Ufunuo 13:13-18
Ufunuo 13:13-18 Biblia Habari Njema (BHN)
Basi, huyu mnyama wa pili akafanya miujiza mikubwa hata akasababisha moto kutoka mbinguni ushuke duniani mbele ya watu. Aliwapotosha wakazi wa dunia kwa miujiza hiyo aliyojaliwa kutenda mbele ya mnyama wa kwanza. Aliwaambia wakazi wa dunia watengeneze sanamu kwa heshima ya yule mnyama aliyekuwa amejeruhiwa kwa upanga lakini akaishi tena. Kisha alijaliwa kuipulizia uhai hiyo sanamu ya yule mnyama wa kwanza, hata ikaweza kuongea na kuwaua watu wote ambao hawakuiabudu. Aliwalazimisha wote, wadogo na wakubwa, matajiri na maskini, watu huru na watumwa, watiwe alama juu ya mikono yao ya kulia au juu ya paji za nyuso zao. Akapiga marufuku mtu yeyote kununua au kuuza kitu isipokuwa tu mtu aliyetiwa alama hiyo, yaani jina la yule mnyama au tarakimu ya jina hilo. Hapa panatakiwa hekima! Mwenye akili anaweza kufafanua maana ya tarakimu ya mnyama huyo, maana ni tarakimu yenye maana ya mtu fulani. Tarakimu hiyo ni 666.
Ufunuo 13:13-18 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Naye afanya ishara kubwa, hata kufanya moto kushuka kutoka mbinguni uje juu ya nchi mbele ya wanadamu. Naye awakosesha wale wakaao juu ya nchi, kwa ishara zile alizopewa kuzifanya mbele ya huyo mnyama, akiwaambia wakaao juu ya nchi kumfanyia sanamu yule mnyama, aliyekuwa na jeraha la upanga naye akaishi. Akapewa kutia pumzi katika ile sanamu ya mnyama, ili ile sanamu ya mnyama iongee, na kuwafanya hao wote wasioisujudu sanamu ya mnyama wauawe. Naye awafanya wote, wadogo kwa wakubwa, na matajiri kwa maskini, na walio huru kwa watumwa, watiwe chapa katika mkono wao wa kulia, au katika vipaji vya nyuso zao; tena kwamba mtu awaye yote asiweze kununua wala kuuza, isipokuwa awe na chapa ile, yaani, jina la mnyama yule, au hesabu ya herufi za jina lake. Hapa ndipo penye hekima. Yeye aliye na akili, na aihesabu hesabu ya mnyama huyo; maana ni hesabu ya kibinadamu. Na hesabu yake ni mia sita, sitini na sita.
Ufunuo 13:13-18 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Naye afanya ishara kubwa, hata kufanya moto kushuka kutoka mbinguni uje juu ya nchi mbele ya wanadamu. Naye awakosesha wale wakaao juu ya nchi, kwa ishara zile alizopewa kuzifanya mbele ya huyo mnyama, akiwaambia wakaao juu ya nchi kumfanyia sanamu yule mnyama, aliyekuwa na jeraha la upanga naye akaishi. Akapewa kutia pumzi katika ile sanamu ya mnyama, hata ile sanamu ya mnyama inene, na kuwafanya hao wote wasioisujudu sanamu ya mnyama wauawe. Naye awafanya wote, wadogo kwa wakubwa, na matajiri kwa maskini, na walio huru kwa watumwa, watiwe chapa katika mkono wao wa kuume, au katika vipaji vya nyuso zao; tena kwamba mtu awaye yote asiweze kununua wala kuuza, isipokuwa ana chapa ile, yaani, jina la mnyama yule, au hesabu ya jina lake. Hapa ndipo penye hekima. Yeye aliye na akili, na aihesabu hesabu ya mnyama huyo; maana ni hesabu ya kibinadamu. Na hesabu yake ni mia sita, sitini na sita.
Ufunuo 13:13-18 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Naye akafanya ishara kuu na za ajabu, hata kusababisha moto kushuka toka mbinguni kuja duniani watu wakiona waziwazi. Kwa sababu ya zile ishara alizokuwa amepewa uwezo wa kuzifanya kwa niaba ya yule mnyama wa kwanza, akawadanganya watu walioishi duniani. Akawaamuru wasimamishe sanamu kwa heshima ya yule mnyama aliyekuwa amejeruhiwa kwa upanga lakini akaishi. Akapewa uwezo wa kuipa pumzi ile sanamu ya yule mnyama wa kwanza, ili iweze kusema na kuwasababisha wale wote waliokataa kuiabudu hiyo sanamu kuuawa. Pia alimlazimisha kila mmoja, mdogo na mkubwa, tajiri na maskini, mtu huru na mtumwa, atiwe chapa kwenye mkono wake wa kuume au kwenye paji la uso wake, ili mtu yeyote asiweze kununua wala kuuza isipokuwa amekuwa na hiyo chapa, ambayo ni jina la huyo mnyama au tarakimu za jina lake. Hapa ndipo penye hekima. Yeye aliye na ufahamu na ahesabu tarakimu za huyo mnyama, kwa maana ni tarakimu za kibinadamu. Tarakimu zake ni mia sita sitini na sita (666).