Zaburi 35:11-18
Zaburi 35:11-18 Biblia Habari Njema (BHN)
Mashahidi wakorofi wanajitokeza; wananiuliza mambo nisiyoyajua. Wananilipa mema yangu kwa mabaya; nami binafsi nimebaki katika ukiwa. Lakini wao walipokuwa wagonjwa, mimi nilivaa magunia kuonesha huzuni; nilijitesa kwa kujinyima chakula. Nilisali nikiwa nimeinamisha kichwa, kana kwamba namlilia rafiki au ndugu yangu. Nilikwenda huko na huko kwa huzuni, kama mtu anayeomboleza kifo cha mama yake. Lakini mimi nilipoanguka walikusanyika kunisimanga. Walikusanyika pamoja dhidi yangu. Watu nisiowajua walinirarua bila kukoma, wala hakuna aliyewazuia. Watu ambao huwadhihaki vilema, walinisagia meno yao kwa chuki. Ee Mwenyezi-Mungu, utatazama tu mpaka lini? Uniokoe kutoka kwenye mashambulio yao; uyaokoe maisha yangu na simba hao. Hapo nitakushukuru kati ya kusanyiko kubwa la watu; nitakutukuza kati ya jumuiya kubwa ya watu.
Zaburi 35:11-18 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Mashahidi wa udhalimu wanasimama, Wananiuliza mambo nisiyoyajua. Wananilipa mabaya badala ya mema, Hata nafsi yangu ikaingia ukiwa. Bali mimi, walipougua wao, Nguo yangu ilikuwa gunia. Nilijitesa nafsi yangu kwa kufunga; Maombi yangu yakarejea kifuani mwangu. Nilisikitika kana kwamba ni rafiki au ndugu yangu, Niliinama nikilia kama aliyefiwa na mamaye. Lakini nikijikwaa wanafurahi na kukusanyana, Walinikusanyikia watu ovyo nisiowajua, Wakanipapura bila kukoma. Bila heshima walinidhihaki kupindukia, Wakanisagia meno yao. BWANA, utatazama hadi lini? Uiokoe nafsi yangu kutoka kwa maangamizi yao, Na maisha yangu kutoka kwa wanasimba. Nitakushukuru katika kusanyiko kubwa; Nitakusifu kati ya watu wengi.
Zaburi 35:11-18 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Mashahidi wa udhalimu wanasimama, Wananiuliza mambo nisiyoyajua. Wananilipa mabaya badala ya mema, Hata nafsi yangu ikaingia ukiwa. Bali mimi, walipougua wao, Nguo yangu ilikuwa gunia. Nalijitesa nafsi yangu kwa kufunga; Maombi yangu yakarejea kifuani mwangu. Nalijifanya kama kwamba ni rafiki au ndugu yangu, Naliinama nikilia kama aliyefiwa na mamaye. Lakini nikijikwaa hufurahi na kukusanyana, Walinikusanyikia watu ovyo nisiowajua, Wananipapura wala hawakomi. Kama wenye mzaha wakikufuru karamuni Wananisagia meno. BWANA, hata lini utatazama? Uiokoe nafsi yangu na maharabu yao, Na mpenzi wangu na wana-simba. Nitakushukuru katika kusanyiko kubwa; Nitakusifu kati ya watu wengi.
Zaburi 35:11-18 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Mashahidi wakatili wanainuka, wananiuliza mambo nisiyoyajua. Wananilipa baya kwa jema na kuiacha nafsi yangu ukiwa. Lakini walipokuwa wagonjwa, nilivaa gunia na nikajinyenyekeza kwa kufunga. Maombi yangu yaliponirudia bila kujibiwa, niliendelea kuomboleza kama vile wao ni rafiki au ndugu. Niliinamisha kichwa chini kwa huzuni kama ninayemwombolezea mama yangu. Lakini nilipojikwaa, walikusanyika kwa shangwe; washambuliaji walijikusanya dhidi yangu bila mimi kujua. Walinisingizia pasipo kukoma. Kama watu wasiomcha Mungu, wamenidhihaki, wamenisagia meno. Ee Bwana, utatazama hadi lini? Niokoe maisha yangu na maangamizi yao, okoa uhai wangu wa thamani kutokana na simba hawa. Nami nitakushukuru mbele ya kusanyiko kubwa, nitakusifu katikati ya watu wengi.