Ufunuo 14:1-5
Ufunuo 14:1-5 Biblia Habari Njema (BHN)
Kisha, nikaona mlima Siyoni na Mwanakondoo amesimama juu yake; pamoja naye walikuwa watu 144,000 ambao juu ya paji za nyuso zao walikuwa wameandikwa jina la Mwanakondoo na jina la Baba yake. Basi, nikasikia sauti kutoka mbinguni, sauti iliyokuwa kama ya maji mengi na kama ya ngurumo kubwa. Sauti niliyosikia ilikuwa kama sauti ya wachezaji muziki wakipiga vinubi vyao. Walikuwa wanaimba wimbo mpya mbele ya kiti cha enzi na mbele ya wale viumbe hai wanne na wale wazee. Hakuna mtu aliyeweza kujifunza wimbo huo isipokuwa hao watu 144,000 waliokombolewa duniani. Watu hao ndio wale ambao hawakujichafua na wanawake, nao ni mabikira. Wao humfuata Mwanakondoo kokote aendako. Wamekombolewa kutoka miongoni mwa binadamu wengine, wakawa wa kwanza kutolewa kwa Mungu na kwa Mwanakondoo. Hawakupata kamwe kuwa waongo; hawana hatia yoyote.
Ufunuo 14:1-5 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kisha nikaona, na tazama, huyo Mwana-kondoo amesimama juu ya mlima Sayuni, na watu elfu mia moja na arubaini na nne pamoja naye, wenye jina lake na jina la Baba yake limeandikwa katika vipaji vya nyuso zao. Nami nikasikia sauti kutoka mbinguni, kama sauti ya maji mengi, na kama sauti ya radi kuu. Na hiyo sauti niliyoisikia ilikuwa kama sauti ya wapiga vinubi, wakivipiga vinubi vyao; na kuimba wimbo mpya mbele ya kile kiti cha enzi, na mbele ya wale wenye uhai wanne, na wale wazee; wala hakuna mtu aliyeweza kujifunza wimbo ule, ila wale elfu mia moja na arubaini na nne, walionunuliwa katika nchi. Hawa ndio wasiojitia unajisi na wanawake, kwa maana ni bikira. Hawa ndio wamfuatao Mwana-kondoo kila aendako. Hawa wamenunuliwa katika wanadamu, malimbuko kwa Mungu na kwa Mwana-kondoo. Na katika vinywa vyao haukuonekana uongo. Maana hawana mawaa.
Ufunuo 14:1-5 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Kisha nikaona, na tazama, huyo Mwana-Kondoo amesimama juu ya mlima Sayuni, na watu mia na arobaini na nne elfu pamoja naye, wenye jina lake na jina la Baba yake limeandikwa katika vipaji vya nyuso zao. Nami nikasikia sauti kutoka mbinguni, kama sauti ya maji mengi, na kama sauti ya radi kuu. Na hiyo sauti niliyoisikia ilikuwa kama sauti ya wapiga vinubi, wakivipiga vinubi vyao; na kuimba wimbo mpya mbele ya kile kiti cha enzi, na mbele ya wale wenye uhai wanne, na wale wazee; wala hapana mtu aliyeweza kujifunza wimbo ule, ila wale mia na arobaini na nne elfu, walionunuliwa katika nchi. Hawa ndio wasiotiwa unajisi pamoja na wanawake, kwa maana ni bikira. Hawa ndio wamfuatao Mwana-Kondoo kila aendako. Hawa wamenunuliwa katika wanadamu, malimbuko kwa Mungu na kwa Mwana-Kondoo. Na katika vinywa vyao haukuonekana uongo. Maana hawana mawaa.
Ufunuo 14:1-5 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Kisha nikatazama, na hapo mbele yangu Mwana-Kondoo alikuwa amesimama juu ya Mlima Sayuni. Pamoja naye walikuwa wale elfu mia moja na arobaini na nne wenye jina la Mwana-Kondoo na jina la Baba yake limeandikwa kwenye paji za nyuso zao. Nami nikasikia sauti kutoka mbinguni kama sauti ya maji mengi yaendayo kwa kasi na sauti kama ngurumo ya radi. Sauti hiyo niliyoisikia ilikuwa kama sauti ya wapiga vinubi wakipiga vinubi vyao. Nao wakaimba wimbo mpya mbele ya hicho kiti cha enzi, na mbele ya wale viumbe wanne wenye uhai, na wale wazee. Hakuna mtu yeyote aliyeweza kujifunza wimbo huo isipokuwa hao elfu mia moja na arobaini na nne waliokuwa wamekombolewa kutoka duniani. Hawa ndio wale ambao hawakujitia unajisi kwa wanawake, kwa kuwa wao ni bikira. Wao humfuata Mwana-Kondoo kila aendako. Hawa wamekombolewa kutoka miongoni mwa wanadamu wakawa malimbuko kwa Mungu na kwa Mwana-Kondoo. Vinywani mwao hapakuonekana uongo, wala hawakuwa na hatia yoyote.