Waroma 10:11-21
Waroma 10:11-21 Biblia Habari Njema (BHN)
Maandiko Matakatifu yasema: “Kila anayemwamini hataaibishwa.” Jambo hili ni kwa wote, kwani hakuna tofauti kati ya Wayahudi na wasio Wayahudi; Bwana wa wote ni mmoja, naye ni mkarimu sana kwao wote wamwombao. Maana Maandiko Matakatifu yasema: “Kila mtu atakayeomba kwa jina la Bwana, ataokolewa.” Basi, watamwombaje yeye ambaye hawamwamini? Tena, watamwaminije kama hawajapata kusikia habari zake? Na watasikiaje habari zake kama hakuna mhubiri? Na watu watahubirije kama hawakutumwa? Kama yasemavyo Maandiko Matakatifu: “Ni jambo la kupendeza mno kuja kwa wale wanaohubiri Habari Njema!” Lakini wote hawakuipokea hiyo habari njema. Maana Isaya alisema: “Bwana, ni nani aliyeamini ujumbe wetu?” Hivyo basi, imani inatokana na kuusikia ujumbe, na huo ujumbe unatokana na neno la Kristo. Lakini nauliza: Je, hawakuusikia huo ujumbe? Naam, waliusikia; kama Maandiko Matakatifu yasemavyo: “Sauti yao imeenea duniani kote; maneno yao yamefika mpaka kingo za ulimwengu.” Tena nauliza: Je, yawezekana kwamba watu wa Israeli hawakufahamu? Mose mwenyewe ni wa kwanza kujibu: “Nitawafanyeni muwaonee wivu watu ambao si taifa; nitawafanyeni muwe na hasira juu ya taifa la watu wapumbavu.” Tena Isaya anathubutu hata kusema: “Wale ambao hawakunitafuta wamenipata; nimejionesha kwao wasiouliza habari zangu.” Lakini kuhusu Israeli anasema: “Mchana kutwa niliwanyoshea mikono yangu watu waasi na wasiotii.”
Waroma 10:11-21 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kwa maana andiko lanena, Kila amwaminiye hatatahayarika. Kwa maana hakuna tofauti ya Myahudi na Mgiriki; maana yeye yule ni Bwana wa wote, mwenye ukarimu mwingi kwa wote wamwitao; kwa kuwa, Kila atakayeliitia Jina la Bwana ataokoka. Basi wamwiteje yeye wasiyemwamini? Tena wamwaminije yeye wasiyemsikia? Tena wamsikieje pasipo mhubiri? Tena wahubirije, wasipopelekwa? Kama ilivyoandikwa, Ni mizuri kama nini miguu yao wahubirio habari ya mema! Lakini si wote walioitii ile Habari Njema. Kwa maana Isaya asema, Bwana, ni nani aliyeziamini habari zetu? Basi imani, hutokana na kusikia; na kusikia huja kwa neno la Kristo. Lakini nasema, Je! Wao hawakusikia? Naam, wamesikia, Sauti yao imeenea duniani kote, Na maneno yao hadi katika miisho ya ulimwengu. Lakini nasema, Je! Waisraeli hawakufahamu? Kwanza Musa anena, Nitawatia wivu kwa watu ambao si taifa, Kwa taifa lisilo na fahamu nitawakasirisha. Na Isaya anao ujasiri mwingi, asema, Nilipatikana nao wasionitafuta, Nilidhihirika kwao wasioniulizia. Lakini kwa Israeli asema, Mchana kutwa niliwanyoshea mikono watu wasiotii na wakaidi.
Waroma 10:11-21 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Kwa maana andiko lanena, Kila amwaminiye hatatahayarika. Kwa maana hakuna tofauti ya Myahudi na Myunani; maana yeye yule ni Bwana wa wote, mwenye utajiri kwa wote wamwitao; kwa kuwa, Kila atakayeliitia Jina la Bwana ataokoka. Basi wamwiteje yeye wasiyemwamini? Tena wamwaminije yeye wasiyemsikia? Tena wamsikieje pasipo mhubiri? Tena wahubirije, wasipopelekwa? Kama ilivyoandikwa, Ni mizuri kama nini miguu yao wahubirio habari ya mema! Lakini si wote walioitii ile habari njema. Kwa maana Isaya asema, Bwana, ni nani aliyeziamini habari zetu? Basi imani, chanzo chake ni kusikia; na kusikia huja kwa neno la Kristo. Lakini nasema, Je! Wao hawakusikia? Naam, wamesikia, Sauti yao imeenea duniani mwote, Na maneno yao hata miisho ya ulimwengu. Lakini nasema, Je! Waisraeli hawakufahamu? Kwanza Musa anena, Nitawatia wivu kwa watu ambao si taifa, Kwa taifa lisilo na fahamu nitawaghadhibisha. Na Isaya anao ujasiri mwingi, asema, Nalipatikana nao wasionitafuta, Nalidhihirika kwao wasioniulizia. Lakini kwa Israeli asema, Mchana kutwa naliwanyoshea mikono watu wasiotii na wakaidi.
Waroma 10:11-21 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Kama Maandiko yanavyosema, “Yeyote amwaminiye hataaibika kamwe.” Kwa maana hakuna tofauti kati ya Myahudi na mtu wa Mataifa, yeye ni Bwana wa wote, mwenye utajiri kwa wote wamwitao. Kwa maana, “Kila mtu atakayeliitia Jina la Bwana, ataokolewa.” Lakini watamwitaje yeye ambaye hawajamwamini? Nao watawezaje kumwamini yeye ambaye hawajamsikia? Tena watamsikiaje bila mtu kuwahubiria? Nao watahubirije wasipopelekwa? Kama ilivyoandikwa, “Tazama jinsi ilivyo mizuri miguu yao wale wanaohubiri Habari Njema!” Lakini si wote waliotii Habari Njema. Kwa maana Isaya asema, “Bwana, ni nani aliyeamini ujumbe wetu?” Basi, imani chanzo chake ni kusikia, na kusikia huja kwa neno la Kristo. Lakini nauliza: Je, wao hawakusikia? Naam, wamesikia, kwa maana: “Sauti yao imeenea duniani pote, nayo maneno yao yameenea hadi miisho ya ulimwengu.” Nami nauliza tena: Je, Waisraeli hawakuelewa? Kwanza, Musa asema, “Nitawafanya mwe na wivu kwa watu wale ambao si taifa. Nitawakasirisha kwa taifa lile lisilo na ufahamu.” Naye Isaya kwa ujasiri mwingi anasema, “Nimeonekana na watu wale ambao hawakunitafuta. Nilijifunua kwa watu wale ambao hawakunitafuta.” Lakini kuhusu Israeli anasema, “Mchana kutwa nimewanyooshea watu wakaidi na wasiotii mikono yangu.”