Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Zaburi 132:1-18

Zaburi 132:1-18 Biblia Habari Njema (BHN)

Ee Mwenyezi-Mungu, mkumbuke Daudi, kumbuka taabu zote alizopata. Ukumbuke ahadi aliyokupa, ee Mwenyezi-Mungu, kiapo alichokuapia, ewe Mwenye Nguvu wa Yakobo: “Sitaingia ndani ya nyumba yangu, wala kulala kitandani mwangu; sitakubali kulala usingizi, wala kusinzia; mpaka nikupatie wewe Mwenyezi-Mungu mahali pa kukaa, makao yako, ewe Mwenye Nguvu wa Yakobo!” Huko Efratha tulisikia habari za sanduku la agano, tukalikuta katika mashamba ya Yearimu. “Haya! Twende nyumbani kwa Mungu, tuabudu mbele ya kiti chake cha enzi!” Inuka ee Mwenyezi-Mungu, nenda kwenye maskani yako; inuka pamoja na sanduku la agano la uwezo wako! Makuhani wako wawe waadilifu daima; na waaminifu wako wapige vigelegele vya furaha! Kwa ajili ya Daudi, mtumishi wako, usimkatae huyo mfalme uliyemweka wakfu. Mwenyezi-Mungu alimwapia Daudi kiapo thabiti, kiapo ambacho hatakibatilisha: “Nitamtawaza mmoja wa wazawa wako mwenyewe, kuwa mfalme baada yako. Watoto wako wakishika agano langu, na kuzingatia mafundisho nitakayowapa, watoto wao pia watakuwa wafalme kama wewe.” Mwenyezi-Mungu ameuchagua mji wa Siyoni, ametaka uwe makao yake: “Hapa ndipo nitakapokaa milele, ndipo maskani yangu maana nimepachagua. Nitaubariki sana mji wa Siyoni kwa mahitaji yake; nitawashibisha chakula maskini wake. Nitawafanikisha makuhani wake kwa wokovu; waaminifu wake watapiga vigelegele vya furaha. Humo nitamchipusha mfalme shujaa wa ukoo wa Daudi: Kama taa iwakayo nitamtegemeza mfalme niliyemteua. Maadui zake nitawavika aibu; lakini yeye nitamvika fahari ya kifalme.”

Shirikisha
Soma Zaburi 132

Zaburi 132:1-18 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

Ee BWANA, mkumbuke Daudi na taabu zote alizozistahimili. Aliapa kiapo kwa BWANA na akaweka nadhiri kwa Yule Mwenye Nguvu wa Yakobo: “Sitaingia nyumbani mwangu au kwenda kitandani mwangu: sitaruhusu usingizi katika macho yangu, wala kope zangu kusinzia, hadi nitakapompatia BWANA mahali, makao kwa ajili ya Yule Mwenye Nguvu wa Yakobo.” Tulisikia habari hii huko Efrata, tulikutana nayo katika mashamba ya Yaara: “Twendeni kwenye makao yake, na tuabudu kwenye kiti cha kuwekea miguu yake; inuka, Ee BWANA, uje mahali pako pa kupumzikia, wewe na Sanduku la nguvu zako. Makuhani wako na wavikwe haki, watakatifu wako na waimbe kwa furaha.” Kwa ajili ya Daudi mtumishi wako, usimkatae mpakwa mafuta wako. BWANA alimwapia Daudi kiapo, kiapo cha uhakika ambacho hatakitangua: “Nitamweka mmoja wa wazao wako mwenyewe kwenye kiti chako cha ufalme, kama wanao watashika agano langu na sheria ninazowafundisha, ndipo wana wao watakalia kiti chako cha ufalme milele na milele.” Kwa maana BWANA ameichagua Sayuni, amepaonea shauku pawe maskani yake: “Hapa ni mahali pangu pa kupumzika milele na milele; hapa ndipo nitakapoketi nikitawala, kwa sababu nimepaonea shauku: Nitambariki kwa kumpa mahitaji tele: nitashibisha maskini wake kwa chakula. Nitawavika makuhani wake wokovu, nao watakatifu wake watadumu wakiimba kwa furaha. “Hapa nitamchipushia Daudi pembe, na kuweka taa kwa ajili ya masiya wangu. Adui zake nitawavika aibu, bali taji kichwani pake litangʼaa sana.”

Shirikisha
Soma Zaburi 132