Zaburi 107:10-16
Zaburi 107:10-16 Biblia Habari Njema (BHN)
Baadhi waliishi katika giza na ukiwa, wafungwa katika mateso na minyororo, kwa sababu waliasi maagizo ya Mungu, na kuyapuuza mashauri yake Mungu Mkuu. Walikuwa hoi kwa kazi ngumu, wakaanguka chini, pasiwe na wa kuwasaidia. Ndipo katika taabu yao wakamlilia Mwenyezi-Mungu, naye akawaokoa katika mateso yao. Aliwatoa katika giza na ukiwa, na minyororo yao akaivunjavunja. Mshukuruni Mwenyezi-Mungu, kwa fadhili zake; kwa sababu ya maajabu aliyowatendea binadamu. Yeye huvunja na kufungua milango ya shaba, na kukatakata fito za chuma.
Zaburi 107:10-16 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Waliokaa katika giza na uvuli wa mauti, Wamefungwa katika taabu na minyororo, Kwa sababu waliyaasi maneno ya Mungu, Wakalidharau shauri lake Aliye Juu. Hata akawadhili moyo kwa taabu, Wakajikwaa, wala pasiwe na wa kuwasaidia. Wakamlilia BWANA katika dhiki zao, Akawaponya kutoka kwa shida zao. Aliwatoa katika giza na uvuli wa mauti, Akaivunja minyororo yao. Na wamshukuru BWANA kwa fadhili zake, Na maajabu yake kwa wanadamu. Maana ameivunja milango ya shaba, Ameyakata mapingo ya chuma.
Zaburi 107:10-16 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Waliokaa katika giza na uvuli wa mauti, Wamefungwa katika taabu na chuma, Kwa sababu waliyaasi maneno ya Mungu, Wakalidharau shauri lake Aliye juu. Hata akawadhili moyo kwa taabu, Wakajikwaa wala hakuna msaidizi. Wakamlilia BWANA katika dhiki zao, Akawaponya na shida zao. Aliwatoa katika giza na uvuli wa mauti, Akayavunja mafungo yao. Na wamshukuru BWANA kwa fadhili zake, Na maajabu yake kwa wanadamu. Maana ameivunja milango ya shaba, Ameyakata mapingo ya chuma.
Zaburi 107:10-16 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Wengine walikaa gizani na katika huzuni kuu, wafungwa wakiteseka katika minyororo, kwa sababu waliasi dhidi ya maneno ya Mungu, na kudharau ushauri wa Aliye Juu Sana. Aliwatumikisha kwa kazi ngumu; walijikwaa na hapakuwa na mtu wa kuwasaidia. Ndipo walipomlilia BWANA katika shida yao, naye akawaokoa kutoka taabu yao. Akawatoa katika giza na huzuni kuu na akavunja minyororo yao. Basi na wamshukuru BWANA kwa upendo wake usiokoma, na kwa matendo yake ya ajabu kwa wanadamu, kwa kuwa yeye huvunja malango ya shaba na kukata mapingo ya chuma.