Zaburi 106:7-12
Zaburi 106:7-12 Biblia Habari Njema (BHN)
Wazee wetu walipokuwa Misri, hawakujali matendo ya ajabu ya Mungu; hawakukumbuka wingi wa fadhili zake, bali walimwasi kando ya bahari ya Shamu. Hata hivyo Mungu aliwaokoa kama alivyoahidi, ili aoneshe nguvu yake kuu. Aliikemea bahari ya Shamu ikakauka; akawapitisha humo kama katika nchi kavu. Aliwaokoa mikononi mwa waliowachukia; aliwaokoa kutoka kwa nguvu za maadui zao. Maji ya bahari yaliwafunika maadui zao; wala hakusalia hata mmoja wao. Hapo watu wake wakaamini maneno yake, wakamwimbia tenzi za sifa yake.
Zaburi 106:7-12 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Baba zetu katika Misri Hawakuzingatia matendo yako ya ajabu; Hawakukumbuka wingi wa fadhili zako; Wakaasi penye bahari, Bahari ya Shamu. Lakini akawaokoa kwa ajili ya jina lake, Ayadhihirishe matendo yake makuu. Akaikemea Bahari ya Shamu ikakauka, Akawaongoza vilindini kana kwamba ni nchi kavu. Akawaokoa kutoka kwa mkono wa mtu adui, aliyewachukia, Na kuwakomboa kutoka kwa mkono wa adui zao. Maji yakawafunika watesi wao, Hakusalia hata mmoja wao. Ndipo walipoyaamini maneno yake, Waliziimba sifa zake.
Zaburi 106:7-12 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Baba zetu katika Misri Hawakufikiri matendo yako ya ajabu; Hawakukumbuka wingi wa fadhili zako; Wakaasi penye bahari, bahari ya Shamu. Lakini akawaokoa kwa ajili ya jina lake, Ayadhihirishe matendo yake makuu. Akaikemea bahari ya Shamu ikakauka, Akawaongoza vilindini kana kwamba ni uwanda. Akawaokoa na mkono wa mtu aliyewachukia, Na kuwakomboa na mkono wa adui zao. Maji yakawafunika watesi wao, Hakusalia hata mmoja wao. Ndipo walipoyaamini maneno yake, Waliziimba sifa zake.
Zaburi 106:7-12 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Baba zetu walipokuwa Misri, hawakuzingatia maajabu yako, wala hawakukumbuka wingi wa fadhili zako, bali waliasi kando ya bahari, ile Bahari ya Shamu. Hata hivyo aliwaokoa kwa ajili ya jina lake, ili apate kudhihirisha uweza wake mkuu. Alikemea Bahari ya Shamu, nayo ikakauka, akawaongoza katika vilindi vyake kama vile jangwani. Aliwaokoa mikononi mwa adui; kutoka mikononi mwa adui aliwakomboa. Maji yaliwafunika adui zao, hakunusurika hata mmoja. Ndipo walipoamini ahadi zake, nao wakaimba sifa zake.