Zaburi 49:1-9
Zaburi 49:1-9 Biblia Habari Njema (BHN)
Sikieni jambo hili enyi watu wote! Tegeni sikio enyi wakazi wote wa dunia; sikilizeni nyote, wakubwa kwa wadogo, matajiri na maskini kwa pamoja. Maneno yangu yatakuwa mazitomazito; mimi nitasema maneno ya hekima. Nitatega sikio nisikilize methali, nitafafanua kitendawili kwa muziki wa zeze. Ya nini niogope siku mbaya, wakati nizungukwapo na uovu wa adui? Watu waovu hutegemea mali zao, hujisifia wingi wa utajiri wao. Lakini binadamu hawezi kamwe kujikomboa mwenyewe; hawezi kumlipa Mungu bei ya maisha yake, maana fidia ya maisha ni kubwa mno. Hawezi kutoa kitu chochote kinachotosha, kimwezeshe aendelee kuishi daima, asipate kuonja kaburi.
Zaburi 49:1-9 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Sikieni haya, enyi mataifa yote; Sikilizeni, ninyi nyote mnaokaa duniani. Watu wakuu na watu wadogo wote pia, Tajiri na maskini wote pamoja. Kinywa changu kitanena hekima, Na fikira za moyo wangu zitakuwa za busara. Nitatega sikio langu nisikie mithali, Na kufumbua fumbo langu kwa kinubi. Kwa nini niogope wakati wa shida, Ubaya ukinizunguka miguuni pangu? Ambao wanazitumainia mali zao, Na kujisifia wingi wa utajiri wao; Hakuna mtu awezaye kumkomboa ndugu yake, Wala kumlipa Mungu fidia kwa ajili ya maisha yake, (Maana fidia ya nafsi zao ina gharama, Wala hawezi kuitoa hata milele;) ndipo aishi milele asilione kaburi.
Zaburi 49:1-9 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Sikieni haya, enyi mataifa yote; Sikilizeni, ninyi nyote mnaokaa duniani. Watu wakuu na watu wadogo wote pia, Tajiri na maskini wote pamoja. Kinywa changu kitanena hekima, Na fikira za moyo wangu zitakuwa za busara. Nitatega sikio langu nisikie mithali, Na kufumbua fumbo langu kwa kinubi Kwa nini niogope siku za uovu, Ubaya ukinizunguka miguuni pangu? Wa hao wanaozitumainia mali zao, Na kujisifia wingi wa utajiri wao; Hakuna mtu awezaye kumkomboa ndugu yake, Wala kumpa Mungu fidia kwa ajili yake, (Maana fidia ya nafsi zao ina gharama, Wala hana budi kuiacha hata milele;) ili aishi sikuzote asilione kaburi.
Zaburi 49:1-9 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Sikieni haya, enyi mataifa yote, sikilizeni, ninyi wote mnaoishi dunia hii. Wakubwa kwa wadogo, matajiri na maskini pamoja: Kinywa changu kitasema maneno ya hekima, usemi wa moyo wangu utatoa ufahamu. Nitatega sikio langu nisikilize mithali, nitafafanua kitendawili kwa zeze: Kwa nini niogope siku mbaya zinapokuja, wakati wadanganyifu waovu wanaponizunguka, wale wanaotegemea mali yao na kujivunia utajiri wao mwingi? Hakuna mwanadamu yeyote awezaye kuukomboa uhai wa mwingine, au kumpa Mungu fidia kwa ajili yake. Fidia ya uhai ni gharama kubwa, hakuna malipo yoyote yanayotosha, ili aishi milele na asione uharibifu.