Zaburi 2:1-12
Zaburi 2:1-12 Biblia Habari Njema (BHN)
Kwa nini mataifa yanafanya ghasia? Mbona watu wanafanya njama za bure? Wafalme wa dunia wanajitayarisha; watawala wanashauriana pamoja, dhidi ya Mwenyezi-Mungu na mteule wake. Wanasema: “Tujiondoe katika utawala wao; tutupilie mbali minyororo yao!” Mwenyezi-Mungu atawalaye juu mbinguni, anawacheka na kuwadhihaki. Kisha, anawakaripia kwa ghadhabu, na kuwatisha kwa hasira, akisema: “Nimemtawaza mfalme niliyemteua, anatawala Siyoni, mlima wangu mtakatifu!” Mfalme asema: “Nitatangaza azimio la Mwenyezi-Mungu. Mungu aliniambia: ‘Wewe ni mwanangu, mimi leo nimekuwa baba yako. Niombe nami nitakupa mataifa yawe urithi wako, na dunia nzima kuwa mali yako. Utawaponda kwa fimbo ya chuma; utawavunja kama chungu cha mfinyanzi!’” Sasa enyi wafalme, tumieni busara; sikilizeni onyo hili, enyi watawala wa dunia. Mtumikieni Mwenyezi-Mungu kwa uchaji; msujudieni na kutetemeka; asije akakasirika, mkaangamia ghafla; kwani hasira yake huwaka haraka. Heri yao wote wanaokimbilia usalama kwake!
Zaburi 2:1-12 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Mbona mataifa yanafanya ghasia, Na watu kuwaza mambo ya bure? Wafalme wa dunia wanajipanga, Na wakuu wanafanya shauri pamoja, Juu ya BWANA, Na juu ya masihi wake, Na tuvipasue vifungo vyao, Na kuzitupa mbali nasi kamba zao. Yeye aketiye mbinguni anacheka, Bwana anawafanyia dhihaka. Ndipo atakaposema nao kwa hasira yake, Na kuwafadhaisha kwa ghadhabu yake, akisema: Nami nimemweka mfalme wangu Juu ya Sayuni, mlima wangu mtakatifu. Nitaihubiri amri; BWANA aliniambia, Wewe ni mwanangu, Mimi leo nimekuzaa. Uniombe, nami nitakupa mataifa kuwa urithi wako, Na miisho ya dunia kuwa milki yako. Utawaponda kwa fimbo ya chuma, Na kuwavunja kama chombo cha mfinyanzi. Na sasa, enyi wafalme, iweni na hekima, Enyi watawala wa dunia, mwaonywa. Mtumikieni BWANA kwa kicho, Shangilieni kwa kutetemeka. Shikeni yaliyo bora, asije akafanya hasira Nanyi mkapotea njiani, Kwa kuwa hasira yake huwaka upesi; Heri wote wanaomkimbilia.
Zaburi 2:1-12 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Mbona mataifa wanafanya ghasia, Na makabila wanatafakari ubatili? Wafalme wa dunia wanajipanga, Na wakuu wanafanya shauri pamoja, Juu ya BWANA, Na juu ya masihi wake, Na tuvipasue vifungo vyao, Na kuzitupia mbali nasi kamba zao. Yeye aketiye mbinguni anacheka, Bwana anawafanyia dhihaka. Ndipo atakaposema nao kwa hasira yake, Na kuwafadhaisha kwa ghadhabu yake. Nami nimemweka mfalme wangu Juu ya Sayuni, mlima wangu mtakatifu. Nitaihubiri amri; BWANA aliniambia, Ndiwe mwanangu, Mimi leo nimekuzaa. Uniombe, nami nitakupa mataifa kuwa urithi wako, Na miisho ya dunia kuwa milki yako. Utawaponda kwa fimbo ya chuma, Na kuwavunja kama chombo cha mfinyanzi. Na sasa, enyi wafalme, fanyeni akili, Enyi waamuzi wa dunia, mwadibiwe. Mtumikieni BWANA kwa kicho, Shangilieni kwa kutetemeka. Shikeni yaliyo bora, asije akafanya hasira Nanyi mkapotea njiani, Kwa kuwa hasira yake itawaka upesi; Heri wote wanaomkimbilia.
Zaburi 2:1-12 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Kwa nini mataifa wanashauriana kufanya mabaya, na makabila ya watu kula njama bure? Wafalme wa dunia wanajipanga na watawala wanajikusanya dhidi ya BWANA na dhidi ya Mpakwa Mafuta wake. Wanasema, “Tuvunje minyororo yao na kuvitupilia mbali vifungo vyao.” Yeye anayetawala mbinguni hucheka, Bwana huwadharau. Kisha huwakemea katika hasira yake na kuwaogopesha katika ghadhabu yake, akisema, “Nimemtawaza Mfalme wangu juu ya Sayuni, mlima wangu mtakatifu.” Nitatangaza amri ya BWANA: Yeye aliniambia, “Wewe ni Mwanangu; leo mimi nimekuwa Baba yako. Niombe, nami nitayafanya mataifa kuwa urithi wako, na miisho ya dunia kuwa milki yako. Utawapondaponda kwa fimbo ya chuma, na kuwavunjavunja kama chombo cha mfinyanzi.” Kwa hiyo, ninyi wafalme, kuweni na hekima; mwonyeke, enyi watawala wa dunia. Mtumikieni BWANA kwa hofu na mshangilie kwa kutetemeka. Mbusu Mwana, asije akakasirika nawe ukaangamizwa katika njia yako, kwa maana hasira yake inaweza kuwaka ghafula. Heri wote wanaomkimbilia.