Zaburi 10:3-11
Zaburi 10:3-11 Biblia Habari Njema (BHN)
Mwovu hujisifia tamaa zake mbaya, mtu wa tamaa hulaani na kumkataa Mwenyezi-Mungu. Katika majivuno yake husema: “Mungu hatagundua.” Mawazo yake yote ni: “Hakuna Mungu.” Njia za mwovu hufanikiwa daima; kwake hukumu zako ziko mbali na mawazo yake, na huwadharau maadui zake wote. Huwaza moyoni: “Sitakuwa na wasiwasi; sitapatwa na dhiki maishani.” Kinywa chake kimejaa laana, udanganyifu na dhuluma; mwepesi kusema maneno ya kuchukiza na maovu. Hujificha vijijini huku anaotea, amuue kwa siri mtu asiye na hatia. Yuko macho kumvizia mnyonge; huotea mafichoni mwake kama simba. Huvizia apate kuwakamata maskini; huwanasa kwa mtego wake na kuwachukua. Mnyonge huvamiwa na kuangushwa chini; huangushwa kwa ukatili wa mtu mwovu. Mwovu huwaza moyoni mwake: “Mungu amesahau; ameficha uso wake, haoni kitu!”
Zaburi 10:3-11 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Maana mdhalimu hujisifia tamaa ya nafsi yake, Na mwenye choyo humkana BWANA na kumdharau. Mdhalimu kwa kiburi cha uso wake Asema, Mungu Hatapatiliza. Mawazo yake yote ni, Hakuna Mungu; Njia zake ni thabiti kila wakati. Hukumu zako ziko juu asizione, Adui zake wote awakaripia. Asema moyoni mwake, Sitaondoshwa, Kizazi baada ya kizazi sitakuwamo taabuni. Kinywa chake kimejaa laana, Na hila na dhuluma. Chini ya ulimi wake kuna madhara na uovu, Hujificha na kuotea vijijini. Katika maficho humwua asiye na hatia, Macho yake humtazama kisiri mtu duni. Huotea faraghani kama simba pangoni, Huotea amkamate mtu mnyonge. Naam, humkamata mtu mnyonge, Na kumkokota akiwa wavuni mwake. Hujikunyata na kuinama; Watu duni huanguka kwa nguvu zake. Asema moyoni mwake, Mungu amesahau, Auficha uso wake, haoni kamwe.
Zaburi 10:3-11 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Maana mdhalimu hujisifia tamaa ya nafsi yake, Na mwenye choyo humkana BWANA na kumdharau. Mdhalimu kwa kiburi cha uso wake Asema, Hatapatiliza. Jumla ya mawazo yake ni, Hakuna Mungu; Njia zake ni thabiti kila wakati. Hukumu zako ziko juu asizione, Adui zake wote awafyonya. Asema moyoni mwake, Sitaondoshwa, Kizazi baada ya kizazi sitakuwamo taabuni. Kinywa chake kimejaa laana, Na hila na dhuluma. Chini ya ulimi wake kuna madhara na uovu, Hukaa katika maoteo ya vijiji. Mahali pa siri humwua asiye na hatia, Macho yake humvizia mtu duni. Huotea faraghani kama simba pangoni, Huotea amkamate mtu mnyonge. Naam, humkamata mtu mnyonge, Akimkokota wavuni mwake. Hujikunyata na kuinama; Watu duni huanguka kwa nguvu zake. Asema moyoni mwake, Mungu amesahau, Auficha uso wake, haoni kamwe.
Zaburi 10:3-11 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Hujivunia tamaa za moyo wake; humbariki mlafi na kumtukana BWANA. Katika kiburi chake, mwovu hamtafuti Mungu, katika mawazo yake yote hakuna nafasi ya Mungu. Njia zake daima hufanikiwa; hujivuna na amri zako ziko mbali naye, huwacheka kwa dharau adui zake wote. Anajisemea mwenyewe, “Hakuna kitakachonitikisa, daima nitakuwa na furaha, kamwe sitakuwa na shida.” Kinywa chake kimejaa laana, uongo na vitisho; shida na ubaya viko chini ya ulimi wake. Huvizia karibu na vijiji; kutoka mafichoni huwanasa wasio na hatia, akivizia wapitaji. Huvizia kama simba aliye mawindoni; huvizia kumkamata mnyonge, huwakamata wanyonge na kuwaburuza katika wavu wake. Mateka wake hupondwa, huzimia; wanaanguka katika nguvu zake. Anajisemea mwenyewe, “Mungu amesahau, huficha uso wake na haoni kabisa.”