Zaburi 106:7-28
Zaburi 106:7-28 Biblia Habari Njema (BHN)
Wazee wetu walipokuwa Misri, hawakujali matendo ya ajabu ya Mungu; hawakukumbuka wingi wa fadhili zake, bali walimwasi kando ya bahari ya Shamu. Hata hivyo Mungu aliwaokoa kama alivyoahidi, ili aoneshe nguvu yake kuu. Aliikemea bahari ya Shamu ikakauka; akawapitisha humo kama katika nchi kavu. Aliwaokoa mikononi mwa waliowachukia; aliwaokoa kutoka kwa nguvu za maadui zao. Maji ya bahari yaliwafunika maadui zao; wala hakusalia hata mmoja wao. Hapo watu wake wakaamini maneno yake, wakamwimbia tenzi za sifa yake. Lakini mara walisahau matendo yake, wakaacha kutegemea shauri lake. Walijawa na tamaa kubwa kule jangwani, wakamjaribu Mungu kule nyikani. Naye akawapa kile walichoomba, lakini akapeleka maradhi mabaya kati yao. Kule kambini walimwonea wivu Mose, na Aroni mtumishi mtakatifu wa Mwenyezi-Mungu. Ndipo ardhi ikafunguka ikammeza Dathani, na kumzika Abiramu na kundi lake lote; moto ukawatokea wafuasi wao, ukawateketeza watu hao waovu. Walitengeneza ndama wa dhahabu kule Horebu, wakaiabudu sanamu hiyo ya kusubu; waliubadilisha utukufu wa Mungu, kwa sanamu ya mnyama ambaye hula nyasi. Walimsahau Mungu aliyewaokoa, aliyetenda mambo makuu nchini Misri, maajabu katika nchi hiyo ya Hamu, na mambo ya kutisha katika bahari ya Shamu. Mungu alisema atawaangamiza watu wake, ila tu Mose mteule wake aliingilia kati, akaizuia hasira yake isiwaangamize. Kisha wakaidharau nchi ile ya kupendeza, kwa sababu hawakuwa na imani na ahadi ya Mungu. Walinungunika mahemani mwao, wala hawakumsikiliza Mwenyezi-Mungu. Hivyo Mungu akainua mkono akaapa kwamba atawaangamizia jangwani; atawatawanya wazawa wao kati ya watu, na kuwasambaza duniani kote. Kisha wakajiunga kumwabudu Baali kule Peori, wakala tambiko zilizotambikiwa mizimu.
Zaburi 106:7-28 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Baba zetu katika Misri Hawakuzingatia matendo yako ya ajabu; Hawakukumbuka wingi wa fadhili zako; Wakaasi penye bahari, Bahari ya Shamu. Lakini akawaokoa kwa ajili ya jina lake, Ayadhihirishe matendo yake makuu. Akaikemea Bahari ya Shamu ikakauka, Akawaongoza vilindini kana kwamba ni nchi kavu. Akawaokoa kutoka kwa mkono wa mtu adui, aliyewachukia, Na kuwakomboa kutoka kwa mkono wa adui zao. Maji yakawafunika watesi wao, Hakusalia hata mmoja wao. Ndipo walipoyaamini maneno yake, Waliziimba sifa zake. Lakini punde wakayasahau matendo yake, Wakakosa kungojea ushauri wake. Bali walitamani sana nyikani, Wakamjaribu Mungu jangwani. Akawapa walichomwomba, Lakini akawatumia ugonjwa wa kuwakondesha. Wakamhusudu Musa kambini, Na Haruni, mtakatifu wa BWANA. Nchi ikapasuka ikammeza Dathani, Ikaufunika mkutano wa Abiramu. Moto ukawaka katika mkutano wao, Miali yake ikawateketeza waovu. Walifanya ndama huko Horebu, Wakaisujudia sanamu ya kusubu. Wakaubadili utukufu wao Kuwa mfano wa ng'ombe mla majani. Wakamsahau Mungu, mwokozi wao, Aliyetenda makuu katika Misri. Matendo ya ajabu katika nchi ya Hamu, Mambo ya kutisha penye Bahari ya Shamu. Akasema ya kuwa atawaangamiza Kama Musa, mteule wake, asingalisimama, Mbele zake na kusimama palipobomoka, Ili aigeuze hasira yake asije akawaangamiza. Wakaidharau nchi ile ya kupendeza, Wala hawakuliamini neno lake. Bali wakanung'unika hemani mwao, Wala hawakuisikiliza sauti ya BWANA. Ndipo alipowainulia mkono wake na kuwaapia, Ya kuwa atawaangamiza jangwani, Na kuwatawanya wazao wao kati ya mataifa, Na kuwatapanya katika nchi mbali. Wakamwabudu Baal-Peori, Wakazila dhabihu zilizotolewa kwa wafu.
Zaburi 106:7-28 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Baba zetu katika Misri Hawakufikiri matendo yako ya ajabu; Hawakukumbuka wingi wa fadhili zako; Wakaasi penye bahari, bahari ya Shamu. Lakini akawaokoa kwa ajili ya jina lake, Ayadhihirishe matendo yake makuu. Akaikemea bahari ya Shamu ikakauka, Akawaongoza vilindini kana kwamba ni uwanda. Akawaokoa na mkono wa mtu aliyewachukia, Na kuwakomboa na mkono wa adui zao. Maji yakawafunika watesi wao, Hakusalia hata mmoja wao. Ndipo walipoyaamini maneno yake, Waliziimba sifa zake. Wakayasahau matendo yake kwa haraka, Hawakulingojea shauri lake. Bali walitamani sana jangwani, Wakamjaribu Mungu nyikani. Akawapa walichomtaka, Akawakondesha roho zao. Wakamhusudu Musa matuoni, Na Haruni, mtakatifu wa BWANA. Nchi ikapasuka ikammeza Dathani, Ikaufunika mkutano wa Abiramu. Moto ukawaka katika mkutano wao, Miali yake ikawateketeza wabaya. Walifanya ndama huko Horebu, Wakaisujudia sanamu ya kuyeyuka. Wakaubadili utukufu wao Kuwa mfano wa ng’ombe mla majani. Wakamsahau Mungu, mwokozi wao, Aliyetenda makuu katika Misri. Matendo ya ajabu katika nchi ya Hamu, Mambo ya kutisha penye bahari ya Shamu. Akasema ya kuwa atawaangamiza Kama Musa, mteule wake, asingalisimama, Mbele zake kama mahali palipobomoka, Ili aigeuze hasira yake asije akawaharibu. Wakaidharau nchi ile ya kupendeza, Wala hawakuliamini neno lake. Bali wakanung’unika hemani mwao, Wala hawakuisikiliza sauti ya BWANA. Ndipo alipowainulia mkono wake, Ya kuwa atawaangamiza jangwani, Na kuwatawanya wazao wao kati ya mataifa, Na kuwatapanya katika nchi mbali. Wakajiambatiza na Baal-Peori, Wakazila dhabihu za wafu.
Zaburi 106:7-28 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Baba zetu walipokuwa Misri, hawakuzingatia maajabu yako, wala hawakukumbuka wingi wa fadhili zako, bali waliasi kando ya bahari, ile Bahari ya Shamu. Hata hivyo aliwaokoa kwa ajili ya jina lake, ili apate kudhihirisha uweza wake mkuu. Alikemea Bahari ya Shamu, nayo ikakauka, akawaongoza katika vilindi vyake kama vile jangwani. Aliwaokoa mikononi mwa adui; kutoka mikononi mwa adui aliwakomboa. Maji yaliwafunika adui zao, hakunusurika hata mmoja. Ndipo walipoamini ahadi zake, nao wakaimba sifa zake. Lakini walisahau upesi aliyowatendea, wala hawakungojea ushauri wake. Jangwani walitawaliwa na tamaa zao, walimjaribu Mungu nyikani. Kwa hiyo aliwapa kile walichoomba, lakini akatuma juu yao ugonjwa wa kudhoofisha. Kambini walimwonea wivu Musa, na pia Haruni aliyekuwa amewekwa wakfu kwa BWANA. Ardhi ilifunguka ikawameza Dathani, ikawazika Abiramu na kundi lake. Moto uliwaka katikati ya wafuasi wao, mwali wa moto uliwateketeza waovu. Huko Horebu walitengeneza ndama, na kuabudu sanamu ya kusubu kwa chuma. Waliubadilisha Utukufu wao kwa sanamu ya fahali, ambaye hula majani. Walimsahau Mungu aliyewaokoa, aliyetenda mambo makuu huko Misri, miujiza katika nchi ya Hamu na mambo ya kutisha huko Bahari ya Shamu. Kwa hiyo alisema kwamba angewaangamiza: kama Musa mteule wake, asingesimama kati yao na Mungu kuizuia ghadhabu yake kuwaangamiza. Kisha waliidharau ile nchi nzuri, hawakuiamini ahadi yake. Walinungʼunika ndani ya mahema yao, wala hawakumtii BWANA. Kwa hiyo akaapa kwa mkono ulioinuliwa kwamba atawafanya waanguke jangwani, kuwatawanya wazao wao waanguke miongoni mwa mataifa, na kuwatawanya katika nchi zote. Walijifunga nira na Baali wa Peori, wakala dhabihu zilizotolewa kwa miungu isiyo na uhai.