Zaburi 106:24-31
Zaburi 106:24-31 Biblia Habari Njema (BHN)
Kisha wakaidharau nchi ile ya kupendeza, kwa sababu hawakuwa na imani na ahadi ya Mungu. Walinungunika mahemani mwao, wala hawakumsikiliza Mwenyezi-Mungu. Hivyo Mungu akainua mkono akaapa kwamba atawaangamizia jangwani; atawatawanya wazawa wao kati ya watu, na kuwasambaza duniani kote. Kisha wakajiunga kumwabudu Baali kule Peori, wakala tambiko zilizotambikiwa mizimu. Waliichochea hasira ya Mwenyezi-Mungu kwa matendo yao, maradhi mabaya yakazuka kati yao. Lakini Finehasi akasimama kufanya malipizi, na yale maradhi yakakoma. Jambo hilo lakumbukwa kwa heshima yake, tangu wakati huo na nyakati zote.
Zaburi 106:24-31 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Wakaidharau nchi ile ya kupendeza, Wala hawakuliamini neno lake. Bali wakanung'unika hemani mwao, Wala hawakuisikiliza sauti ya BWANA. Ndipo alipowainulia mkono wake na kuwaapia, Ya kuwa atawaangamiza jangwani, Na kuwatawanya wazao wao kati ya mataifa, Na kuwatapanya katika nchi mbali. Wakamwabudu Baal-Peori, Wakazila dhabihu zilizotolewa kwa wafu. Wakamkasirisha kwa matendo yao; Tauni ikawashambulia. Ndipo Finehasi akasimama akafanya hukumu; Tauni ikazuiliwa. Akahesabiwa kuwa ana haki Kizazi baada ya kizazi hata milele.
Zaburi 106:24-31 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Wakaidharau nchi ile ya kupendeza, Wala hawakuliamini neno lake. Bali wakanung’unika hemani mwao, Wala hawakuisikiliza sauti ya BWANA. Ndipo alipowainulia mkono wake, Ya kuwa atawaangamiza jangwani, Na kuwatawanya wazao wao kati ya mataifa, Na kuwatapanya katika nchi mbali. Wakajiambatiza na Baal-Peori, Wakazila dhabihu za wafu. Wakamkasirisha kwa matendo yao; Tauni ikawashambulia. Ndipo Finehasi akasimama akafanya hukumu; Tauni ikazuiliwa. Akahesabiwa kuwa ana haki Kizazi baada ya kizazi hata milele.
Zaburi 106:24-31 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Kisha waliidharau ile nchi nzuri, hawakuiamini ahadi yake. Walinungʼunika ndani ya mahema yao, wala hawakumtii BWANA. Kwa hiyo akaapa kwa mkono ulioinuliwa kwamba atawafanya waanguke jangwani, kuwatawanya wazao wao waanguke miongoni mwa mataifa, na kuwatawanya katika nchi zote. Walijifunga nira na Baali wa Peori, wakala dhabihu zilizotolewa kwa miungu isiyo na uhai. Waliichochea hasira ya BWANA, wakamkasirisha kwa matendo yao maovu, nayo tauni ikazuka katikati yao. Lakini Finehasi alisimama na kuingilia kati, nayo tauni ikazuiliwa. Hili likahesabiwa kwake haki, kwa vizazi visivyo na mwisho vijavyo.