Zaburi 116:1-19
Zaburi 116:1-19 Biblia Habari Njema (BHN)
Nampenda Mwenyezi-Mungu, kwa maana anisikia, maana amesikia kilio cha ombi langu. Yeye amenitegea sikio, hivyo nitamwomba muda wote niishio. Hatari ya kifo ilinizunguka, vitisho vya kaburi vilinivamia; nilijawa na mahangaiko na majonzi. Kisha nikamlilia Mwenyezi-Mungu: “Ee Mwenyezi-Mungu, tafadhali unisalimishe!” Mwenyezi-Mungu amejaa wema na uaminifu; Mungu wetu ni mwenye huruma. Mwenyezi-Mungu huwalinda wanyofu; nilipokuwa nimekandamizwa aliniokoa. Uwe na utulivu mkuu, ee nafsi yangu, maana Mwenyezi-Mungu amenitendea mema. Ameniokoa kifoni na kufuta machozi yangu; akanilinda nisije nikaanguka. Nitatembea mbele yake Mwenyezi-Mungu, katika nchi ya watu walio hai. Nilikuwa na imani hata niliposema: “Mimi nimetaabika mno.” Hata nilisema kwa hofu yangu: “Binadamu wote hawaaminiki!” Nimrudishie nini Mwenyezi-Mungu, kwa ukarimu wote alionitendea? Nitamtolea tambiko ya divai kwa kunikomboa, nitaomba kwa jina lake Mwenyezi-Mungu. Nitamtimizia Mwenyezi-Mungu nadhiri zangu, mbele ya watu wake wote. Kifo cha waaminifu wake Mwenyezi-Mungu si jambo dogo mbele yake. Ee Mwenyezi-Mungu, mimi ni mtumishi wako; ni mtumishi wako, mtoto wa mjakazi wako; umenifungulia vifungo vyangu. Nitakutolea tambiko za shukrani, na kukupa heshima zangu. Nitakutimizia ahadi zangu, ee Mwenyezi-Mungu mbele ya watu wako wote, waliokusanyika hekaluni mwako, katikati ya Yerusalemu. Msifuni Mwenyezi-Mungu!
Zaburi 116:1-19 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Haleluya. Nampenda BWANA kwa kuwa anaisikiliza Sauti yangu na dua zangu. Kwa maana amenitegea sikio lake, Kwa hiyo nitamwita siku zangu zote. Kamba za mauti zilinizunguka, Shida za kuzimu zilinipata. Nilipata dhiki na mateso; Nikaliitia jina la BWANA. Ee BWANA, nakuomba sana, Uniokoe nafsi yangu. BWANA ni mwenye neema na haki, Naam, Mungu wetu ni mwenye rehema. BWANA huwalinda wasio na hila; Nilidhilika, akaniokoa. Ee nafsi yangu, urudi pumzikoni mwako, Kwa kuwa BWANA amekutendea ukarimu. Maana umeniponya nafsi yangu na mauti, Macho yangu na machozi, Na miguu yangu na kuanguka. Nitaenenda mbele za BWANA Katika nchi za walio hai. Nilidumisha imani yangu, hata niliposema, Mimi nateseka sana. Nikiwa katika hangaiko langu nikasema, Wanadamu wote ni waongo. Nimrudishie BWANA nini Kwa ukarimu wake wote alionitendea? Nitakipokea kikombe cha wokovu; Na kulitangaza jina la BWANA; Nitaziondoa nadhiri zangu kwa BWANA, Naam, mbele ya watu wake wote. Kifo cha waaminifu wa Mungu, kina thamani machoni pa BWANA. Ee BWANA, hakika mimi ni mtumishi wako, Mtumishi wako, mwana wa mjakazi wako, Umevifungua vifungo vyangu. Nitakutolea dhabihu ya kushukuru; Na kulitangaza jina la BWANA; Nitaziondoa nadhiri zangu kwa BWANA, Naam, mbele ya watu wake wote. Katika nyua za nyumba ya BWANA, Ndani yako, Ee Yerusalemu.
Zaburi 116:1-19 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Haleluya. Nampenda BWANA kwa kuwa anaisikiliza Sauti yangu na dua zangu. Kwa maana amenitegea sikio lake, Kwa hiyo nitamwita siku zangu zote. Kamba za mauti zilinizunguka, Shida za kuzimu zilinipata. Naliona taabu na huzuni; Nikaliitia jina la BWANA. Ee BWANA, nakuomba sana, Uniokoe nafsi yangu. BWANA ni mwenye neema na haki, Naam, Mungu wetu ni mwenye rehema. BWANA huwalinda wasio na hila; Nalidhilika, akaniokoa. Ee nafsi yangu, urudi rahani mwako, Kwa kuwa BWANA amekutendea ukarimu. Maana umeniponya nafsi yangu na mauti, Macho yangu na machozi, Na miguu yangu na kuanguka. Nitaenenda mbele za BWANA Katika nchi za walio hai. Naliamini, kwa maana nitasema, Mimi naliteswa sana. Mimi nalisema kwa haraka yangu, Wanadamu wote ni waongo. Nimrudishie BWANA nini Kwa ukarimu wake wote alionitendea? Nitakipokea kikombe cha wokovu; Na kulitangaza jina la BWANA; Nitaziondoa nadhiri zangu kwa BWANA, Naam, mbele ya watu wake wote. Ina thamani machoni pa BWANA Mauti ya wacha Mungu wake. Ee BWANA, hakika mimi ni mtumishi wako, Mtumishi wako, mwana wa mjakazi wako, Umevifungua vifungo vyangu. Nitakutolea dhabihu ya kushukuru; Na kulitangaza jina la BWANA; Nitaziondoa nadhiri zangu kwa BWANA, Naam, mbele ya watu wake wote. Katika nyua za nyumba ya BWANA, Ndani yako, Ee Yerusalemu.
Zaburi 116:1-19 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Nampenda BWANA kwa maana amesikia sauti yangu; amesikia kilio changu ili anihurumie. Kwa sababu amenitegea sikio lake, nitamwita siku zote za maisha yangu. Kamba za mauti zilinizunguka, vitisho vya Kuzimu vilinipata, nikalemewa na taabu na huzuni. Ndipo nikaliitia jina la BWANA: “Ee BWANA, niokoe!” BWANA ni mwenye neema na haki, Mungu wetu ni mwingi wa huruma. BWANA huwalinda wanyenyekevu, nilipokuwa katika shida kubwa, aliniokoa. Ee nafsi yangu, tulia tena, kwa kuwa BWANA amekuwa mwema kwako. Kwa kuwa wewe, Ee BWANA, umeniokoa nafsi yangu na mauti, macho yangu kutokana na machozi, miguu yangu kutokana na kujikwaa, ili niweze kutembea mbele za BWANA, katika nchi ya walio hai. Nilimwamini BWANA, niliposema, “Mimi nimeteseka sana.” Katika taabu yangu nilisema, “Wanadamu wote ni waongo.” Nimrudishie BWANA nini kwa wema wake wote alionitendea? Nitakiinua kikombe cha wokovu na kulitangaza jina la BWANA. Nitazitimiza nadhiri zangu kwa BWANA mbele za watu wake wote. Kifo cha watakatifu kina thamani machoni pa BWANA. Ee BWANA, hakika mimi ni mtumishi wako, mimi ni mtumishi wako, mwana wa mjakazi wako; umeniweka huru toka katika minyororo yangu. Nitakutolea dhabihu ya kukushukuru na kuliita jina la BWANA. Nitazitimiza nadhiri zangu kwa BWANA mbele za watu wake wote, katika nyua za nyumba ya BWANA, katikati yako, ee Yerusalemu.