tumaini awajaze ninyi furaha yote na amani katika kumwamini, ili mpate kujawa na tumaini tele kwa nguvu ya Roho Mtakatifu. Ndugu zangu, mimi mwenyewe ninasadiki kwamba mmejaa wema, mkijazwa ufahamu wote na mnaweza kufundishana ninyi kwa ninyi. Hata hivyo, nimewaandikia kwa ujasiri vipengele kadha wa kadha katika waraka huu ili kuwakumbusha tena kuvihusu, kutokana na ile neema Mungu aliyonipa niwe mhudumu wa Kristo Yesu kwa watu wa Mataifa. Alinipa huduma ya kikuhani ya kutangaza Injili ya Mungu, ili watu wa Mataifa wapate kuwa dhabihu inayokubalika na Mungu, kwa kutakaswa na Roho Mtakatifu. Kwa hiyo ninajisifu katika Kristo Yesu, kwenye utumishi wangu kwa Mungu. Kwa maana sitathubutu kusema kitu chochote zaidi ya kile ambacho Kristo amefanya kwa kunitumia mimi katika kuwaongoza watu wa Mataifa wamtii Mungu kwa yale niliyosema na kufanya, kwa nguvu za ishara na miujiza, kwa uweza wa Roho wa Mungu, hivyo kuanzia Yerusalemu hadi maeneo yote ya kandokando yake hadi Iliriko, nimekwisha kuihubiri Injili ya Kristo kwa ukamilifu. Hivyo imekuwa nia yangu kuhubiri Habari Njema pale ambapo Kristo hajajulikana, ili nisije nikajenga juu ya msingi wa mtu mwingine. Lakini kama ilivyoandikwa: “Wale ambao hawajahubiriwa habari zake wataona, nao wale ambao hawajazisikia watafahamu.” Hii ndiyo sababu nimezuiliwa mara nyingi nisiweze kuja kwenu. Lakini sasa kwa kuwa hakuna nafasi zaidi kwa ajili yangu katika sehemu hii, ninatamani kuja kwenu kama ambavyo nimekuwa na shauku kwa miaka mingi. Nimekusudia kufanya hivyo nitakapokuwa njiani kwenda Hispania. Natarajia kuwaona katika safari yangu na kusafirishwa nanyi hadi huko, baada ya kufurahia ushirika wenu kwa kitambo kidogo. Ila sasa niko njiani kuelekea Yerusalemu kwa ajili ya kuwahudumia watakatifu huko. Kwa kuwa imewapendeza watu wa Makedonia na Akaya kufanya changizo kwa ajili ya maskini walio miongoni mwa watakatifu huko Yerusalemu. Imewapendeza kufanya hivyo, naam, kwani ni wadeni wao. Kwa maana ikiwa watu wa Mataifa wameshiriki baraka za rohoni za Wayahudi, wao ni wadeni wa Wayahudi, ili Wayahudi nao washiriki baraka zao za mambo ya mwilini. Kwa hiyo baada ya kukamilisha kazi hii na kuhakikisha kuwa wamepokea kila kitu kilichokusanywa, nitapitia kwenu nikiwa njiani kwenda Hispania. Ninajua kwamba nitakapokuja kwenu, nitakuja na wingi wa baraka za Kristo. Basi, ndugu zangu, nawasihi kwa Jina la Bwana wetu Yesu Kristo na kwa upendo wa Roho Mtakatifu, kujiunga nami katika taabu zangu mkiniombea kwa Mungu. Ombeni ili nipate kuokolewa mikononi mwa wale wasioamini walio Yudea, na kwamba utumishi wangu upate kukubaliwa na watakatifu wa huko Yerusalemu, ili kwa mapenzi ya Mungu niweze kuja kwenu kwa furaha, nami niburudishwe pamoja nanyi. Mungu wa amani na awe pamoja nanyi nyote. Amen.