Zaburi 93:1-5
Zaburi 93:1-5 Biblia Habari Njema (BHN)
Mwenyezi-Mungu anatawala; amejivika fahari kuu! Mwenyezi-Mungu amevaa fahari na nguvu! Ameuimarisha ulimwengu, nao hautatikisika kamwe. Kiti chako cha enzi ni imara tangu kale; wewe umekuwapo kabla ya nyakati zote. Vilindi vimetoa sauti, ee Mwenyezi-Mungu; naam, vimepaza sauti yake, vilindi vyapaza tena mvumo wake. Mwenyezi-Mungu ana enzi kuu juu mbinguni, ana nguvu kuliko mlio wa bahari, ana nguvu kuliko mawimbi ya maji. Ee Mwenyezi-Mungu, maagizo yako ni thabiti; nyumba yako ni takatifu milele na milele.
Zaburi 93:1-5 Swahili Revised Union Version (SRUV)
BWANA ametamalaki, amejivika adhama, BWANA amejivika, ukuu na nguvu, kama mavazi ya kifalme. Naam, ulimwengu umethibitika usitikisike; Kiti chako kimekuwa thabiti tokea zamani; Wewe ndiwe uliye tangu milele. Ee BWANA, mito imepaza, Mito imepaza sauti zake, Mito imepaza uvumi wake. Kupita sauti ya maji mengi, maji makuu, Kupita mawimbi ya bahari yaumkayo, BWANA Aliye Juu ndiye mwenye ukuu. Shuhuda zako ni amini sana; Utakatifu ndio uifaao nyumba yako, Ee BWANA, milele na milele.
Zaburi 93:1-5 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
BWANA ametamalaki, amejivika adhama, BWANA amejivika, na kujikaza nguvu. Naam, ulimwengu umethibitika usitikisike; Kiti chako kimekuwa thabiti tokea zamani; Wewe ndiwe uliye tangu milele. Ee BWANA, mito imepaza, Mito imepaza sauti zake, Mito imepaza uvumi wake. Kupita sauti ya maji mengi, maji makuu, Kupita mawimbi ya bahari yaumkayo, BWANA Aliye juu ndiye mwenye ukuu. Shuhuda zako ni amini sana; Utakatifu ndio uifaao nyumba yako, Ee BWANA, milele na milele.
Zaburi 93:1-5 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
BWANA anatawala, amejivika utukufu; BWANA amejivika utukufu tena amejivika nguvu. Dunia imewekwa imara, haitaondoshwa. Kiti chako cha enzi kimekuwa thabiti tangu zamani; wewe umekuwa tangu milele. Bahari zimepaza, Ee BWANA, bahari zimepaza sauti zake; bahari zimepaza sauti za mawimbi yake. Yeye ni mkuu kuliko ngurumo ya maji makuu, ni mkuu kuliko mawimbi ya bahari: BWANA aishiye juu sana ni mkuu. Ee BWANA, sheria zako ni imara; utakatifu umepamba nyumba yako pasipo mwisho.