Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Zaburi 49:1-20

Zaburi 49:1-20 Biblia Habari Njema (BHN)

Sikieni jambo hili enyi watu wote! Tegeni sikio enyi wakazi wote wa dunia; sikilizeni nyote, wakubwa kwa wadogo, matajiri na maskini kwa pamoja. Maneno yangu yatakuwa mazitomazito; mimi nitasema maneno ya hekima. Nitatega sikio nisikilize methali, nitafafanua kitendawili kwa muziki wa zeze. Ya nini niogope siku mbaya, wakati nizungukwapo na uovu wa adui? Watu waovu hutegemea mali zao, hujisifia wingi wa utajiri wao. Lakini binadamu hawezi kamwe kujikomboa mwenyewe; hawezi kumlipa Mungu bei ya maisha yake, maana fidia ya maisha ni kubwa mno. Hawezi kutoa kitu chochote kinachotosha, kimwezeshe aendelee kuishi daima, asipate kuonja kaburi. Yeye afahamu kuwa hata wenye hekima hufa, wapumbavu hali kadhalika na watu wajinga. Wote hao huwaachia wengine mali zao. Makaburi ni makao yao hata milele; ni makao yao vizazi hata vizazi, ingawa hapo awali walimiliki ardhi. Binadamu hatadumu katika fahari yake; atakufa tu kama mnyama. Hayo ndiyo yawapatao wanaojiamini kipumbavu, ndio mwisho wa wale wanaojivunia mali zao. Wataongozwa kama kondoo hadi kuzimu, kifo kitakuwa mchungaji wao. Watashuka moja kwa moja kaburini. Miili yao itaozea huko, Kuzimu kutakuwa makao yao. Lakini Mungu ataniokoa na kuzimu. Atanisalimisha kutoka huko. Usihangaike ukiona mtu anatajirika, wala mali yake ikiongezeka zaidi na zaidi. Maana atakapokufa hatachukua chochote, mali yake haitashuka huko chini pamoja naye. Ajapojikuza katika maisha haya, na kusifiwa kwa sababu ya kufanikiwa, atajiunga na wazee waliomtangulia kufa, ambao hawawezi kuona tena mwanga. Binadamu hatadumu milele katika fahari yake, atakufa tu kama mnyama.

Shirikisha
Soma Zaburi 49

Zaburi 49:1-20 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Sikieni haya, enyi mataifa yote; Sikilizeni, ninyi nyote mnaokaa duniani. Watu wakuu na watu wadogo wote pia, Tajiri na maskini wote pamoja. Kinywa changu kitanena hekima, Na fikira za moyo wangu zitakuwa za busara. Nitatega sikio langu nisikie mithali, Na kufumbua fumbo langu kwa kinubi. Kwa nini niogope wakati wa shida, Ubaya ukinizunguka miguuni pangu? Ambao wanazitumainia mali zao, Na kujisifia wingi wa utajiri wao; Hakuna mtu awezaye kumkomboa ndugu yake, Wala kumlipa Mungu fidia kwa ajili ya maisha yake, (Maana fidia ya nafsi zao ina gharama, Wala hawezi kuitoa hata milele;) ndipo aishi milele asilione kaburi. Naam, ataliona, hata wenye hekima hufa; Mpumbavu na mjinga hupotea pamoja, Na kuwaachia wengine mali zao. Makaburi ni nyumba zao hata milele, Maskani zao vizazi hata vizazi. Japo waliwahi kuyamiliki mashamba, Kwa majina yao wenyewe. Lakini mwanadamu hadumu katika heshima, Bali amefanana na wanyama wapoteao. Hiyo ndiyo njia yao, ujinga wao, Nao walioko baada yao huyaridhia maneno yao. Kama kondoo wamewekwa kwenda kuzimu, Na kifo kitakuwa mchungaji wao; Watu wanyofu watawamiliki asubuhi; Miili yao itaoza, kao lao ni kuzimu. Bali Mungu atanikomboa nafsi yangu, Atanitoa mkononi mwa kuzimu, maana atanipokea. Usiogope mtu atakapopata utajiri, Na fahari ya nyumba yake itakapoongezeka. Maana atakapokufa hatachukua chochote; Utukufu wake hautashuka ukimfuata. Ajapojibariki nafsi yake alipokuwa hai, Na watu watakusifu ukijitendea mema, Atakwenda kwenye kizazi cha baba zake Hawataona nuru hata milele. Mwanadamu mwenye heshima, iwapo hana akili, Amefanana na wanyama wapoteao.

Shirikisha
Soma Zaburi 49

Zaburi 49:1-20 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Sikieni haya, enyi mataifa yote; Sikilizeni, ninyi nyote mnaokaa duniani. Watu wakuu na watu wadogo wote pia, Tajiri na maskini wote pamoja. Kinywa changu kitanena hekima, Na fikira za moyo wangu zitakuwa za busara. Nitatega sikio langu nisikie mithali, Na kufumbua fumbo langu kwa kinubi Kwa nini niogope siku za uovu, Ubaya ukinizunguka miguuni pangu? Wa hao wanaozitumainia mali zao, Na kujisifia wingi wa utajiri wao; Hakuna mtu awezaye kumkomboa ndugu yake, Wala kumpa Mungu fidia kwa ajili yake, (Maana fidia ya nafsi zao ina gharama, Wala hana budi kuiacha hata milele;) ili aishi sikuzote asilione kaburi. Naam, ataliona, hata wenye hekima hufa; Mpumbavu na mjinga hupotea pamoja, Na kuwaachia wengine mali zao. Makaburi ni nyumba zao hata milele, Maskani zao vizazi hata vizazi. Hao waliotaja mashamba yao Kwa majina yao wenyewe. Lakini mwanadamu hadumu katika heshima, Bali amefanana na wanyama wapoteao. Hiyo ndiyo njia yao, ujinga wao, Nao walioko baada yao huyaridhia maneno yao. Kama kondoo wamewekwa kwenda kuzimu, Na mauti itawachunga; Watu wanyofu watawamiliki asubuhi; Umbo lao litachakaa, kao lao ni kuzimu. Bali Mungu atanikomboa nafsi yangu, Atanitoa mkononi mwa kuzimu, maana atanikaribisha. Usiogope mtu atakapopata utajiri, Na fahari ya nyumba yake itakapozidi. Maana atakapokufa hatachukua cho chote; Utukufu wake hautashuka ukimfuata. Ajapojibariki nafsi yake alipokuwa hai, Na watu watakusifu ukijitendea mema, Atakwenda kwenye kizazi cha baba zake Hawataona nuru hata milele. Mwanadamu mwenye heshima, iwapo hana akili, Amefanana na wanyama wapoteao.

Shirikisha
Soma Zaburi 49

Zaburi 49:1-20 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

Sikieni haya, enyi mataifa yote, sikilizeni, ninyi wote mnaoishi dunia hii. Wakubwa kwa wadogo, matajiri na maskini pamoja: Kinywa changu kitasema maneno ya hekima, usemi wa moyo wangu utatoa ufahamu. Nitatega sikio langu nisikilize mithali, nitafafanua kitendawili kwa zeze: Kwa nini niogope siku mbaya zinapokuja, wakati wadanganyifu waovu wanaponizunguka, wale wanaotegemea mali yao na kujivunia utajiri wao mwingi? Hakuna mwanadamu yeyote awezaye kuukomboa uhai wa mwingine, au kumpa Mungu fidia kwa ajili yake. Fidia ya uhai ni gharama kubwa, hakuna malipo yoyote yanayotosha, ili aishi milele na asione uharibifu. Wote wanaona kwamba watu wenye hekima hufa; wajinga na wapumbavu vivyo hivyo huangamia na kuwaachia wengine mali yao. Makaburi yao yatabaki kuwa nyumba zao za milele, makao yao vizazi vyote; ingawa walikuwa na mashamba na kuyaita kwa majina yao. Lakini mwanadamu, licha ya utajiri wake, hadumu; anafanana na mnyama aangamiaye. Hii ndiyo hatima ya wale wanaojitumainia wenyewe, pia ya wafuasi wao, waliothibitisha misemo yao. Kama kondoo, wamewekewa kwenda kaburini, nacho kifo kitawala. Wanyofu watawatawala asubuhi, maumbile yao yataozea kaburini, mbali na majumba yao makubwa ya fahari. Lakini Mungu atakomboa uhai wangu dhidi ya kaburi; hakika atanichukua kwake. Usitishwe mtu anapotajirika, fahari ya nyumba yake inapoongezeka, kwa maana hatachukua chochote atakapokufa, fahari yake haitashuka pamoja naye. Ingawa alipokuwa akiishi alijihesabu kuwa heri, na wanadamu wanakusifu unapofanikiwa, atajiunga na kizazi cha baba zake, ambao hawataona kamwe nuru ya uzima. Wanadamu wenye utajiri bila ufahamu ni kama wanyama wanaoangamia.

Shirikisha
Soma Zaburi 49