Methali 9:1-18
Methali 9:1-18 Biblia Habari Njema (BHN)
Hekima amejenga nyumba yake, nyumba yenye nguzo saba. Amechinja wanyama wa karamu, divai yake ameitayarisha, ametandika meza yake. Amewatuma watumishi wake wa kike mjini, waite watu kutoka kwenye vilele vya miinuko: “Yeyote aliye mjinga na aje hapa!” Na yeyote aliye mpumbavu humwambia: “Njoo ukale chakula, na unywe divai niliyotengeneza. Achana na ujinga upate kuishi; fuata njia ya akili.” Anayemkosoa mwenye dharau hupata matusi, amkaripiaye mwovu huishia kwa kuumizwa. Usimwonye mwenye dharau maana atakuchukia; mwonye mwenye hekima naye atakupenda. Mfunze mwenye hekima naye atazidi kuwa na hekima; mfundishe mwadilifu naye atazidi kuelimika. Kumcha Mwenyezi-Mungu ni msingi wa hekima; na kumjua yule Mtakatifu ni kupata akili. Kwa msaada wangu mimi Hekima siku zako zitaongezwa; utaongezewa miaka mingi maishani mwako. Kama una hekima, itakufaa wewe mwenyewe; kama ukiidharau, mwenyewe utapata hasara. Mwanamke mpumbavu ana kelele, hajui kitu wala hana haya. Hukaa kitako mlangoni mwa nyumba yake, huweka kiti chake mahali pa juu mjini, na kuwaita watu wapitao njiani, watu wanaokwenda kwenye shughuli zao: “Yeyote aliye mjinga na aje hapa!” Na yeyote aliye mpumbavu humwambia: “Maji ya wizi ni matamu sana; mkate unaoliwa kwa siri ni mzuri sana.” Lakini mjinga hajui kwamba humo mna wafu, wageni wa mwanamke huyo wamo chini Kuzimu.
Methali 9:1-18 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Hekima ameijenga nyumba yake, Amezichonga nguzo zake saba; Amechinja nyama zake, amechanganya divai yake, Ameiandalia meza yake pia. Amewatuma wajakazi wake, analia, Mahali pa mjini palipoinuka sana, Kila aliye mjinga na aingie humu. Tena amwambia mtu aliyepungukiwa na akili, Njoo ule mkate wangu, Ukanywe divai niliyoichanganya. Enyi wajinga, acheni ujinga, mkaishi, Mkaende katika njia ya ufahamu. Amkemeaye mwenye dharau hujipatia fedheha; Amkaripiaye mtu mbaya hujipatia aibu. Usimkaripie mwenye dharau, asije akakuchukia; Mkaripie mwenye hekima, naye atakupenda. Mwelimishe mwenye hekima, naye atazidi kuwa na hekima; Mfundishe mwenye haki, naye atazidi kuwa na elimu; Kumcha BWANA ni mwanzo wa hekima; Na kumjua Mtakatifu ni ufahamu. Maana, kwa msaada wangu siku zako zitazidishwa; Na miaka ya maisha yako itaongezwa. Kama una hekima, una hekima kwa nafsi yako; Na kama una dharau, utaichukua peke yako. Mwanamke mpumbavu hupiga kelele, Ni mjinga, hajui kitu. Hukaa mlangoni pa nyumba yake, Juu ya kiti mahali pa mjini palipoinuka, Apate kuwaita wapitao njiani, Waendao moja kwa moja katika njia zao. Kila aliye mjinga na aingie humu. Tena amwambia mtu aliyepungukiwa na akili, Maji yaliyoibiwa ni matamu, Na mkate ulioliwa kwa siri hupendeza. Lakini huyo hajui ya kuwa wafu wamo humo; Ya kuwa wageni wake wamo chini kuzimuni.
Methali 9:1-18 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Hekima umeijenga nyumba yake, Amezichonga nguzo zake saba; Amechinja nyama zake, umechanganya divai yake, Ameiandalia meza yake pia. Amewatuma wajakazi wake, analia, Mahali pa mjini palipoinuka sana, Kila aliye mjinga na aingie humu. Tena amwambia mtu aliyepungukiwa na akili, Njoo ule mkate wangu, Ukanywe divai niliyoichanganya. Enyi wajinga, acheni ujinga, mkaishi, Mkaende katika njia ya ufahamu. Amkemeaye mwenye dharau hujipatia fedheha; Amkaripiaye mtu mbaya hujipatia aibu. Usimkaripie mwenye dharau, asije akakuchukia; Mkaripie mwenye hekima, naye atakupenda. Mwelimishe mwenye hekima, naye atazidi kuwa na hekima; Mfundishe mwenye haki, naye atazidi kuwa na elimu; Kumcha BWANA ni mwanzo wa hekima; Na kumjua Mtakatifu ni ufahamu. Maana, kwa msaada wangu siku zako zitazidishwa; Na miaka ya maisha yako itaongezwa. Kama una hekima, una hekima kwa nafsi yako; Na kama una dharau, utaichukua peke yako. Mwanamke mpumbavu hupiga kelele, Ni mjinga, hajui kitu. Hukaa mlangoni pa nyumba yake, Juu ya kiti mahali pa mjini palipoinuka, Apate kuwaita wapitao njiani, Waendao moja kwa moja katika njia zao. Kila aliye mjinga na aingie humu. Tena amwambia mtu aliyepungukiwa na akili, Maji yaliyoibiwa ni matamu, Na mkate ulioliwa kwa siri hupendeza. Lakini huyo hajui ya kuwa wafu wamo humo; Ya kuwa wageni wake wamo chini kuzimuni.
Methali 9:1-18 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Hekima amejenga nyumba yake; amechonga nguzo zake saba. Ameandaa nyama na kuchanganya divai yake; pia ameandaa meza yake. Amewatuma wajakazi wake, naye huita kutoka mahali pa juu sana pa mji. Anawaambia wale wasio na akili, “Wote ambao ni wajinga na waje hapa! Njooni, mle chakula changu na mnywe divai niliyoichanganya. Acheni njia zenu za ujinga nanyi mtaishi; tembeeni katika njia ya ufahamu. “Yeyote anayemkosoa mwenye dhihaka hukaribisha matusi; yeyote anayekemea mtu mwovu hupatwa na matusi. Usimkemee mwenye dhihaka, la sivyo atakuchukia; mkemee mwenye hekima naye atakupenda. Mfundishe mtu mwenye hekima naye atakuwa na hekima zaidi; mfundishe mtu mwadilifu naye atazidi kufundishika. “Kumcha BWANA ndicho chanzo cha hekima, na kumjua Aliye Mtakatifu ni ufahamu. Kwa maana kwa msaada wangu siku zako zitakuwa nyingi, na miaka itaongezwa katika maisha yako. Kama wewe una hekima, hekima yako itakupa tuzo; kama wewe ni mtu wa mzaha, wewe mwenyewe ndiwe utateseka.” Mwanamke aitwaye Mpumbavu ana kelele; hana adabu na hana maarifa. Huketi kwenye mlango wa nyumba yake, kwenye kiti katika mahali pa juu sana pa mji, akiita wale wanaopita karibu, wanaoenda moja kwa moja kwenye njia yao. Anawaambia wale wasio na akili, “Wote ambao ni wajinga na waje hapa ndani! Maji yaliyoibiwa ni matamu; chakula kinacholiwa sirini ni kitamu!” Lakini hawajui hata kidogo kuwa wafu wako humo, kwamba wageni wake huyo mwanamke wako katika vilindi vya Kuzimu.