Zaburi 106:13-23
Zaburi 106:13-23 Biblia Habari Njema (BHN)
Lakini mara walisahau matendo yake, wakaacha kutegemea shauri lake. Walijawa na tamaa kubwa kule jangwani, wakamjaribu Mungu kule nyikani. Naye akawapa kile walichoomba, lakini akapeleka maradhi mabaya kati yao. Kule kambini walimwonea wivu Mose, na Aroni mtumishi mtakatifu wa Mwenyezi-Mungu. Ndipo ardhi ikafunguka ikammeza Dathani, na kumzika Abiramu na kundi lake lote; moto ukawatokea wafuasi wao, ukawateketeza watu hao waovu. Walitengeneza ndama wa dhahabu kule Horebu, wakaiabudu sanamu hiyo ya kusubu; waliubadilisha utukufu wa Mungu, kwa sanamu ya mnyama ambaye hula nyasi. Walimsahau Mungu aliyewaokoa, aliyetenda mambo makuu nchini Misri, maajabu katika nchi hiyo ya Hamu, na mambo ya kutisha katika bahari ya Shamu. Mungu alisema atawaangamiza watu wake, ila tu Mose mteule wake aliingilia kati, akaizuia hasira yake isiwaangamize.
Zaburi 106:13-23 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Lakini punde wakayasahau matendo yake, Wakakosa kungojea ushauri wake. Bali walitamani sana nyikani, Wakamjaribu Mungu jangwani. Akawapa walichomwomba, Lakini akawatumia ugonjwa wa kuwakondesha. Wakamhusudu Musa kambini, Na Haruni, mtakatifu wa BWANA. Nchi ikapasuka ikammeza Dathani, Ikaufunika mkutano wa Abiramu. Moto ukawaka katika mkutano wao, Miali yake ikawateketeza waovu. Walifanya ndama huko Horebu, Wakaisujudia sanamu ya kusubu. Wakaubadili utukufu wao Kuwa mfano wa ng'ombe mla majani. Wakamsahau Mungu, mwokozi wao, Aliyetenda makuu katika Misri. Matendo ya ajabu katika nchi ya Hamu, Mambo ya kutisha penye Bahari ya Shamu. Akasema ya kuwa atawaangamiza Kama Musa, mteule wake, asingalisimama, Mbele zake na kusimama palipobomoka, Ili aigeuze hasira yake asije akawaangamiza.
Zaburi 106:13-23 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Wakayasahau matendo yake kwa haraka, Hawakulingojea shauri lake. Bali walitamani sana jangwani, Wakamjaribu Mungu nyikani. Akawapa walichomtaka, Akawakondesha roho zao. Wakamhusudu Musa matuoni, Na Haruni, mtakatifu wa BWANA. Nchi ikapasuka ikammeza Dathani, Ikaufunika mkutano wa Abiramu. Moto ukawaka katika mkutano wao, Miali yake ikawateketeza wabaya. Walifanya ndama huko Horebu, Wakaisujudia sanamu ya kuyeyuka. Wakaubadili utukufu wao Kuwa mfano wa ng’ombe mla majani. Wakamsahau Mungu, mwokozi wao, Aliyetenda makuu katika Misri. Matendo ya ajabu katika nchi ya Hamu, Mambo ya kutisha penye bahari ya Shamu. Akasema ya kuwa atawaangamiza Kama Musa, mteule wake, asingalisimama, Mbele zake kama mahali palipobomoka, Ili aigeuze hasira yake asije akawaharibu.
Zaburi 106:13-23 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Lakini mara walisahau aliyowatendea, wala hawakungojea shauri lake. Jangwani walitawaliwa na tamaa zao, walimjaribu Mungu nyikani. Kwa hiyo aliwapa kile walichoomba, lakini akatuma juu yao ugonjwa wa kudhoofisha. Kambini walimwonea wivu Mose, na pia Aroni aliyekuwa amewekwa wakfu kwa BWANA. Ardhi ilifunguka ikawameza Dathani, ikawazika Abiramu na kundi lake. Moto uliwaka katikati ya wafuasi wao, mwali wa moto uliwateketeza waovu. Huko Horebu walitengeneza ndama, na kuabudu sanamu ya kusubu kwa chuma. Waliubadilisha Utukufu wao kwa sanamu ya fahali, ambaye hula majani. Walimsahau Mungu aliyewaokoa, aliyekuwa ametenda mambo makuu huko Misri, miujiza katika nchi ya Hamu na mambo ya kutisha huko Bahari ya Shamu. Kwa hiyo alisema kwamba angewaangamiza: kama Mose mteule wake, asingesimama kati yao na Mungu kuizuia ghadhabu yake kuwaangamiza.