Zaburi 17:1-7
Zaburi 17:1-7 Biblia Habari Njema (BHN)
Ee Mwenyezi-Mungu usikie kisa changu cha haki, usikilize kilio changu, uitegee sikio sala yangu isiyo na hila. Haki yangu na ije kutoka kwako, kwani wewe wajua jambo lililo la haki. Wewe wajua kabisa moyo wangu; umenijia usiku, kunichunguza, umenitia katika jaribio; hukuona uovu ndani yangu, sikutamka kitu kisichofaa. Kuhusu matendo watendayo watu; mimi nimeitii amri yako, nimeepa njia ya wadhalimu. Nimefuata daima njia yako; wala sijateleza kamwe. Nakuita, ee Mungu, kwani wewe wanijibu; unitegee sikio, uyasikie maneno yangu. Onesha fadhili zako za ajabu, uwaokoe kutoka kwa adui zao, wale wanaokimbilia usalama kwako.
Zaburi 17:1-7 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ee BWANA, usikie haki, ukisikilize kilio changu, Utege sikio lako kwa maombi yangu, Yasiyotoka katika midomo ya hila. Hukumu yangu na itoke kwako, Macho yako na yatazame mambo ya adili. Umenijaribu moyo wangu, umenijia usiku, Umenichunguza usione neno; Nimenuia kinywa changu kisikose, Kuhusu matendo ya wanadamu; Kwa neno la midomo yako Nimejiepusha na njia za wenye jeuri. Nyayo zangu zimeshikamana na njia zako, Hatua zangu hazikuondoshwa. Ee Mungu, nimekuita kwa maana utaitika, Utege sikio lako ulisikie neno langu. Dhihirisha fadhili zako za ajabu Wewe uwaokoaye wanaokukimbilia; Kwa mkono wako wa kulia Uwaokoe kutoka kwa adui zao.
Zaburi 17:1-7 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ee BWANA, usikie haki, ukisikilize kilio changu, Utege sikio lako kwa maombi yangu, Yasiyotoka katika midomo ya hila. Hukumu yangu na itoke kwako, Macho yako na yatazame mambo ya adili. Umenijaribu moyo wangu, umenijilia usiku, Umenihakikisha usione neno; Nimenuia kinywa changu kisikose, Mintarafu matendo ya wanadamu; Kwa neno la midomo yako Nimejiepusha na njia za wenye jeuri. Nyayo zangu zimeshikamana na njia zako, Hatua zangu hazikuondoshwa. Ee Mungu, nimekuita kwa maana utaitika, Utege sikio lako ulisikie neno langu. Dhihirisha fadhili zako za ajabu Wewe uwaokoaye wanaokukimbilia; Kwa mkono wako wa kuume Uwaokoe nao wanaowaondokea.
Zaburi 17:1-7 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Sikia, Ee BWANA, kusihi kwangu kwa haki, sikiliza kilio changu. Tega sikio kwa ombi langu, halitoki katika midomo ya udanganyifu. Hukumu yangu na itoke kwako, macho yako na yaone yale yaliyo haki. Ingawa unauchunguza moyo wangu na kunikagua usiku, ingawa umenijaribu, hutaona chochote. Nimeamua kwamba kinywa changu hakitatenda dhambi. Kuhusu matendo ya wanadamu: kwa neno la midomo yako, nimejiepusha na njia za wenye jeuri. Hatua zangu zimeshikamana na njia zako; nyayo zangu hazikuteleza. Ee Mungu, ninakuita, kwa kuwa utanijibu, nitegee sikio lako na usikie ombi langu. Uoneshe ajabu ya upendo wako mkuu, wewe unayeokoa kwa mkono wako wa kuume wale wanaokukimbilia kutokana na adui zao.