Waroma 1:7-17
Waroma 1:7-17 Biblia Habari Njema (BHN)
Basi, nawaandikia nyinyi nyote mlioko Roma ambao Mungu anawapenda, akawateua muwe watu wake. Nawatakieni neema na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu na Bwana Yesu Kristo. Awali ya yote, namshukuru Mungu wangu kwa njia ya Yesu Kristo kwa ajili yenu nyote, kwa sababu imani yenu inasikika duniani kote. Mungu, ambaye ninamtumikia kwa moyo wangu wote katika kuhubiri Habari Njema ya Mwanae, ni shahidi wangu kwamba ninawakumbukeni daima katika sala zangu. Namwomba Mungu akipenda, anipatie nafasi nzuri ya kuja kwenu sasa. Kwa maana ninatamani sana kuwaoneni ili nipate kuwagawieni zawadi ya kiroho na kuwaimarisha. Ndiyo kusema, tutaimarishana: Imani yenu itaniimarisha mimi, na yangu itawaimarisha nyinyi. Ndugu zangu, nataka mjue kwamba mara nyingi nilikusudia kuwatembeleeni, lakini mpaka sasa nimezuiwa. Ningependa kupata mafanikio mema kati yenu kama nilivyopata kati ya watu wa mataifa mengine. Ninalo jukumu kwa watu wote, waliostaarabika na wasiostaarabika, wenye elimu na wasio na elimu. Ndiyo maana ninatamani pia kuihubiri Habari Njema kwenu nyinyi mlioko huko Roma. Sioni aibu kutangaza Habari Njema; yenyewe ni nguvu ya Mungu inayowaokoa wote wanaoamini: Wayahudi kwanza na wasio Wayahudi pia. Kwa maana Habari Njema inaonesha wazi jinsi Mungu anavyowakubali watu kuwa waadilifu; jambo hili hufanyika kwa imani, tangu mwanzo mpaka mwisho; kama ilivyoandikwa: “Mwadilifu kwa imani ataishi.”
Waroma 1:7-17 Swahili Revised Union Version (SRUV)
kwa wote walioko Rumi, wapendwao na Mungu, walioitwa kuwa watakatifu. Neema na iwe kwenu na amani itokayo kwa Mungu Baba yetu, na kwa Bwana Yesu Kristo. Kwanza namshukuru Mungu wangu katika Yesu Kristo kwa ajili yenu nyote, kwa kuwa imani yenu inahubiriwa kote duniani. Kwa maana Mungu, nimwabuduye kwa roho yangu katika Injili ya Mwana wake, ni shahidi wangu jinsi niwatajavyo pasipo kukoma, siku zote katika sala zangu, nikiomba nije kwenu hivi karibu, Mungu akipenda kuifanikisha safari yangu. Kwa maana ninatamani sana kuwaona, nipate kuwapa karama ya rohoni, ili mfanywe imara; yaani, tufarijiane mimi na ninyi, kila mtu kwa imani ya mwenzake, yenu na yangu. Lakini, ndugu zangu, sipendi msiwe na habari, ya kuwa mara nyingi nilikusudia kuja kwenu, nikazuiliwa mpaka sasa, ili nipate kuwa na matunda kwenu ninyi pia kama nilivyo nayo katika Mataifa wengine. Nawiwa na Wagiriki na wasio Wagiriki, nawiwa na wenye hekima na wasio na hekima. Kwa hiyo, kwa upande wangu, mimi ni tayari kuihubiri Injili hata na kwenu ninyi mnaokaa Rumi. Kwa maana siionei haya Injili; kwa sababu ni uweza wa Mungu uuletao wokovu, kwa kila aaminiye, kwa Myahudi kwanza, na kwa Mgiriki pia. Kwa maana haki ya Mungu inadhihirishwa ndani yake, toka imani hadi imani; kama ilivyoandikwa, Mwenye haki ataishi kwa imani.
Waroma 1:7-17 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
kwa wote walioko Rumi, wapendwao na Mungu, walioitwa kuwa watakatifu. Neema na iwe kwenu na amani itokayo kwa Mungu Baba yetu, na kwa Bwana Yesu Kristo. Kwanza namshukuru Mungu wangu katika Yesu Kristo kwa ajili yenu nyote, kwa kuwa imani yenu inahubiriwa katika dunia nzima. Kwa maana Mungu, nimwabuduye kwa roho yangu katika Injili ya Mwana wake, ni shahidi wangu jinsi niwatajavyo pasipo kukoma, siku zote katika sala zangu, nikiomba nije kwenu hivi karibu, Mungu akipenda kuifanikisha safari yangu. Kwa maana ninatamani sana kuwaona, nipate kuwapa karama ya rohoni, ili mfanywe imara; yaani, tufarijiane mimi na ninyi, kila mtu kwa imani ya mwenzake, yenu na yangu. Lakini, ndugu zangu, sipendi msiwe na habari, ya kuwa mara nyingi nalikusudia kuja kwenu, nikazuiliwa hata sasa, ili nipate kuwa na matunda kwenu ninyi pia kama nilivyo nayo katika Mataifa wengine. Nawiwa na Wayunani na wasio Wayunani, nawiwa na wenye hekima na wasio na hekima. Kwa hiyo, kwa upande wangu, mimi ni tayari kuihubiri Injili hata na kwenu ninyi mnaokaa Rumi. Kwa maana siionei haya Injili; kwa sababu ni uweza wa Mungu uuletao wokovu, kwa kila aaminiye, kwa Myahudi kwanza, na kwa Myunani pia. Kwa maana haki ya Mungu inadhihirishwa ndani yake, toka imani hata imani; kama ilivyoandikwa, Mwenye haki ataishi kwa imani.
Waroma 1:7-17 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Kwa wote walio Rumi wanaopendwa na Mungu na kuitwa kuwa watakatifu. Neema na amani zinazotoka kwa Mungu Baba yetu na kwa Bwana Yesu Kristo ziwe nanyi. Kwanza kabisa, namshukuru Mungu wangu kupitia kwa Yesu Kristo kwa ajili yenu nyote, kwa sababu imani yenu inatangazwa duniani kote. Kwa maana Mungu ninayemtumikia kwa moyo wangu wote katika kuhubiri Injili ya Mwanawe, ni shahidi wangu jinsi ninavyowakumbuka daima katika maombi yangu siku zote. Nami ninaomba kwamba hatimaye sasa kwa mapenzi ya Mungu, njia ipate kufunguliwa kwa ajili yangu ili nije kwenu. Ninatamani sana kuwaona ili nipate kuwapa karama za rohoni ili mwe imara, au zaidi, ninyi pamoja nami tuweze kutiana moyo katika imani sisi kwa sisi. Ndugu zangu, napenda mfahamu kwamba mara nyingi nimekusudia kuja kwenu (ingawa hadi sasa nimezuiliwa), ili nipate kuvuna mavuno miongoni mwenu kama nilivyovuna miongoni mwa watu wa Mataifa wengine. Mimi ni mdeni kwa Wayunani na kwa wasio Wayunani, kwa wenye hekima na kwa wasio na hekima. Ndiyo sababu ninatamani sana kuihubiri Injili kwenu pia ninyi mlioko Rumi. Mimi siionei haya Injili, kwa maana ni uweza wa Mungu uletao wokovu kwa kila aaminiye, kwanza kwa Myahudi na kwa Myunani pia. Kwa maana katika Injili haki ya Mungu imedhihirishwa, haki ile iliyo ya imani hadi imani. Kama ilivyoandikwa: “Mwenye haki ataishi kwa imani.”