Zaburi 40:1-17
Zaburi 40:1-17 Biblia Habari Njema (BHN)
Nilimngojea Mwenyezi-Mungu kwa uvumilivu, akanielekea na kukisikia kilio changu. Aliniondoa katika shimo la hatari, alinitoa katika matope ya dimbwi, akanisimamisha salama juu ya mwamba, na kuziimarisha hatua zangu. Alinifundisha wimbo mpya, wimbo wa sifa kwa Mungu wetu. Wengi wataona na kuogopa, na kumtumainia Mwenyezi-Mungu. Heri mtu anayemtumainia Mwenyezi-Mungu; mtu asiyejiunga na watu wenye majivuno, watu waliopotoka kwa kuabudu miungu ya uongo. Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu, umetufanyia mengi ya ajabu, na mipango yako juu yetu haihesabiki; hakuna yeyote aliye kama wewe. Kama ningeweza kusimulia hayo yote, idadi yake ingenishinda. Wewe hutaki tambiko wala sadaka, tambiko za kuteketeza wala za kuondoa dhambi; lakini umenipa masikio nikusikie. Ndipo niliposema: “Niko tayari; ninayotakiwa kufanya yameandikwa katika kitabu cha sheria; kutimiza matakwa yako, ee Mungu wangu ni furaha yangu, sheria yako naishika kwa moyo wangu wote!” Nimesimulia habari njema za ukombozi, mbele ya kusanyiko kubwa la watu. Kama ujuavyo ee Mwenyezi-Mungu, mimi sikujizuia kuitangaza. Sikuuficha moyoni mwangu ukombozi ulionijalia, nimetangaza daima kuwa wewe ni mwokozi mwaminifu; sikulificha kusanyiko kubwa la watu fadhili zako na uaminifu wako. Ee Mwenyezi-Mungu, usininyime huruma yako! Fadhili zako na uaminifu wako vinihifadhi daima. Maafa yasiyohesabika yanizunguka, maovu yangu yanikaba hata siwezi kuona; ni mengi kuliko nywele kichwani mwangu, nami nimevunjika moyo. Upende ee Mwenyezi-Mungu kuniokoa; ee Mwenyezi-Mungu, uje haraka kunisaidia. Wanaonuia kuniangamiza, na waaibike na kufedheheka! Hao wanaotamani niumie, na warudi nyuma na kuaibika! Hao wanaonisimanga, na wapumbazike kwa kushindwa kwao! Lakini wote wale wanaokutafuta wafurahi na kushangilia kwa sababu yako. Wapendao wokovu wako, waseme daima: “Mwenyezi-Mungu ni Mkuu!” Mimi ni maskini na fukara, ee Bwana; lakini ee Bwana wewe wanikumbuka. Ndiwe msaada wangu na mwokozi wangu; uje, ee Mungu wangu, usikawie!
Zaburi 40:1-17 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Nilimngoja BWANA kwa subira, Akaniinamia na kusikia kilio changu. Akanipandisha toka shimo la uharibifu, Toka udongo wa utelezi; Akaisimamisha miguu yangu mwambani, Akaziimarisha hatua zangu. Akatia wimbo mpya kinywani mwangu, Ndio sifa zake Mungu wetu. Wengi wataona na kuogopa, Nao watamtumainia BWANA. Heri aliyemfanya BWANA kuwa tumaini lake, Wala hakuwaelekea wenye kiburi, Wala hao wanaogeukia uongo. Ee BWANA, Mungu wangu, umefanya kwa wingi Miujiza yako na mawazo yako kwetu; Hakuna awezaye kufananishwa nawe; Kama ningependa kuyatangaza na kuyahubiri, Ni mengi sana hayahesabiki. Dhabihu na matoleo hukupendezwa nazo, Umetuzidishia ila masikio, Kafara na sadaka za dhambi hukuzitaka. Ndipo niliposema, Tazama nimekuja, (Katika gombo la kitabu nimeandikiwa,) Kuyafanya mapenzi yako, Ee Mungu wangu, ndiyo furaha yangu; Naam, sheria yako imo moyoni mwangu. Nimehubiri habari za haki katika kusanyiko kubwa. Sikuizuia midomo yangu; Ee BWANA, unajua. Sikusitiri haki yako moyoni mwangu; Nimetangaza uaminifu wako na wokovu wako. Sikuficha fadhili zako wala kweli yako Katika kusanyiko kubwa. Nawe, BWANA, usinizuilie rehema zako, Fadhili zako na kweli yako na zinihifadhi daima. Kwa maana mabaya yasiyohesabika Yamenizunguka mimi. Maovu yangu yamenipata, Wala siwezi kuona. Yamezidi kuliko nywele za kichwa changu, Nami nimevunjika moyo. Ee BWANA, uwe radhi kuniokoa, Ee BWANA, unisaidie hima. Waaibike na wafedheheke, Wote wanaotaka kuniua. Warudishwe nyuma, watahayarishwe, Wapendezwao na shari yangu. Wafadhaike kwa aibu yao, Wanaoniambia Ewe! Ewe! Washangilie na wakufurahie, Wote wakutafutao. Waupendao wokovu wako Waseme daima, BWANA ni Mkuu. Nami ni maskini na mhitaji, Bwana atanitunza. Ndiwe msaada wangu na mwokozi wangu, Ee Mungu wangu, usikawie.
Zaburi 40:1-17 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Nalimngoja BWANA kwa saburi, Akaniinamia akakisikia kilio changu. Akanipandisha toka shimo la uharibifu, Toka udongo wa utelezi; Akaisimamisha miguu yangu mwambani, Akaziimarisha hatua zangu. Akatia wimbo mpya kinywani mwangu, Ndio sifa zake Mungu wetu. Wengi wataona na kuogopa, Nao watamtumaini BWANA Heri aliyemfanya BWANA kuwa tumaini lake, Wala hakuwaelekea wenye kiburi, Wala hao wanaogeukia uongo. Ee BWANA, Mungu wangu, umefanya kwa wingi Miujiza yako na mawazo yako kwetu; Hakuna awezaye kufananishwa nawe; Kama ningependa kuyatangaza na kuyahubiri, Ni mengi sana hayahesabiki. Dhabihu na matoleo hukupendezwa nazo, Masikio yangu umeyazibua, Kafara na sadaka za dhambi hukuzitaka. Ndipo niliposema, Tazama nimekuja, (Katika gombo la chuo nimeandikiwa,) Kuyafanya mapenzi yako, Ee Mungu wangu, ndiyo furaha yangu; Naam, sheria yako imo moyoni mwangu. Nimehubiri habari za haki katika kusanyiko kubwa. Sikuizuia midomo yangu; Ee BWANA, unajua. Sikusitiri haki yako moyoni mwangu; Nimetangaza uaminifu wako na wokovu wako. Sikuficha fadhili zako wala kweli yako Katika kusanyiko kubwa. Nawe, BWANA, usinizuilie rehema zako, Fadhili zako na kweli yako na zinihifadhi daima. Kwa maana mabaya yasiyohesabika Yamenizunguka mimi. Maovu yangu yamenipata, Wala siwezi kuona. Yamezidi kuliko nywele za kichwa changu, Na moyo wangu umeniacha. Ee BWANA, uwe radhi kuniokoa, Ee BWANA, unisaidie hima. Waaibike, wafedheheke pamoja, Wanaoitafuta nafsi yangu waiangamize. Warudishwe nyuma, watahayarishwe, Wapendezwao na shari yangu. Wakae hali ya ukiwa, na iwe aibu yao, Wanaoniambia, Ewe! Ewe! Washangilie, wakufurahie, Wote wakutafutao. Waupendao wokovu wako Waseme daima, Atukuzwe BWANA. Nami ni maskini na mhitaji, Bwana atanitunza. Ndiwe msaada wangu na mwokozi wangu, Ee Mungu wangu, usikawie.
Zaburi 40:1-17 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Nilimngoja BWANA kwa saburi, naye akanijia na kusikia kilio changu. Akanipandisha kutoka shimo la uharibifu, kutoka matope na utelezi; akaiweka miguu yangu juu ya mwamba na kunipa mahali imara pa kusimama. Akaweka wimbo mpya kinywani mwangu, wimbo wa sifa kwa Mungu wetu. Wengi wataona na kuogopa na kuweka tumaini lao kwa BWANA. Heri mtu yule amfanyaye BWANA kuwa tumaini lake, asiyewategemea wenye kiburi, wale wenye kugeukia miungu ya uongo. Ee BWANA Mungu wangu, umefanya mambo mengi ya ajabu. Mambo uliyopanga kwa ajili yetu hakuna awezaye kukuhesabia; kama ningesema na kuyaelezea, yangekuwa mengi mno kuyatangaza. Dhabihu na sadaka hukuvitaka, lakini umefungua masikio yangu; sadaka za kuteketezwa na sadaka za dhambi hukuzihitaji. Ndipo niliposema, “Mimi hapa, nimekuja: imeandikwa kunihusu katika kitabu. Ee Mungu wangu, natamani kuyafanya mapenzi yako; sheria yako iko ndani ya moyo wangu.” Nimehubiri haki katika kusanyiko kubwa, sikufunga mdomo wangu, Ee BWANA, kama ujuavyo. Sikuficha haki yako moyoni mwangu; ninasema juu ya uaminifu wako na wokovu wako. Sikuficha upendo wako na kweli yako mbele ya kusanyiko kubwa. Ee BWANA, usinizuilie huruma zako, upendo wako na kweli yako daima vinilinde. Kwa maana taabu zisizohesabika zimenizunguka, dhambi zangu zimenikamata, hata nisiweze kuona. Zimekuwa nyingi kuliko nywele za kichwa changu, nao moyo unazimia ndani yangu. Ee BWANA, uwe radhi kuniokoa; Ee BWANA, njoo hima unisaidie. Wote wanaotafuta kuniua, waaibishwe na kufadhaishwa; wote wanaotamani kuangamizwa kwangu, wafukuzwe mbali kwa aibu. Wale wanaoniambia, “Aha! Aha!” wafadhaishwe na iwe aibu yao. Lakini wote wanaokutafuta washangilie na kukufurahia, wale wanaoupenda wokovu wako siku zote waseme, “BWANA atukuzwe!” Lakini mimi bado ni maskini na mhitaji; Bwana na anifikirie. Wewe ndiwe msaada wangu na Mwokozi wangu; Ee Mungu wangu, usikawie.