Zaburi 44:1-26
Zaburi 44:1-26 Biblia Habari Njema (BHN)
Ee Mungu, sisi tumesikia kwa masikio yetu, wazee wetu wametusimulia mambo uliyotenda nyakati zao, naam, mambo uliyotenda hapo kale: Kwa mkono wako mwenyewe uliyafukuza mataifa mengine, na mahali pao ukawakalisha watu wako; uliyaadhibu mataifa mengine, na kuwafanikisha watu wako. Watu wako hawakuitwaa nchi kwa silaha zao, wala hawakupata ushindi kwa nguvu zao; ila uliwasalimisha kwa mkono wako mwenyewe, kwa kuwaangazia uso wako, kwani wewe uliwapenda. Wewe ni mfalme wangu na Mungu wangu! Wawajalia ushindi wazawa wa Yakobo. Kwa nguvu yako twawashinda maadui zetu, kwa jina lako twawakanyaga wanaotushambulia. Mimi siutegemei upinde wangu, wala upanga wangu hauwezi kuniokoa. Wewe ndiwe uliyetuokoa na maadui zetu; uliwavuruga wale waliotuchukia. Daima tutaona fahari juu yako, ee Mungu; tutakutolea shukrani milele. Lakini sasa umetuacha na kutufedhehesha; huandamani tena na majeshi yetu. Umetufanya tuwakimbie maadui zetu, nao wakaziteka nyara mali zetu. Umetufanya kama kondoo wanaopelekwa kuchinjwa; umetutawanya kati ya mataifa mengine. Umewauza watu wako kwa bei ya chini; wala hukupata faida yoyote. Umetufanya kuwa kioja kwa jirani zetu, nao wanatudhihaki na kutucheka. Umetufanya tudharauliwe na watu wa mataifa; wanatutikisia vichwa vyao kwa kutupuuza. Mchana kutwa fedheha yaniandama, na uso wangu umejaa aibu tele kwa maneno na madharau ya wenye kunitukana, kwa kukabiliwa na maadui zangu na walipiza kisasi. Hayo yote yametupata sisi ijapokuwa hatujakusahau, wala hatujavunja agano lako. Hatujakuasi wewe, wala hatujaziacha njia zako. Hata hivyo umetuacha hoi kati ya wanyama wakali; umetuacha katika giza kuu. Tungalikuwa tumekusahau wewe Mungu wetu, tukamkimbilia mungu wa uongo, ee Mungu, ungalikwisha jua jambo hilo, kwa maana wewe wazijua siri za moyoni. Lakini kwa ajili yako twakikabili kifo kila siku; tunatendewa kama kondoo wanaopelekwa kuchinjwa. Amka, ee Bwana! Mbona umelala? Inuka! Tafadhali usitutupe milele! Mbona wajificha mbali nasi, na kusahau dhiki na mateso yetu? Tumedidimia hata mavumbini, tumegandamana na ardhi. Uinuke, uje kutusaidia! Utukomboe kwa sababu ya fadhili zako.
Zaburi 44:1-26 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ee Mungu, tumesikia kwa masikio yetu Baba zetu wametuambia, Matendo uliyoyatenda siku zao, siku za kale. Wewe kwa mkono wako uliwafukuza mataifa, Ukawakalisha wao. Wewe uliwatesa watu wa nchi, Ukawafanikisha wao. Maana hawakuitwaa nchi kwa upanga wao, Wala hawakupata ushindi kwa mkono wao; Bali mkono wako wa kulia, naam, mkono wako, Na nuru ya uso wako, kwa kuwa ulipendezwa nao. Ee Mungu, Wewe ndiwe mfalme wangu, Uagize mambo ya wokovu kwa Yakobo. Kwa nguvu zako tutawaangusha watesi wetu; Kwa jina lako tutawakanyaga watupingao. Maana sitautumainia upinde wangu, Wala upanga wangu hauwezi kuniokoa. Bali Wewe ndiwe uliyetuokoa kutoka kwa watesi wetu; Na watuchukiao umewaaibisha. Tumejisifia Mungu mchana kutwa, Na jina lako tutalishukuru milele. Lakini umetutupa, umetufedhehesha, Wala huendi na majeshi yetu. Waturudisha nyuma tukampa mtesi kisogo, Na watuchukiao wanajipatia mateka. Umetutoa kama kondoo tuwe chakula, Na kututawanya kati ya mataifa. Wawauza watu wako bila kupata mali, Wala hukupata faida kwa thamani yao. Umetufanya kuwa lawama kwa jirani zetu, Mzaha na dhihaka kwao wanaotuzunguka. Umetufanya kuwa mithali kwa mataifa, Sababu ya kutikisa kichwa kwa watu wa nchi. Mchana kutwa fedheha yangu i mbele yangu, Na aibu imeufunika uso wangu, Kwa sauti ya mwenye kulaumu na kukufuru, Kwa sababu ya adui na mjilipiza kisasi. Haya yote yametupata, bali hatukukusahau, Wala hatukulivunja agano lako. Hatukuiacha mioyo yetu irudi nyuma, Wala hatua zetu hazikuiacha njia yako, Japo ulituponda katika pango la mbwamwitu, Na kutufunika kwa uvuli wa mauti. Ikiwa tumelisahau jina la Mungu wetu, Au kumnyoshea mungu mgeni mikono yetu; Je! Mungu hangegundua jambo hilo? Maana ndiye azijuaye siri za moyo. Hasha! Kwa ajili yako tunauawa mchana kutwa; Tunafanywa kama kondoo waendao kuchinjwa. Amka, Bwana, mbona umelala? Ondoka, usitutupe milele. Mbona unatuficha uso wako, Na kusahau kuonewa na kudhulumiwa kwetu? Maana nafsi yetu imeinama mavumbini, Tumbo letu limegandamana na nchi. Uinuke, uwe msaada wetu, Utukomboe kwa ajili ya fadhili zako.
Zaburi 44:1-26 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ee Mungu, tumesikia kwa masikio yetu Baba zetu wametuambia, Matendo uliyoyatenda siku zao, siku za kale. Wewe kwa mkono wako uliwafukuza mataifa, Ukawakalisha wao. Wewe uliwatesa watu wa nchi, Ukawaeneza wao. Maana si kwa upanga wao walivyoimiliki nchi, Wala si mkono wao uliowaokoa; Bali mkono wako wa kuume, naam, mkono wako, Na nuru ya uso wako, kwa kuwa uliwaridhia. Ee Mungu, Wewe ndiwe mfalme wangu, Uagize mambo ya wokovu kwa Yakobo. Kwa nguvu zako tutawaangusha watesi wetu; Kwa jina lako tutawakanyaga watupingao. Maana sitautumainia upinde wangu, Wala upanga wangu hautaniokoa. Bali Wewe ndiwe uliyetuokoa na watesi wetu; Na watuchukiao umewaaibisha. Tumejisifia Mungu mchana kutwa, Na jina lako tutalishukuru milele. Lakini umetutupa, umetufedhehesha, Wala hutoki na majeshi yetu. Waturudisha nyuma tukampa mtesi kisogo, Na watuchukiao wanajipatia mateka. Umetutoa kama kondoo tuwe chakula, Na kututawanya kati ya mataifa. Wawauza watu wako bila kupata mali, Wala hukupata faida kwa thamani yao. Umetufanya kuwa lawama kwa jirani zetu, Mzaha na dhihaka kwao wanaotuzunguka. Umetufanya kuwa mithali kwa mataifa, Sababu ya kutikisa kichwa kwa watu wa nchi. Mchana kutwa fedheha yangu i mbele yangu, Na haya ya uso wangu imenifunika, Kwa sauti ya mwenye kulaumu na kukufuru, Kwa sababu ya adui na mjilipiza kisasi. Haya yote yametupata, bali hatukukusahau, Wala hatukulihalifu agano lako. Hatukuiacha mioyo yetu irudi nyuma, Wala hatua zetu hazikuiacha njia yako. Hata utuponde katika kao la mbwa-mwitu, Na kutufunika kwa uvuli wa mauti. Ikiwa tumelisahau jina la Mungu wetu, Au kumnyoshea mungu mgeni mikono yetu; Je! Mungu hatalichunguza neno hilo? Maana ndiye azijuaye siri za moyo. Hasha! Kwa ajili yako tunauawa mchana kutwa; Tunafanywa kondoo waendao kuchinjwa. Amka, Bwana, mbona umelala? Ondoka, usitutupe kabisa. Mbona unatuficha uso wako, Na kusahau kuonewa na kudhulumiwa kwetu? Maana nafsi yetu imeinama mavumbini, Tumbo letu limegandamana na nchi. Uondoke, uwe msaada wetu, Utukomboe kwa ajili ya fadhili zako.
Zaburi 44:1-26 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Ee Mungu, tumesikia kwa masikio yetu, baba zetu wametueleza yale uliyotenda katika siku zao, siku za kale. Kwa mkono wako uliwafukuza mataifa na ukawapanda baba zetu, uliangamiza mataifa na kuwastawisha baba zetu. Sio kwa upanga wao waliipata nchi, wala si mkono wao uliwapatia ushindi; ilikuwa ni kitanga cha mkono wako wa kuume, na nuru ya uso wako, kwa kuwa uliwapenda. Wewe ni mfalme wangu na Mungu wangu, unayeamuru ushindi kwa Yakobo. Kwa uwezo wako tunawasukuma nyuma watesi wetu; kwa jina lako tunawakanyaga adui zetu. Siutumaini upinde wangu, upanga wangu hauniletei ushindi; bali wewe unatupatia ushindi juu ya adui zetu, unawaaibisha watesi wetu. Katika Mungu wetu tunajivuna mchana kutwa, nasi tutalisifu jina lako milele. Lakini sasa umetukataa na kutudhili, wala huendi tena na jeshi letu. Umetufanya tukimbie mbele ya adui, nao watesi wetu wametuteka nyara. Umetuacha tutafunwe kama kondoo na umetutawanya katika mataifa. Umewauza watu wako kwa fedha kidogo, wala hukupata faida yoyote kwa mauzo yao. Umetufanya lawama kwa majirani zetu, dharau na dhihaka kwa wale wanaotuzunguka. Umetufanya kuwa mithali miongoni mwa mataifa; mataifa hututikisia vichwa vyao. Fedheha yangu iko mbele yangu mchana kutwa, na uso wangu umejaa aibu tele, kwa ajili ya dhihaka ya wale wanaonilaumu na kunitukana, kwa sababu ya adui, ambaye anatamani kulipiza kisasi. Hayo yote yametutokea, ingawa tulikuwa hatujakusahau wala hatujaenda kinyume na agano lako. Mioyo yetu ilikuwa haijarudi nyuma; nyayo zetu zilikuwa hazijaiacha njia yako. Lakini ulituponda na kutufanya makao ya mbweha, na ukatufunika kwa giza nene. Kama tungekuwa tumelisahau jina la Mungu wetu au kunyooshea mikono yetu kwa mungu mgeni, je, si Mungu angegundua hili, kwa kuwa anazijua siri za moyo? Hata hivyo kwa ajili yako tunauawa mchana kutwa; tumehesabiwa kama kondoo wa kuchinjwa. Amka, Ee Bwana! Kwa nini unalala? Zinduka! Usitukatae milele. Kwa nini unauficha uso wako na kusahau taabu na mateso yetu? Tumeshushwa hadi mavumbini, miili yetu imegandamana na ardhi. Inuka na utusaidie, utukomboe kwa sababu ya upendo wako usio na mwisho.