Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Waroma 15:1-20

Waroma 15:1-20 Biblia Habari Njema (BHN)

Sisi tulio imara katika imani tunapaswa kuwasaidia wale walio dhaifu wayakabili matatizo yao. Tusijipendelee sisi wenyewe tu. Kila mmoja wetu anapaswa kumpendeza jirani yake kwa wema ili huyo apate kujijenga katika imani. Maana Kristo hakujipendelea mwenyewe; ila alikuwa kama yasemavyo Maandiko: “Kashfa zote walizokutolea wewe zimenipata mimi.” Maana, yote yaliyoandikwa yameandikwa kwa ajili ya kutufundisha sisi ili kutokana na saburi na faraja tupewayo na hayo Maandiko Matakatifu tupate kuwa na matumaini. Mungu aliye msingi wa saburi na faraja yote, awajalieni nyinyi kuwa na msimamo mmoja kufuatana na mfano wake Kristo Yesu, ili nyinyi nyote, kwa nia moja na sauti moja, mumtukuze Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo. Basi, karibishaneni kwa ajili ya utukufu wa Mungu kama naye Kristo alivyowakaribisheni. Maana, nawaambieni Kristo aliwatumikia Wayahudi apate kuonesha uaminifu wa Mungu, na zile ahadi Mungu alizowapa babu zetu zipate kutimia; ili nao watu wa mataifa mengine wapate kumtukuza Mungu kwa sababu ya huruma yake. Kama yasemavyo Maandiko Matakatifu: “Kwa hiyo nitakusifu miongoni mwa watu wa mataifa. Nitaziimba sifa za jina lako.” Tena Maandiko yasema: “Furahini, enyi watu wa mataifa; furahini pamoja na watu wake.” Na tena: “Enyi mataifa yote, msifuni Bwana; enyi watu wote, msifuni.” Tena Isaya asema: “Atatokea chipukizi katika ukoo wa Yese, naye atawatawala watu wa mataifa; nao watamtumainia.” Basi, Mungu aliye msingi wa matumaini, awajazeni furaha yote na amani kutokana na imani yenu; tumaini lenu lipate kuongezeka kwa nguvu ya Roho Mtakatifu. Ndugu zangu, mimi binafsi nina hakika kwamba nyinyi pia mmejaa wema, elimu yote, na mnaweza kushauriana nyinyi kwa nyinyi. Lakini nimewaandikia hapa na pale katika barua hii bila woga, nipate kuwakumbusheni juu ya mambo fulani. Nimefanya hivyo kwa sababu ya neema aliyonijalia Mungu ya kuwa mtumishi wa Yesu Kristo kwa watu wa mataifa. Ni jukumu langu la kikuhani kuihubiri Habari Njema ya Mungu ili watu wa mataifa mengine wapate kuwa tambiko inayokubaliwa na Mungu, tambiko iliyotakaswa na Roho Mtakatifu. Kwa hiyo, nikiwa nimeungana na Kristo Yesu, naweza kujivunia huduma yangu kwa ajili ya Mungu. Sithubutu kusema kitu kingine chochote isipokuwa tu kile ambacho Kristo Yesu amekifanya kwa kunitumia mimi ili watu wa mataifa wapate kutii. Amefanya hivyo kwa maneno na vitendo, kwa nguvu ya miujiza na maajabu, na kwa nguvu ya Roho wa Mungu. Basi, kwa kusafiri kila mahali, tangu kule Yerusalemu mpaka Iluriko, nimeihubiri kikamilifu Habari Njema ya Kristo. Nia yangu imekuwa daima kuihubiri Habari Njema popote pale ambapo jina la Kristo halijapata kusikika, nisije nikajenga juu ya msingi wa mtu mwingine.

Shirikisha
Soma Waroma 15

Waroma 15:1-20 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Basi imetupasa sisi tulio na nguvu kuuchukua udhaifu wao wasio na nguvu, wala haitupasi kujipendeza wenyewe. Kila mtu miongoni mwetu na ampendeze jirani yake, apate wema, akajengwe. Kwa maana Kristo naye hakujipendeza mwenyewe; bali kama ilivyoandikwa, Matusi yao waliokutusi wewe yalinipata mimi. Kwa kuwa yote yaliyotangulia kuandikwa yaliandikwa ili kutufundisha sisi; ili kwa saburi na faraja ya Maandiko tupate kuwa na tumaini. Na Mungu mwenye saburi na faraja awajalie kunuia mamoja ninyi kwa ninyi, kwa kufuata mfano wa Kristo Yesu; ili kwa moyo mmoja na kwa kinywa kimoja mpate kumtukuza Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo. Kwa hiyo mkaribishane ninyi kwa ninyi, kama naye Kristo alivyotukaribisha, ili Mungu atukuzwe. Kwa maana nasema, ya kwamba Kristo amefanyika mhudumu wa agano la kutahiriwa kwa ajili ya kweli ya Mungu, kusudi azithibitishe ahadi walizopewa baba zetu; tena ili Mataifa wamtukuze Mungu kwa ajili ya rehema zake; kama ilivyoandikwa, Kwa hiyo nitakushukuru kati ya Mataifa, Nami nitaliimbia jina lako. Na tena anena, Furahini, Mataifa, pamoja na watu wake. Na tena, Enyi Mataifa yote, msifuni Bwana; Enyi watu wote, mhimidini. Na tena Isaya anena, Litakuwako shina la Yese, Naye aondokeaye kuwatawala Mataifa; Ndiye Mataifa watakayemtumaini. Basi Mungu wa tumaini na awajaze ninyi furaha yote na amani katika kuamini, mpate kuzidi sana kuwa na tumaini, katika nguvu za Roho Mtakatifu. Ndugu zangu, mimi mwenyewe nina hakika juu yenu, kuwa ninyi mmejaa wema, na mmejazwa ujuzi wote, tena mnaweza kuonyana. Lakini nawaandikia, kwa ujasiri zaidi katika sehemu za waraka huu, kana kwamba kuwakumbusha, kwa neema ile niliyopewa na Mungu, ili niwe mhudumu wa Kristo Yesu kati ya watu wa Mataifa, niifanyie Injili ya Mungu kazi ya ukuhani, kusudi Mataifa wawe sadaka yenye kibali, ikiisha kutakaswa na Roho Mtakatifu. Basi, nina sababu ya kuona fahari katika Kristo Yesu mbele za Mungu. Maana sitathubutu kutaja neno asilolitenda Kristo kwa kazi yangu, Mataifa wapate kutii, kwa neno au kwa tendo, kwa nguvu za ishara na maajabu, katika nguvu za Roho Mtakatifu; hata ikawa tangu Yerusalemu, na kandokando yake, mpaka Iliriko nimekwisha kuihubiri Injili ya Kristo kwa utimilifu; kadhalika nikijitahidi kuihubiri Injili, nisihubiri hapo ambapo jina la Kristo limekwisha kutajwa, nisije nikajenga juu ya msingi wa mtu mwingine

Shirikisha
Soma Waroma 15

Waroma 15:1-20 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Basi imetupasa sisi tulio na nguvu kuuchukua udhaifu wao wasio na nguvu, wala haitupasi kujipendeza wenyewe. Kila mtu miongoni mwetu na ampendeze jirani yake, apate wema, akajengwe. Kwa maana Kristo naye hakujipendeza mwenyewe; bali kama ilivyoandikwa, Malaumu yao waliokulaumu wewe yalinipata mimi. Kwa kuwa yote yaliyotangulia kuandikwa yaliandikwa ili kutufundisha sisi; ili kwa saburi na faraja ya maandiko tupate kuwa na tumaini. Na Mungu mwenye saburi na faraja awajalie kunia mamoja ninyi kwa ninyi, kwa mfano wa Kristo Yesu; ili kwa moyo mmoja na kwa kinywa kimoja mpate kumtukuza Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo. Kwa hiyo mkaribishane ninyi kwa ninyi, kama naye Kristo alivyotukaribisha, ili Mungu atukuzwe. Kwa maana nasema, ya kwamba Kristo amefanyika mhudumu wa agano la kutahiriwa kwa ajili ya kweli ya Mungu, kusudi azithibitishe ahadi walizopewa baba zetu; tena ili Mataifa wamtukuze Mungu kwa ajili ya rehema zake; kama ilivyoandikwa, Kwa hiyo nitakushukuru kati ya Mataifa, Nami nitaliimbia jina lako. Na tena anena, Furahini, Mataifa, pamoja na watu wake. Na tena, Enyi Mataifa yote, msifuni Bwana; Enyi watu wote, mhimidini. Na tena Isaya anena, Litakuwako shina la Yese, Naye aondokeaye kuwatawala Mataifa; Ndiye Mataifa watakayemtumaini. Basi Mungu wa tumaini na awajaze ninyi furaha yote na amani katika kuamini, mpate kuzidi sana kuwa na tumaini, katika nguvu za Roho Mtakatifu. Ndugu zangu, nimehakikishwa mimi mwenyewe kwa habari zenu ya kuwa ninyi nanyi mmejaa wema, mmejazwa elimu yote, tena mwaweza kuonyana. Lakini nawaandikia, kwa ujasiri zaidi katika sehemu za waraka huu, kana kwamba kuwakumbusha, kwa neema ile niliyopewa na Mungu, ili niwe mhudumu wa Kristo Yesu kati ya watu wa Mataifa, niifanyie Injili ya Mungu kazi ya ukuhani, kusudi Mataifa wawe sadaka yenye kibali, ikiisha kutakaswa na Roho Mtakatifu. Basi, nina sababu ya kuona fahari katika Kristo Yesu mbele za Mungu. Maana sitathubutu kutaja neno asilolitenda Kristo kwa kazi yangu, Mataifa wapate kutii, kwa neno au kwa tendo, kwa nguvu za ishara na maajabu, katika nguvu za Roho Mtakatifu; hata ikawa tangu Yerusalemu, na kando kando yake, mpaka Iliriko nimekwisha kuihubiri Injili ya Kristo kwa utimilifu; kadhalika nikijitahidi kuihubiri Injili, nisihubiri hapo ambapo jina la Kristo limekwisha kutajwa, nisije nikajenga juu ya msingi wa mtu mwingine

Shirikisha
Soma Waroma 15

Waroma 15:1-20 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

Sisi tulio na nguvu, hatuna budi kuchukuliana na kushindwa kwa wale walio dhaifu wala si kujipendeza nafsi zetu wenyewe. Kila mmoja wetu inampasa kumpendeza jirani yake kwa mambo mema, ili kumjenga katika imani. Kwa maana hata Kristo hakujipendeza mwenyewe, bali kama ilivyoandikwa: “Matukano yao wale wanaokutukana wewe yalinipata mimi.” Kwa maana kila kitu kilichoandikwa zamani, kiliandikwa kutufundisha, ili kwa saburi na faraja tunayopata katika Maandiko tuwe na tumaini. Mungu atoaye saburi na faraja awajalie ninyi roho ya umoja miongoni mwenu mnapomfuata Kristo Yesu, ili kwa moyo mmoja mpate kumtukuza Mungu aliye Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo. Karibishaneni ninyi kwa ninyi kama Kristo alivyowakaribisha ninyi ili kumletea Mungu utukufu. Kwa maana nawaambia kwamba Kristo amekuwa mtumishi kwa wale waliotahiriwa ili kuonesha kweli ya Mungu, na kuthibitisha zile ahadi walizopewa baba zetu wa zamani, na pia ili watu wa Mataifa wamtukuze Mungu kwa rehema zake. Kama ilivyoandikwa: “Kwa hiyo nitakutukuza kati ya watu wa Mataifa; nitaliimbia sifa jina lako.” Tena yasema, “Enyi watu wa Mataifa, furahini pamoja na watu wa Mungu.” Tena, “Msifuni Bwana, ninyi watu wa Mataifa wote, na kumwimbia sifa, enyi watu wote.” Tena Isaya anasema, “Shina la Yese litachipuka, yeye atakayeinuka ili kuyatawala mataifa. Watu wa Mataifa watamtumaini.” Mungu wa tumaini awajaze ninyi furaha yote na amani katika kumwamini, ili mpate kujawa na tumaini tele kwa nguvu ya Roho Mtakatifu. Ndugu zangu, mimi mwenyewe ninasadiki kwamba mmejaa wema, mkijazwa ufahamu wote na mnaweza kufundishana ninyi kwa ninyi. Hata hivyo, nimewaandikia kwa ujasiri vipengele kadha wa kadha katika waraka huu ili kuwakumbusha tena kuvihusu, kutokana na ile neema Mungu aliyonipa niwe mhudumu wa Kristo Yesu kwa watu wa Mataifa. Alinipa huduma ya kikuhani ya kutangaza Injili ya Mungu, ili watu wa Mataifa wapate kuwa dhabihu inayokubalika na Mungu, kwa kutakaswa na Roho Mtakatifu. Kwa hiyo ninajisifu katika Kristo Yesu, kwenye utumishi wangu kwa Mungu. Kwa maana sitathubutu kusema kitu chochote zaidi ya kile ambacho Kristo amefanya kwa kunitumia mimi katika kuwaongoza watu wa Mataifa wamtii Mungu kwa yale niliyosema na kufanya, kwa nguvu za ishara na miujiza, kwa uweza wa Roho wa Mungu, hivyo kuanzia Yerusalemu hadi maeneo yote ya kandokando yake hadi Iliriko, nimekwisha kuihubiri Injili ya Kristo kwa ukamilifu. Hivyo imekuwa nia yangu kuhubiri Habari Njema pale ambapo Kristo hajajulikana, ili nisije nikajenga juu ya msingi wa mtu mwingine.

Shirikisha
Soma Waroma 15