Waroma 1:1-15
Waroma 1:1-15 Biblia Habari Njema (BHN)
Kutoka kwangu mimi Paulo, mtumishi wa Kristo Yesu, na mtume niliyeteuliwa na kuitwa kwa ajili ya kuhubiri Habari Njema ya Mungu. Hapo kale, Mungu aliwaahidi watu hii Habari Njema kwa njia ya manabii wake katika Maandiko Matakatifu. Hii Habari Njema inamhusu Mwana wa Mungu, Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye kuhusu ubinadamu wake, alikuwa mzawa wa Daudi; kuhusu utakatifu wake wa kimungu, alithibitishwa kwa uwezo mkuu kwamba ni Mwana wa Mungu kwa kufufuliwa kutoka kwa wafu. Kwa njia yake, mimi nimepewa neema ya kuwa mtume, ili kwa ajili yake niwaongoze watu wa mataifa yote wapate kuamini na kutii. Nyinyi ni miongoni mwa watu hao; mmeitwa muwe watu wake Yesu Kristo. Basi, nawaandikia nyinyi nyote mlioko Roma ambao Mungu anawapenda, akawateua muwe watu wake. Nawatakieni neema na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu na Bwana Yesu Kristo. Awali ya yote, namshukuru Mungu wangu kwa njia ya Yesu Kristo kwa ajili yenu nyote, kwa sababu imani yenu inasikika duniani kote. Mungu, ambaye ninamtumikia kwa moyo wangu wote katika kuhubiri Habari Njema ya Mwanae, ni shahidi wangu kwamba ninawakumbukeni daima katika sala zangu. Namwomba Mungu akipenda, anipatie nafasi nzuri ya kuja kwenu sasa. Kwa maana ninatamani sana kuwaoneni ili nipate kuwagawieni zawadi ya kiroho na kuwaimarisha. Ndiyo kusema, tutaimarishana: Imani yenu itaniimarisha mimi, na yangu itawaimarisha nyinyi. Ndugu zangu, nataka mjue kwamba mara nyingi nilikusudia kuwatembeleeni, lakini mpaka sasa nimezuiwa. Ningependa kupata mafanikio mema kati yenu kama nilivyopata kati ya watu wa mataifa mengine. Ninalo jukumu kwa watu wote, waliostaarabika na wasiostaarabika, wenye elimu na wasio na elimu. Ndiyo maana ninatamani pia kuihubiri Habari Njema kwenu nyinyi mlioko huko Roma.
Waroma 1:1-15 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Paulo, mtumwa wa Kristo Yesu, aliyeitwa kuwa mtume, na kutengwa aihubiri Injili ya Mungu; ambayo Mungu amekwisha kuiahidi kwa kinywa cha manabii wake katika Maandiko Matakatifu; yaani, habari za Mwanawe, aliyezaliwa katika ukoo wa Daudi kwa jinsi ya mwili, na kudhihirishwa kwa uweza kuwa Mwana wa Mungu, kwa jinsi ya roho ya utakatifu, kwa ufufuo wa wafu, Yesu Kristo Bwana wetu; ambaye katika yeye tulipokea neema na utume ili mataifa yote wapate kujitiisha kwa imani, kwa ajili ya jina lake; ambao katika hao ninyi mmekuwa wateule wa Yesu Kristo; kwa wote walioko Rumi, wapendwao na Mungu, walioitwa kuwa watakatifu. Neema na iwe kwenu na amani itokayo kwa Mungu Baba yetu, na kwa Bwana Yesu Kristo. Kwanza namshukuru Mungu wangu katika Yesu Kristo kwa ajili yenu nyote, kwa kuwa imani yenu inahubiriwa kote duniani. Kwa maana Mungu, nimwabuduye kwa roho yangu katika Injili ya Mwana wake, ni shahidi wangu jinsi niwatajavyo pasipo kukoma, siku zote katika sala zangu, nikiomba nije kwenu hivi karibu, Mungu akipenda kuifanikisha safari yangu. Kwa maana ninatamani sana kuwaona, nipate kuwapa karama ya rohoni, ili mfanywe imara; yaani, tufarijiane mimi na ninyi, kila mtu kwa imani ya mwenzake, yenu na yangu. Lakini, ndugu zangu, sipendi msiwe na habari, ya kuwa mara nyingi nilikusudia kuja kwenu, nikazuiliwa mpaka sasa, ili nipate kuwa na matunda kwenu ninyi pia kama nilivyo nayo katika Mataifa wengine. Nawiwa na Wagiriki na wasio Wagiriki, nawiwa na wenye hekima na wasio na hekima. Kwa hiyo, kwa upande wangu, mimi ni tayari kuihubiri Injili hata na kwenu ninyi mnaokaa Rumi.
Waroma 1:1-15 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Paulo, mtumwa wa Kristo Yesu, aliyeitwa kuwa mtume, na kutengwa aihubiri Injili ya Mungu; ambayo Mungu amekwisha kuiahidi kwa kinywa cha manabii wake katika maandiko matakatifu; yaani, habari za Mwanawe, aliyezaliwa katika ukoo wa Daudi kwa jinsi ya mwili, na kudhihirishwa kwa uweza kuwa Mwana wa Mungu, kwa jinsi ya roho ya utakatifu, kwa ufufuo wa wafu, Yesu Kristo Bwana wetu; ambaye katika yeye tulipokea neema na utume ili mataifa yote wapate kujitiisha kwa imani, kwa ajili ya jina lake; ambao katika hao ninyi mmekuwa wateule wa Yesu Kristo; kwa wote walioko Rumi, wapendwao na Mungu, walioitwa kuwa watakatifu. Neema na iwe kwenu na amani itokayo kwa Mungu Baba yetu, na kwa Bwana Yesu Kristo. Kwanza namshukuru Mungu wangu katika Yesu Kristo kwa ajili yenu nyote, kwa kuwa imani yenu inahubiriwa katika dunia nzima. Kwa maana Mungu, nimwabuduye kwa roho yangu katika Injili ya Mwana wake, ni shahidi wangu jinsi niwatajavyo pasipo kukoma, siku zote katika sala zangu, nikiomba nije kwenu hivi karibu, Mungu akipenda kuifanikisha safari yangu. Kwa maana ninatamani sana kuwaona, nipate kuwapa karama ya rohoni, ili mfanywe imara; yaani, tufarijiane mimi na ninyi, kila mtu kwa imani ya mwenzake, yenu na yangu. Lakini, ndugu zangu, sipendi msiwe na habari, ya kuwa mara nyingi nalikusudia kuja kwenu, nikazuiliwa hata sasa, ili nipate kuwa na matunda kwenu ninyi pia kama nilivyo nayo katika Mataifa wengine. Nawiwa na Wayunani na wasio Wayunani, nawiwa na wenye hekima na wasio na hekima. Kwa hiyo, kwa upande wangu, mimi ni tayari kuihubiri Injili hata na kwenu ninyi mnaokaa Rumi.
Waroma 1:1-15 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Paulo, mtumishi wa Kristo Yesu, aliyeitwa kuwa mtume na kutengwa kwa ajili ya Injili ya Mungu, Injili ambayo Mungu alitangulia kuiahidi kwa vinywa vya manabii wake katika Maandiko Matakatifu, yaani Injili inayomhusu Mwanawe, yeye ambaye kwa uzao wa mwili alikuwa mzao wa Daudi, na ambaye kwa uwezo wa Roho wa utakatifu alidhihirishwa kuwa Mwana wa Mungu kwa ufufuo wake kutoka kwa wafu, yaani Yesu Kristo, Bwana wetu. Kupitia kwake tumepokea neema na utume ili kuwaita watu wote wa mataifa waje kwenye utii utokanao na imani kwa ajili ya jina lake. Ninyi nyote pia mko miongoni mwa watu walioitwa ili wapate kuwa mali ya Yesu Kristo. Kwa wote walio Rumi wanaopendwa na Mungu na kuitwa kuwa watakatifu. Neema na amani zinazotoka kwa Mungu Baba yetu na kwa Bwana Yesu Kristo ziwe nanyi. Kwanza kabisa, namshukuru Mungu wangu kupitia kwa Yesu Kristo kwa ajili yenu nyote, kwa sababu imani yenu inatangazwa duniani kote. Kwa maana Mungu ninayemtumikia kwa moyo wangu wote katika kuhubiri Injili ya Mwanawe, ni shahidi wangu jinsi ninavyowakumbuka daima katika maombi yangu siku zote. Nami ninaomba kwamba hatimaye sasa kwa mapenzi ya Mungu, njia ipate kufunguliwa kwa ajili yangu ili nije kwenu. Ninatamani sana kuwaona ili nipate kuwapa karama za rohoni ili mwe imara, au zaidi, ninyi pamoja nami tuweze kutiana moyo katika imani sisi kwa sisi. Ndugu zangu, napenda mfahamu kwamba mara nyingi nimekusudia kuja kwenu (ingawa hadi sasa nimezuiliwa), ili nipate kuvuna mavuno miongoni mwenu kama nilivyovuna miongoni mwa watu wa Mataifa wengine. Mimi ni mdeni kwa Wayunani na kwa wasio Wayunani, kwa wenye hekima na kwa wasio na hekima. Ndiyo sababu ninatamani sana kuihubiri Injili kwenu pia ninyi mlioko Rumi.