Zaburi 27:7-14
Zaburi 27:7-14 Biblia Habari Njema (BHN)
Usikie, ee Mwenyezi-Mungu, ninapokulilia, unionee huruma na kunijibu. Moyo wangu waniambia: “Njoo umtafute Mungu!” Basi, naja kwako, ee Mwenyezi-Mungu. Usiache kuniangalia kwa wema. Usinikatae kwa hasira mimi mtumishi wako; wewe umekuwa daima msaada wangu. Usinitupe wala usiniache, ee Mungu Mwokozi wangu. Hata kama wazazi wangu wakinitupa, Mwenyezi-Mungu atanipokea kwake. Unifundishe njia yako, ee Mwenyezi-Mungu; uniongoze katika njia iliyo sawa, kwa sababu ya maadui zangu. Usiniache maadui wanitende wapendavyo; maana mashahidi wa uongo wananikabili, nao wanatoa vitisho vya ukatili. Naamini nitauona wema wake Mwenyezi-Mungu katika makao ya walio hai. Mtegemee Mwenyezi-Mungu! Uwe na moyo, usikate tamaa! Naam, mtegemee Mwenyezi-Mungu!
Zaburi 27:7-14 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ee BWANA, usikie, kwa sauti yangu ninalia, Unifadhili, unijibu. Uliposema, “Nitafuteni uso wangu,” Moyo wangu umekuambia, BWANA, uso wako nitautafuta. Usinifiche uso wako, Usimkatalie mtumishi wako kwa hasira. Umekuwa msaada wangu, usinitupe, Wala usiniache, Ee Mungu wa wokovu wangu. Hata baba yangu na mama yangu wakiniacha, Bali BWANA atanikaribisha kwake. Ee BWANA, unifundishe njia yako, Na kuniongoza katika njia iliyonyoka; Kwa sababu yao wanaoniotea; Usinitie katika nia ya watesi wangu; Maana mashahidi wa uongo wamenijia, Nao watoao jeuri kama pumzi. Naamini ya kuwa nitauona wema wa BWANA Katika nchi ya walio hai. Umtumainie BWANA, uwe imara, Upige moyo konde, naam, umngoje BWANA.
Zaburi 27:7-14 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ee BWANA, usikie, kwa sauti yangu ninalia, Unifadhili, unijibu. Uliposema, Nitafuteni uso wangu, Moyo wangu umekuambia, BWANA, uso wako nitautafuta. Usinifiche uso wako, Usijiepushe na mtumishi wako kwa hasira. Umekuwa msaada wangu, usinitupe, Wala usiniache, Ee Mungu wa wokovu wangu. Baba yangu na mama yangu wameniacha, Bali BWANA atanikaribisha kwake. Ee BWANA, unifundishe njia yako, Na kuniongoza katika njia iliyonyoka; Kwa sababu yao wanaoniotea; Usinitie katika nia ya watesi wangu; Maana mashahidi wa uongo wameniondokea, Nao watoao jeuri kama pumzi. Naamini ya kuwa nitauona wema wa BWANA Katika nchi ya walio hai. Umngoje BWANA, uwe hodari, Upige moyo konde, naam, umngoje BWANA.
Zaburi 27:7-14 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Isikie sauti yangu nikuitapo, Ee BWANA, unihurumie na unijibu. Moyo wangu unasema kuhusu wewe, “Utafute uso wake!” Uso wako, BWANA “Nitautafuta.” Usinifiche uso wako, usimkatae mtumishi wako kwa hasira; wewe umekuwa msaada wangu. Usinikatae wala usiniache, Ee Mungu Mwokozi wangu. Hata baba yangu na mama yangu wakiniacha, BWANA atanipokea. Nifundishe njia yako, Ee BWANA, niongoze katika njia iliyo nyoofu, kwa sababu ya watesi wangu. Usiniachilie kwa nia za adui zangu, kwa maana mashahidi wa uongo wameinuka dhidi yangu, wakipumua ujeuri. Nami bado nina tumaini hili: nitauona wema wa BWANA katika nchi ya walio hai. Mngojee BWANA; uwe hodari na mwenye moyo mkuu, na umngojee BWANA.