Zaburi 68:1-10
Zaburi 68:1-10 Biblia Habari Njema (BHN)
Mungu ainuka, na maadui zake watawanyika; wanaomchukia wakimbia mbali naye! Kama moshi unavyopeperushwa na upepo, ndivyo anavyowapeperusha; kama nta inavyoyeyuka karibu na moto, ndivyo waovu wanavyoangamia mbele ya Mungu! Lakini waadilifu hufurahi ajapo Mungu, hushangilia na kuimba kwa furaha. Mwimbieni Mungu, lisifuni jina lake; mtengenezeeni njia yake apandaye mawinguni. Jina lake ni Mwenyezi-Mungu; furahini mbele yake. Mungu akaaye mahali pake patakatifu, ni Baba wa yatima na mlinzi wa wajane. Mungu huwapa fukara makao ya kudumu, huwafungua wafungwa na kuwapa fanaka. Lakini waasi wataishi katika nchi kame. Ee Mungu, ulipowaongoza watu wako, uliposafiri kule jangwani, dunia ilitetemeka, mbingu zilitiririsha mvua; kwa kuweko kwako, Mungu wa Sinai, naam, kwa kuweko kwako, Mungu wa Israeli! Ee Mungu, uliinyeshea nchi mvua nyingi, uliiburudisha nchi yako ilipokuwa imechakaa. Watu wako wakapata humo makao; ukawaruzuku maskini kwa wema wako.
Zaburi 68:1-10 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Mungu na ainuke, adui zake watawanyike, Nao wamchukiao huukimbia uso wake. Kama moshi upeperushwavyo, Ndivyo uwapeperushavyo wao; Kama nta iyeyukavyo mbele ya moto, Ndivyo waovu wapoteavyo usoni pa Mungu. Bali wenye haki hufurahi, Na kuushangilia uso wa Mungu, Naam, hupiga kelele kwa furaha. Mwimbieni Mungu, lisifuni jina lake, Mwimbieni wimbo yeye apitaye katika mawingu, Jina lake ni YAHU; Shangilieni mbele zake. Baba wa yatima na mwamuzi wa wajane, Ni Mungu aliye katika kao lake takatifu. Mungu huwapa wapweke makao yao; Huwapa wafungwa uhuru na kuwafanikisha; Bali wakaidi huishi katika nchi kavu. Ee Mungu, ulipowaongoza watu wako, Ulipopita nyikani, Nchi ilitetemeka Naam, mbingu zilidondoka usoni pa Mungu; Hata Sinai usoni pa Mungu; Mungu wa Israeli. Ee Mungu, ulinyesha mvua ya neema; Urithi wako ulipochoka uliutia nguvu. Watu wako wakafanya makao ya huko; Ee Mungu, kwa wema wako uliwaruzuku walioonewa.
Zaburi 68:1-10 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Mungu huondoka, adui zake wakatawanyika, Nao wamchukiao huukimbia uso wake. Kama moshi upeperushwavyo, Ndivyo uwapeperushavyo wao; Kama nta iyeyukavyo mbele ya moto, Ndivyo waovu wapoteavyo usoni pa Mungu. Bali wenye haki hufurahi, Na kuushangilia uso wa Mungu, Naam, hupiga kelele kwa furaha. Mwimbieni Mungu, lisifuni jina lake, Mtengenezeeni njia ya barabara, Apitaye majangwani kama mpanda farasi; Jina lake ni YAHU; shangilieni mbele zake. Baba wa yatima na mwamuzi wa wajane, Mungu katika kao lake takatifu. Mungu huwakalisha wapweke nyumbani; Huwatoa wafungwa wakae hali ya kufanikiwa; Bali wakaidi hukaa katika nchi kavu. Ee Mungu, ulipotoka mbele ya watu wako, Ulipopita nyikani, Nchi ilitetemeka Naam, mbingu zilidondoka usoni pa Mungu; Hata Sinai usoni pa Mungu; Mungu wa Israeli. Ee Mungu, ulinyesha mvua ya neema; Urithi wako ulipochoka uliutia nguvu. Kabila yako ilifanya kao lake huko; Ee Mungu, kwa wema wako uliwaruzuku walioonewa.
Zaburi 68:1-10 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Mungu na ainuke, watesi wake watawanyike, adui zake na wakimbie mbele zake. Kama moshi unavyopeperushwa na upepo, vivyo hivyo uwapeperushe mbali, kama nta inavyoyeyuka kwenye moto, vivyo hivyo waovu na waangamie mbele za Mungu. Bali wenye haki na wafurahi, washangilie mbele za Mungu, wafurahi na kushangilia. Mwimbieni Mungu, liimbieni sifa jina lake, mtukuzeni yeye anayepita juu ya mawingu: jina lake ni BWANA, furahini mbele zake. Baba wa yatima, mtetezi wa wajane, ni Mungu katika makao yake matakatifu. Mungu huwaweka wapweke katika jamaa, huwaongoza wafungwa wakiimba, bali waasi huishi katika nchi kame. Ee Mungu, ulipowatangulia watu wako, ulipopita nyikani, dunia ilitikisika, mbingu zikanyesha mvua, mbele za Mungu, Yule wa Sinai, mbele za Mungu, Mungu wa Israeli. Ee Mungu, ulinyesha mvua nyingi na kuiburudisha ardhi iliyokuwa imechoka. Ee Mungu, watu wako waliishi huko, nawe kwa wingi wa utajiri wako uliwapa maskini mahitaji yao.