Zaburi 10:7-18
Zaburi 10:7-18 Biblia Habari Njema (BHN)
Kinywa chake kimejaa laana, udanganyifu na dhuluma; mwepesi kusema maneno ya kuchukiza na maovu. Hujificha vijijini huku anaotea, amuue kwa siri mtu asiye na hatia. Yuko macho kumvizia mnyonge; huotea mafichoni mwake kama simba. Huvizia apate kuwakamata maskini; huwanasa kwa mtego wake na kuwachukua. Mnyonge huvamiwa na kuangushwa chini; huangushwa kwa ukatili wa mtu mwovu. Mwovu huwaza moyoni mwake: “Mungu amesahau; ameficha uso wake, haoni kitu!” Inuka, ee Mwenyezi-Mungu, uwaadhibu; usiwasahau wanaodhulumiwa. Ee Mungu, kwa nini mwovu anakudharau, na kusema ati hutamfanya awajibike? Lakini wewe wawaona wenye dhiki na shida; nawe daima uko tayari kuwasaidia. Mnyonge anakutegemea wewe, ee Mungu, wewe umekuwa daima msaada wa yatima. Uzivunje nguvu za mtu mwovu; ukomeshe uovu wake wote, usiwepo tena. Mwenyezi-Mungu ni mfalme milele na milele! Mataifa yasiyomjua yatatoweka nchini mwake. Ee Mwenyezi-Mungu, wapokea dua za mnyonge; wampa moyo na kumtegea sikio. Utawatendea haki yatima na wanaodhulumiwa, binadamu aliye udongo asiweze tena kuleta hofu.
Zaburi 10:7-18 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kinywa chake kimejaa laana, Na hila na dhuluma. Chini ya ulimi wake kuna madhara na uovu, Hujificha na kuotea vijijini. Katika maficho humwua asiye na hatia, Macho yake humtazama kisiri mtu duni. Huotea faraghani kama simba pangoni, Huotea amkamate mtu mnyonge. Naam, humkamata mtu mnyonge, Na kumkokota akiwa wavuni mwake. Hujikunyata na kuinama; Watu duni huanguka kwa nguvu zake. Asema moyoni mwake, Mungu amesahau, Auficha uso wake, haoni kamwe. Inuka, Ee Mungu BWANA, uuinue mkono wako, Ee Mungu Usiwasahau wanyonge. Kwa nini mdhalimu amdharau Mungu. Akisema moyoni mwake, Hutapatiliza? Umeona, maana unaangalia matatizo na dhiki, Uyatwae mkononi mwako. Mtu duni hukuachia nafsi yake, Maana umekuwa msaidizi wa yatima. Uuvunje mkono wa mdhalimu, Na mwovu, uipatilize dhuluma yake, hadi usiione. BWANA ndiye Mfalme milele na milele; Mataifa yataangamia kutoka nchi yake. BWANA, utayasikia matakwa ya wanyonge, Uutaidhibiti mioyo yao, utalitega sikio lako. Ili kumhukumu yatima na aliyeonewa, Binadamu aliye udongo asizidi kudhulumu.
Zaburi 10:7-18 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Kinywa chake kimejaa laana, Na hila na dhuluma. Chini ya ulimi wake kuna madhara na uovu, Hukaa katika maoteo ya vijiji. Mahali pa siri humwua asiye na hatia, Macho yake humvizia mtu duni. Huotea faraghani kama simba pangoni, Huotea amkamate mtu mnyonge. Naam, humkamata mtu mnyonge, Akimkokota wavuni mwake. Hujikunyata na kuinama; Watu duni huanguka kwa nguvu zake. Asema moyoni mwake, Mungu amesahau, Auficha uso wake, haoni kamwe. BWANA, uondoke, Ee Mungu, uuinue mkono wako, Usiwasahau wanyonge. Kwani mdhalimu kumdharau Mungu. Akisema moyoni mwake, Hutapatiliza? Umeona, maana unaangalia madhara na jeuri, Uyatwae mkononi mwako. Mtu duni hukuachia nafsi yake, Maana umekuwa msaidizi wa yatima. Uuvunje mkono wake mdhalimu, Na mbaya, uipatilize dhuluma yake, hata usiione. BWANA ndiye Mfalme milele na milele; Mataifa wamepotea kutoka nchi yake. BWANA, umeisikia tamaa ya wanyonge, Utaitengeneza mioyo yao, utalitega sikio lako. Ili kumhukumu yatima naye aliyeonewa, Binadamu aliye udongo asizidi kudhulumu.
Zaburi 10:7-18 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Kinywa chake kimejaa laana, uongo na vitisho; shida na ubaya viko chini ya ulimi wake. Huvizia karibu na vijiji; kutoka mafichoni huwanasa wasio na hatia, akivizia wapitaji. Huvizia kama simba aliye mawindoni; huvizia kumkamata mnyonge, huwakamata wanyonge na kuwaburuza katika wavu wake. Mateka wake hupondwa, huzimia; wanaanguka katika nguvu zake. Anajisemea mwenyewe, “Mungu amesahau, huficha uso wake na haoni kabisa.” Inuka BWANA! Inua mkono wako, Ee Mungu. Usiwasahau wanyonge. Kwa nini mtu mwovu anamtukana Mungu? Kwa nini anajiambia mwenyewe, “Hataniita nitoe hesabu”? Lakini wewe, Ee Mungu, unaona shida na huzuni, umekubali kuyapokea mkononi mwako. Mhanga anajisalimisha kwako, wewe ni msaada wa yatima. Vunja mkono wa mtu mbaya na mwovu; mwite mtu mbaya atoe hesabu ya uovu wake ambao usingejulikana vinginevyo. BWANA ni Mfalme milele na milele, mataifa wataangamia watoke nchini mwake. Unasikia, Ee BWANA, shauku ya wanaoonewa; wewe huwatia moyo, na kusikiliza kilio chao, ukiwatetea yatima na waliodhulumiwa, ili mwanadamu ambaye ni udongo asiogopeshe tena.