Zaburi 145:8-14
Zaburi 145:8-14 Biblia Habari Njema (BHN)
Mwenyezi-Mungu ni mwenye huruma na rehema; hakasiriki ovyo, amejaa fadhili. Mwenyezi-Mungu ni mwema kwa wote, ni mwenye huruma kwa viumbe vyake vyote. Viumbe vyako vyote vitakushukuru, ee Mwenyezi-Mungu, nao waaminifu wako watakutukuza. Watasema juu ya utukufu wa ufalme wako, na kutangaza juu ya nguvu yako kuu, ili kila mtu ajue matendo yako makuu, na fahari tukufu ya ufalme wako. Ufalme wako ni ufalme wa milele; mamlaka yako yadumu vizazi vyote. Mwenyezi-Mungu ni mwaminifu katika ahadi zake zote, ni mwema katika matendo yake yote. Mwenyezi-Mungu huwategemeza wote wanaoanguka; huwainua wote waliokandamizwa.
Zaburi 145:8-14 Swahili Revised Union Version (SRUV)
BWANA ni mwenye fadhili na huruma, Si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa rehema, BWANA ni mwema kwa watu wote, Na rehema zake ziko juu ya vyote alivyoumba. Ee BWANA, kazi zako zote zitakushukuru, Na wacha Mungu wako watakuhimidi. Wataunena utukufu wa ufalme wako, Na kusena uweza wako. Ili kuwajulisha watu matendo yake makuu, Na utukufu wa fahari ya ufalme wake. Ufalme wako ni ufalme wa milele, BWANA ni mwaminifu katika maneno yake yote, Na mwenye fadhili katika matendo yake yote Na mamlaka yako ni ya vizazi vyote. BWANA huwategemeza wote waangukao, Huwainua wote walioinama chini.
Zaburi 145:8-14 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
BWANA ana fadhili, ni mwingi wa huruma, Si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa rehema, BWANA ni mwema kwa watu wote, Na rehema zake zi juu ya kazi zake zote. Ee BWANA, kazi zako zote zitakushukuru, Na wacha Mungu wako watakuhimidi. Wataunena utukufu wa ufalme wako, Na kuuhadithia uweza wako. Ili kuwajulisha watu matendo yake makuu, Na utukufu wa fahari ya ufalme wake. Ufalme wako ni ufalme wa zamani zote, Na mamlaka yako ni ya vizazi vyote. BWANA huwategemeza wote waangukao, Huwainua wote walioinama chini.
Zaburi 145:8-14 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
BWANA ni mwenye neema na mwingi wa huruma, si mwepesi wa hasira, bali ni mwingi wa upendo. BWANA ni mwema kwa wote, ana huruma kwa vyote alivyovifanya. Ee BWANA, vyote ulivyovifanya vitakusifu, watakatifu wako watakutukuza. Watasimulia utukufu wa ufalme wako na kusema kuhusu ukuu wako, ili watu wote wajue matendo yako makuu na utukufu wa fahari ya ufalme wako. Ufalme wako ni ufalme wa milele, mamlaka yako hudumu vizazi vyote. BWANA ni mwaminifu kwa ahadi zake zote na mwenye upendo kwa vyote alivyovifanya. BWANA huwategemeza wote waangukao, na huwainua wote waliolemewa na mizigo yao.