Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Zaburi 89:1-18

Zaburi 89:1-18 Biblia Habari Njema (BHN)

Ee Mwenyezi-Mungu, nitaimba fadhili zako milele; nitavitangazia vizazi vyote uaminifu wako. Natamka kuwa fadhili zako zadumu milele; uaminifu wako ni thabiti kama mbingu. Umesema: “Nimefanya agano na mteule wangu, nimemwapia mtumishi wangu Daudi: ‘Daima nitamweka mzawa wako kuwa mfalme, tena nitaudumisha ufalme wako milele.’” Mbingu na zisifu maajabu yako, ee Mwenyezi-Mungu; uaminifu wako usifiwe katika kusanyiko la watakatifu. Nani mbinguni awezaye kulinganishwa nawe ee Mwenyezi-Mungu? Nani aliye sawa nawe kati ya viumbe vya mbinguni? Wewe waogopwa katika baraza la watakatifu; wote wanaokuzunguka wanatiwa hofu kuu. Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wa majeshi, ni nani mwenye nguvu kama wewe, ee Mwenyezi-Mungu? Uaminifu umekuzunguka pande zote. Wewe watawala machafuko ya bahari; mawimbi yake yakiinuka, wayatuliza. Uliliponda joka Rahabu na kuliua; uliwatawanya adui zako kwa nguvu yako. Mbingu ni zako na dunia ni yako pia; ulimwengu na vitu vyote vilivyomo wewe uliviumba. Wewe uliumba kaskazini na kusini; milima Tabori na Hermoni inakusifu kwa furaha. Mkono wako una nguvu, mkono wako una nguvu na umeshinda! Uadilifu na haki ni msingi wa utawala wako; fadhili na uaminifu vyakutangulia! Heri watu wanaojua kukushangilia, wanaoishi katika mwanga wa wema wako, ee Mwenyezi-Mungu. Wanafurahi mchana kutwa kwa sababu yako, na kukusifu kwa ajili ya uadilifu wako. Wewe ndiwe fahari na nguvu yao; kwa wema wako twapata ushindi. Ee Mwenyezi-Mungu, mlinzi wetu ni wako, mfalme wetu ametoka kwako ewe Mtakatifu wa Israeli.

Shirikisha
Soma Zaburi 89

Zaburi 89:1-18 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Fadhili za BWANA nitaziimba milele; Kwa kinywa changu nitavijulisha vizazi vyote uaminifu wako. Maana nimesema, Fadhili zitajengwa milele; Katika mbingu utauthibitisha uaminifu wako. Nimefanya agano na mteule wangu, Nimemuapia Daudi, mtumishi wangu. Wazao wako nitawaimarisha milele, Nitakijenga kiti chako cha enzi hata milele. Ee BWANA, mbingu zitayasifu maajabu yako, Uaminifu wako katika kusanyiko la watakatifu. Maana ni nani katika mbingu awezaye kulinganishwa na BWANA? Ni nani afananaye na BWANA miongoni mwa malaika? Mungu huogopwa sana barazani pa watakatifu, Ni wa kuhofiwa kuliko wote wanaomzunguka. BWANA, Mungu wa majeshi, Ni nani aliye hodari kama Wewe, Ee YAHU? Na uaminifu wako unakuzunguka. Wewe ndiwe ukitawalaye kiburi cha bahari. Mawimbi yake yainukapo, wewe unayatuliza. Ndiwe uliyemponda Rahabu akawa kama aliyeuawa, Kwa mkono hodari umewatawanya wakuchukiao. Mbingu ni mali yako, nchi nayo ni mali yako, Ulimwengu na vyote viujazavyo Ndiwe uliyeupiga msingi wake. Kaskazini na kusini ndiwe uliyeziumba, Tabori na Hermoni hulifurahia jina lako. Mkono wako ni mkono wenye uweza, Mkono wako una nguvu, Mkono wako wa kulia umetukuka. Haki na hukumu ndio msingi wa kiti chako, Fadhili na kweli zimo mbele za uso wako. Heri watu wale waijuao sauti ya shangwe, Ee BWANA, waendao, katika nuru ya uso wako. Kwa jina lako hufurahi mchana kutwa, Na kwa haki yako hutukuzwa. Maana fahari ya nguvu zao ni Wewe, Na kwa radhi yako pembe yetu itatukuka. Maana ngao yetu ni BWANA, Na mfalme wetu ni wake Mtakatifu wa Israeli.

Shirikisha
Soma Zaburi 89

Zaburi 89:1-18 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Fadhili za BWANA nitaziimba milele; Kwa kinywa changu nitavijulisha vizazi vyote uaminifu wako. Maana nimesema, Fadhili zitajengwa milele; Katika mbingu utauthibitisha uaminifu wako. Nimefanya agano na mteule wangu, Nimemuapia Daudi, mtumishi wangu. Wazao wako nitawafanya imara milele, Nitakijenga kiti chako cha enzi hata milele. Ee BWANA, mbingu zitayasifu maajabu yako, Uaminifu wako katika kusanyiko la watakatifu. Maana ni nani katika mbingu awezaye kulinganishwa na BWANA? Ni nani afananaye na BWANA miongoni mwa malaika? Mungu huogopwa sana barazani pa watakatifu, Ni wa kuhofiwa kuliko wote wanaomzunguka. BWANA, Mungu wa majeshi, Ni nani aliye hodari kama Wewe, Ee YAHU? Na uaminifu wako unakuzunguka. Wewe ndiwe ukitawalaye kiburi cha bahari. Mawimbi yake yainukapo wayatuliza Wewe. Ndiwe uliyemseta Rahabu akawa kama aliyeuawa, Kwa mkono hodari umewatawanya wakuchukiao. Mbingu ni mali yako, nchi nayo ni mali yako, Ulimwengu na vyote viujazavyo Ndiwe uliyeupiga msingi wake. Kaskazini na kusini ndiwe uliyeziumba, Tabori na Hermoni hulifurahia jina lako. Mkono wako ni mkono wenye uweza, Mkono wako una nguvu, Mkono wako wa kuume umetukuka. Haki na hukumu ndio msingi wa kiti chako, Fadhili na kweli zahudhuria mbele za uso wako. Heri watu wale waijuao sauti ya shangwe, Ee BWANA, huenenda katika nuru ya uso wako. Kwa jina lako hufurahi mchana kutwa, Na kwa haki yako hutukuzwa. Maana fahari ya nguvu zao ni Wewe, Na kwa radhi yako pembe yetu itatukuka. Maana ngao yetu ina BWANA, Na mfalme wetu ni wake Mtakatifu wa Israeli.

Shirikisha
Soma Zaburi 89

Zaburi 89:1-18 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Nitaimba juu ya upendo mkuu wa BWANA milele; kwa kinywa changu nitajulisha uaminifu wako ujulikane kwa vizazi vyote. Nitatangaza kuwa upendo wako unasimama imara milele na uaminifu wako umeuthibitisha mbinguni. Ulisema, “Nimefanya agano na mteule wangu, nimemwapia mtumishi wangu Daudi, ‘Nitaimarisha uzao wako milele na kudumisha ufalme wako kwa vizazi vyote.’ ” Ee BWANA, mbingu zinayasifu maajabu yako, uaminifu wako pia katika kusanyiko la watakatifu. Kwa kuwa ni nani katika mbingu anayeweza kulinganishwa na BWANA? Ni nani miongoni mwa viumbe vya mbinguni aliye kama BWANA? Katika kusanyiko la watakatifu, Mungu huogopwa sana, anahofiwa kuliko wote wanaomzunguka. Ee BWANA Mwenye Nguvu Zote, ni nani aliye kama wewe? Ee BWANA, wewe ni mwenye nguvu, na uaminifu wako unakuzunguka. Wewe unatawala bahari yenye msukosuko; wakati mawimbi yake yanapoinuka, wewe unayatuliza. Wewe ulimponda Rahabu kama mmojawapo wa waliochinjwa; kwa mkono wako wenye nguvu, uliwatawanya adui zako. Mbingu ni zako, nayo nchi pia ni yako, uliuwekea ulimwengu msingi pamoja na vyote vilivyomo. Uliumba kaskazini na kusini; Tabori na Hermoni wanaliimbia jina lako kwa furaha. Mkono wako umejaa uwezo; mkono wako una nguvu, mkono wako wa kuume umetukuzwa. Haki na hukumu ndio msingi wa kiti chako cha enzi; upendo na uaminifu vinakutangulia. Heri ni wale ambao wamejifunza kukusifu kwa shangwe, wanaotembea katika mwanga wa uwepo wako, Ee BWANA. Wanashangilia katika jina lako mchana kutwa, wanafurahi katika haki yako. Kwa kuwa wewe ni utukufu na nguvu yao, kwa wema wako unatukuza pembe yetu. Naam, ngao yetu ni mali ya BWANA, na mfalme wetu mali ya Aliye Mtakatifu wa Israeli.

Shirikisha
Soma Zaburi 89

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha