Waroma 1:26-32
Waroma 1:26-32 Biblia Habari Njema (BHN)
Kwa hiyo, Mungu amewaacha wafuate tamaa mbaya. Hata wanawake wanabadili matumizi yanayopatana na maumbile. Nao wanaume hali kadhalika, wanaacha kufuata matumizi ya maumbile ya mume na mke, wakawakiana tamaa wao kwa wao. Wanaume wanafanyiana mambo ya aibu, na hivyo wanajiletea wenyewe adhabu wanayostahili kwa vitendo vyao viovu. Kwa vile watu walikataa kumtambua Mungu, Mungu amewaacha katika fikira zao potovu, wakafanya yale ambayo hawangestahili kufanya. Wamejaa kila aina ya uovu, dhuluma, ulafi na ufisadi. Wamejaa wivu, uuaji, ugomvi, udanganyifu na nia mbaya; husengenya, na kusingiziana; ni watu wa kuchukiza kwa Mungu, wafidhuli, wenye kiburi na majivuno; hodari sana katika kutenda mabaya, na hawawatii wazazi wao; hawana dhamiri, hawatimizi ahadi zao, hawana wema wala huruma kwa wengine. Wanajua kwamba sheria ya Mungu yasema kwamba watu wanaoishi mithili hiyo, wanastahili kifo. Zaidi ya hayo, siyo tu kwamba wanafanya mambo hayo wao wenyewe, bali hata huwapongeza wale wanaofanya mambo hayohayo.
Waroma 1:26-32 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Hivyo Mungu aliwaacha wafuate tamaa zao za aibu, hata wanawake wakabadili matumizi ya asili kwa matumizi yasiyo ya asili; wanaume nao vivyo hivyo waliyaacha matumizi ya mke, ya asili, wakawakiana tamaa, wanaume wakiyatenda yasiyopasa, wakapata nafsini mwao malipo ya upotevu wao yaliyo haki yao. Na kama walivyokataa kuwa na Mungu katika fahamu zao, Mungu aliwaacha wafuate akili zao zisizofaa, wayafanye yasiyowapasa. Wamejawa na udhalimu wa kila namna, uovu na tamaa na ubaya; wamejawa na husuda, na uuaji, na fitina, na hadaa; watu wa nia mbaya, wenye kusengenya, wenye kusingizia, wenye kumchukia Mungu, wenye jeuri, wenye kutakabari, wenye majivuno, wenye kutunga mabaya, wasiowatii wazazi wao, wasio na ufahamu, wenye kuvunja maagano, wasiopenda jamaa zao, wasio na rehema; ambao wakijua sana hukumu ya haki ya Mungu, ya kwamba wayatendao hayo wamestahili mauti, wanatenda hayo, wala si hivyo tu, bali wanakubaliana nao wayatendao.
Waroma 1:26-32 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Waroma 1:26-32 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Kwa sababu hii, Mungu aliwaacha wazifuate tamaa za aibu. Hata wanawake wao wakabadili mahusiano ya kimwili ya asili kwa mahusiano yasiyokusudiwa. Vivyo hivyo wanaume pia wakaacha mahusiano ya kimwili ya asili na wanawake, wakawakiana kwa tamaa mbaya wao kwa wao. Wanaume wakafanya matendo ya aibu na wanaume wengine, nao wakapata adhabu waliyostahili kwa ajili ya upotovu wao. Nao kwa kuwa hawakuona umuhimu wa kudumisha ufahamu wa Mungu, yeye akawaachilia wafuate akili za upotovu, watende mambo yale yasiyostahili kutendwa. Wamejawa na udhalimu wa kila namna, uasherati, uovu, tamaa mbaya na hila. Wamejawa na husuda, uuaji, ugomvi, udanganyifu, hadaa na nia mbaya. Wao pia ni wasengenyaji, wasingiziaji, wanaomchukia Mungu, wajeuri, wenye kiburi na majivuno, wenye hila, wasiotii wazazi wao, wajinga, wasioamini, wasio na huruma na wakatili. Ingawa wanafahamu sheria ya haki ya Mungu kwamba watu wanaofanya mambo kama hayo wanastahili mauti, si kwamba wanaendelea kutenda hayo tu, bali pia wanakubaliana na wale wanaoyatenda.