Zaburi 107:23-32
Zaburi 107:23-32 Biblia Habari Njema (BHN)
Baadhi walisafiri baharini kwa meli, na kufanya shughuli zao humo baharini. Waliyaona matendo ya Mwenyezi-Mungu, mambo ya ajabu aliyotenda huko. Aliamuru, akazusha dhoruba kali, ikarusha juu mawimbi ya bahari. Walitupwa juu angani, kisha chini vilindini; uhodari wao ukawaishia katika mkasa huo. Waliyumbayumba na kupepesuka kama walevi; maarifa yao ya uanamaji yakawaishia. Ndipo katika taabu zao wakamlilia Mwenyezi-Mungu, naye akawaokoa katika mateso zao. Aliifanya ile dhoruba kali itulie, nayo mawimbi yakanyamaza. Hapo wakafurahi kwa kupata utulivu; akawafikisha kwenye bandari waliyoiendea. Mshukuruni Mwenyezi-Mungu kwa fadhili zake; kwa sababu ya maajabu aliyowatendea binadamu. Mtukuzeni katika kusanyiko la watu, na kumsifu katika baraza la wazee.
Zaburi 107:23-32 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Washukao baharini katika merikebu, Wafanyao kazi yao katika maji mengi, Hao huziona kazi za BWANA, Na maajabu yake vilindini. Maana alisema, akavumisha upepo wa dhoruba, Ukayainua juu mawimbi ya bahari. Walirushwa juu mbinguni, waliteremka hadi vilindini, Uhodari wao ukayeyuka katika maafa yao. Waliyumbayumba, walipepesuka kama mlevi, Ujuzi wao wote uliwaishia. Wakamlilia BWANA katika dhiki zao, Akawaponya kutoka kwa shida zao. Huituliza dhoruba, ikawa shwari, Mawimbi yake yakanyamaza. Ndipo walipofurahi kwa kuwa yametulia Naye akawaleta mpaka bandani waliyoitamani. Na wamshukuru BWANA kwa fadhili zake, Na maajabu yake kwa wanadamu. Na wamtukuze katika kusanyiko la watu, Na wamhimidi katika baraza la wazee.
Zaburi 107:23-32 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Washukao baharini katika merikebu, Wafanyao kazi yao katika maji mengi, Hao huziona kazi za BWANA, Na maajabu yake vilindini. Maana husema, akavumisha upepo wa dhoruba, Ukayainua juu mawimbi yake. Wapanda mbinguni, watelemka vilindini, Nafsi yao yayeyuka kwa hali mbaya. Wayumba-yumba, wapepesuka kama mlevi, Akili zao zote zawapotea. Wakamlilia BWANA katika dhiki zao, Akawaponya na shida zao. Huituliza dhoruba, ikawa shwari, Mawimbi yake yakanyamaza. Ndipo walipofurahi kwa kuwa yametulia Naye huwaleta mpaka bandari waliyoitamani. Na wamshukuru BWANA kwa fadhili zake, Na maajabu yake kwa wanadamu. Na wamtukuze katika kusanyiko la watu, Na wamhimidi katika baraza ya wazee.
Zaburi 107:23-32 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Wengine walisafiri baharini kwa meli, walikuwa wafanyabiashara kwenye maji makuu. Waliziona kazi za BWANA, matendo yake ya ajabu kilindini. Kwa maana alisema na kuamsha tufani iliyoinua mawimbi juu. Yakainuka juu mbinguni, yakashuka chini hadi vilindini; katika hatari hii ujasiri wao uliyeyuka. Walipepesuka na kuyumbayumba kama walevi, ujanja wao ukafikia ukomo. Ndipo walipomlilia BWANA katika shida yao, naye akawatoa kwenye taabu yao. Akatuliza dhoruba kwa mnongʼono, mawimbi ya bahari yakatulia. Walifurahi ilipokuwa shwari, naye akawaongoza hadi bandari waliyoitamani. Basi na wamshukuru BWANA kwa upendo wake usiokoma, na kwa matendo yake ya ajabu kwa wanadamu. Na wamtukuze yeye katika kusanyiko la watu, na wamsifu katika baraza la wazee.