Waroma 1:21-32
Waroma 1:21-32 Biblia Habari Njema (BHN)
Ingawa wanajua kuna Mungu, lakini hawampi heshima anayostahili, wala hawamshukuru. Badala yake, fikira zao zimekuwa batili na akili zao tupu zimejaa giza. Wanajidai kuwa wenye hekima, kumbe ni wapumbavu. Wanaacha kumwabudu Mungu aishiye milele, na badala yake, wanaabudu sanamu zilizo mfano wa binadamu ambaye hufa, mfano wa wanyama, ndege, au wanyama watambaao. Kwa sababu hiyo, Mungu amewaacha wafuate tamaa mbaya za mioyo yao na kufanyiana mambo ya aibu kwa miili yao. Wanaubadili ukweli juu ya Mungu kwa uongo; wanaheshimu na kuabudu kiumbe badala ya Muumba mwenyewe, ambaye ndiye astahiliye sifa milele! Amina. Kwa hiyo, Mungu amewaacha wafuate tamaa mbaya. Hata wanawake wanabadili matumizi yanayopatana na maumbile. Nao wanaume hali kadhalika, wanaacha kufuata matumizi ya maumbile ya mume na mke, wakawakiana tamaa wao kwa wao. Wanaume wanafanyiana mambo ya aibu, na hivyo wanajiletea wenyewe adhabu wanayostahili kwa vitendo vyao viovu. Kwa vile watu walikataa kumtambua Mungu, Mungu amewaacha katika fikira zao potovu, wakafanya yale ambayo hawangestahili kufanya. Wamejaa kila aina ya uovu, dhuluma, ulafi na ufisadi. Wamejaa wivu, uuaji, ugomvi, udanganyifu na nia mbaya; husengenya, na kusingiziana; ni watu wa kuchukiza kwa Mungu, wafidhuli, wenye kiburi na majivuno; hodari sana katika kutenda mabaya, na hawawatii wazazi wao; hawana dhamiri, hawatimizi ahadi zao, hawana wema wala huruma kwa wengine. Wanajua kwamba sheria ya Mungu yasema kwamba watu wanaoishi mithili hiyo, wanastahili kifo. Zaidi ya hayo, siyo tu kwamba wanafanya mambo hayo wao wenyewe, bali hata huwapongeza wale wanaofanya mambo hayohayo.
Waroma 1:21-32 Swahili Revised Union Version (SRUV)
kwa sababu, walipomjua Mungu hawakumtukuza kama ndiye Mungu wala kumshukuru; bali walipotea katika uzushi wao, na mioyo yao yenye ujinga ikatiwa giza. Wakijinena kuwa wenye hekima walipumbazika; wakaubadili utukufu wa Mungu asiye na uharibifu kwa mfano wa sura ya binadamu aliye na uharibifu, na ya ndege, na ya wanyama, na ya vitambaavyo. Kwa ajili ya hayo Mungu aliwaacha katika tamaa za mioyo yao, waufuate uchafu, hata wakavunjiana heshima miili yao. Kwa maana waliibadili kweli ya Mungu kuwa uongo, wakakisujudia kiumbe na kukiabudu badala ya Muumba anayehimidiwa milele. Amina. Hivyo Mungu aliwaacha wafuate tamaa zao za aibu, hata wanawake wakabadili matumizi ya asili kwa matumizi yasiyo ya asili; wanaume nao vivyo hivyo waliyaacha matumizi ya mke, ya asili, wakawakiana tamaa, wanaume wakiyatenda yasiyopasa, wakapata nafsini mwao malipo ya upotevu wao yaliyo haki yao. Na kama walivyokataa kuwa na Mungu katika fahamu zao, Mungu aliwaacha wafuate akili zao zisizofaa, wayafanye yasiyowapasa. Wamejawa na udhalimu wa kila namna, uovu na tamaa na ubaya; wamejawa na husuda, na uuaji, na fitina, na hadaa; watu wa nia mbaya, wenye kusengenya, wenye kusingizia, wenye kumchukia Mungu, wenye jeuri, wenye kutakabari, wenye majivuno, wenye kutunga mabaya, wasiowatii wazazi wao, wasio na ufahamu, wenye kuvunja maagano, wasiopenda jamaa zao, wasio na rehema; ambao wakijua sana hukumu ya haki ya Mungu, ya kwamba wayatendao hayo wamestahili mauti, wanatenda hayo, wala si hivyo tu, bali wanakubaliana nao wayatendao.
Waroma 1:21-32 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Waroma 1:21-32 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Kwa maana ingawa walimjua Mungu, hawakumtukuza yeye kama ndiye Mungu wala hawakumshukuru, bali fikira zao zimekuwa batili na mioyo yao ya ujinga ikatiwa giza. Ingawa walijidai kuwa wenye hekima, wakawa wajinga, na kubadili utukufu wa Mungu aishiye milele kwa sanamu zilizotengenezwa zifanane na mwanadamu ambaye hufa, na mfano wa ndege, wanyama na viumbe vinavyotambaa. Kwa hiyo, Mungu akawaacha wazifuate tamaa mbaya za mioyo yao katika uasherati, hata wakaivunjia heshima miili yao wao kwa wao. Waliibadili kweli ya Mungu kuwa uongo, wakaabudu na kutumikia kiumbe badala ya Muumba, ahimidiwaye milele! Amen. Kwa sababu hii, Mungu aliwaacha wazifuate tamaa za aibu. Hata wanawake wao wakabadili mahusiano ya kimwili ya asili kwa mahusiano yasiyokusudiwa. Vivyo hivyo wanaume pia wakaacha mahusiano ya kimwili ya asili na wanawake, wakawakiana kwa tamaa mbaya wao kwa wao. Wanaume wakafanya matendo ya aibu na wanaume wengine, nao wakapata adhabu waliyostahili kwa ajili ya upotovu wao. Nao kwa kuwa hawakuona umuhimu wa kudumisha ufahamu wa Mungu, yeye akawaachilia wafuate akili za upotovu, watende mambo yale yasiyostahili kutendwa. Wamejawa na udhalimu wa kila namna, uasherati, uovu, tamaa mbaya na hila. Wamejawa na husuda, uuaji, ugomvi, udanganyifu, hadaa na nia mbaya. Wao pia ni wasengenyaji, wasingiziaji, wanaomchukia Mungu, wajeuri, wenye kiburi na majivuno, wenye hila, wasiotii wazazi wao, wajinga, wasioamini, wasio na huruma na wakatili. Ingawa wanafahamu sheria ya haki ya Mungu kwamba watu wanaofanya mambo kama hayo wanastahili mauti, si kwamba wanaendelea kutenda hayo tu, bali pia wanakubaliana na wale wanaoyatenda.