Waroma 10:8-13
Waroma 10:8-13 Biblia Habari Njema (BHN)
Maandiko Matakatifu yasema hivi: “Ujumbe huo wa Mungu uko karibu nawe, uko kinywani mwako na moyoni mwako” nao ndio ile imani tunayoihubiri. Kama ukikiri kwa kinywa chako kwamba Yesu ni Bwana na kuamini moyoni mwako kwamba Mungu alimfufua kutoka kwa wafu, utaokoka. Maana mtu huamini kwa moyo akafanywa mwadilifu; na hukiri kwa kinywa akaokolewa. Maandiko Matakatifu yasema: “Kila anayemwamini hataaibishwa.” Jambo hili ni kwa wote, kwani hakuna tofauti kati ya Wayahudi na wasio Wayahudi; Bwana wa wote ni mmoja, naye ni mkarimu sana kwao wote wamwombao. Maana Maandiko Matakatifu yasema: “Kila mtu atakayeomba kwa jina la Bwana, ataokolewa.”
Waroma 10:8-13 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Lakini yanenaje? Lile neno liko karibu nawe, katika kinywa chako, na katika moyo wako; yaani, ni lile neno la imani tulihubirilo. Kwa sababu, ukimkiri Yesu kwa kinywa chako ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni mwako ya kuwa Mungu alimfufua katika wafu, utaokoka. Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu. Kwa maana andiko lanena, Kila amwaminiye hatatahayarika. Kwa maana hakuna tofauti ya Myahudi na Mgiriki; maana yeye yule ni Bwana wa wote, mwenye ukarimu mwingi kwa wote wamwitao; kwa kuwa, Kila atakayeliitia Jina la Bwana ataokoka.
Waroma 10:8-13 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Lakini yanenaje? Lile neno li karibu nawe, katika kinywa chako, na katika moyo wako; yaani, ni lile neno la imani tulihubirilo. Kwa sababu, ukimkiri Yesu kwa kinywa chako ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni mwako ya kuwa Mungu alimfufua katika wafu, utaokoka. Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu. Kwa maana andiko lanena, Kila amwaminiye hatatahayarika. Kwa maana hakuna tofauti ya Myahudi na Myunani; maana yeye yule ni Bwana wa wote, mwenye utajiri kwa wote wamwitao; kwa kuwa, Kila atakayeliitia Jina la Bwana ataokoka.
Waroma 10:8-13 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Lakini andiko lasemaje? “Lile neno liko karibu nawe, liko kinywani mwako na moyoni mwako,” yaani lile neno la imani tunalolihubiri. Kwa sababu, ukikiri kwa kinywa chako kwamba “Yesu ni Bwana,” na kuamini moyoni mwako kwamba Mungu alimfufua kutoka kwa wafu, utaokoka. Kwa maana kwa moyo mtu huamini na hivyo kuhesabiwa haki, tena kwa kinywa mtu hukiri na hivyo kupata wokovu. Kama Maandiko yanavyosema, “Yeyote amwaminiye hataaibika kamwe.” Kwa maana hakuna tofauti kati ya Myahudi na mtu wa Mataifa, yeye ni Bwana wa wote, mwenye utajiri kwa wote wamwitao. Kwa maana, “Kila mtu atakayeliitia Jina la Bwana, ataokolewa.”