Methali 7:1-27
Methali 7:1-27 Biblia Habari Njema (BHN)
Mwanangu, yashike maneno yangu, zihifadhi kwako amri zangu. Zifuate amri zangu nawe utaishi; yalinde mafundisho yangu kama mboni ya jicho lako. Yafunge vidoleni mwako; yaandike moyoni mwako. Iambie Hekima: “Wewe ni dada yangu”, na Busara “Wewe ni rafiki yangu”. Vitakulinda mbali na mwanamke mbaya, vitakuepusha na maneno matamu ya mwanamke mgeni. Siku moja dirishani mwa nyumba yangu, nilichungulia nje kupitia viunzi vya dirisha, nikawaona vijana wengi wajinga, na mmoja hasa aliyekuwa mpumbavu. Huyo alikuwa akitembea kwenye barabara ile, karibu na kona alikoishi mwanamke fulani. Basi akashika njia iendayo nyumbani kwa mwanamke huyo. Ilikuwa yapata wakati wa jioni, giza na usiku vilikuwa vimeanza kuingia. Punde kijana akakutana na huyo mwanamke; amevalia kama malaya, ana mipango yake. Alikuwa mwanamke wa makelele na mkaidi; miguu yake haitulii nyumbani: Mara barabarani, mara sokoni, katika kila kona ya njia hakosekani akivizia. Alimkumbatia kijana huyo na kumbusu, na kwa maneno matamu, akamwambia: “Ilinilazimu kutoa tambiko zangu; leo hii nimekamilisha nadhiri yangu. Ndio maana nimetoka ili nikulaki, nimekutafuta kwa hamu nikakupata. Nimetandika kitanda changu vizuri, kwa shuka za rangi za kitani kutoka Misri. Nimekitia manukato, manemane, udi na mdalasini. Njoo tulale pamoja mpaka asubuhi; njoo tujifurahishe kwa mahaba. Mume wangu hayumo nyumbani, amekwenda safari ya mbali. Amechukua bunda la fedha; hatarejea nyumbani karibuni.” Alimshawishi kwa maneno mengi ya kubembeleza; kijana akashawishika kwa maneno yake matamu. Hapo akamfuata huyo mwanamke moja kwa moja, kama ng'ombe aendaye machinjioni, kama paa arukiaye mtegoni. Hakutambua kwamba hiyo itamgharimu maisha yake, mpaka alipojikuta amekuwa kama amechomwa mshale moyoni, amekuwa kama ndege aliyenaswa wavuni. Sasa wanangu, nisikilizeni; yategeeni sikio maneno ya kinywa changu. Msikubali kuongozwa na mwanamke kama huyo, wala msipitepite katika mapito yake. Maana amewaangusha wanaume wengi; ni wengi mno hao aliowachinja. Nyumba yake ni njia ya kwenda kuzimu, ni mahali pa kuteremkia mautini.
Methali 7:1-27 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Mwanangu, yashike maneno yangu, Na kuziweka amri zangu akiba kwako. Uzishike amri zangu ukaishi, Na sheria yangu kama mboni ya jicho lako. Zifunge katika vidole vyako; Ziandike juu ya kibao cha moyo wako. Mwambie hekima, Wewe ndiwe dada yangu; Mwite ufahamu jamaa yako mwandani. Wapate kukulinda na malaya, Na mwasherati akubembelezaye kwa maneno yake. Maana katika dirisha la nyumba yangu Nilichungulia katika shubaka yake. Nikaona katikati ya wajinga, Nikamtambua miongoni mwa vijana, Kijana mmoja asiyekuwa na akili, Akipita njiani karibu na pembe yake, Akiishika njia iendayo nyumbani kwake, Wakati wa magharibi, wakati wa jioni, Usiku wa manane, gizani. Na tazama, mwanamke akamkuta, Ana mavazi ya kikahaba, mwerevu wa moyo; Ana kelele, na ukaidi; Miguu yake haikai nyumbani mwake. Mara yuko katika njia kuu, mara viwanjani, Naye huotea kwenye pembe za kila njia. Basi akamshika, akambusu, Akamwambia kwa uso usio na haya, Kwangu ziko sadaka za amani; Leo hivi nimeziondoa nadhiri zangu; Ndiyo maana nikatoka nikulaki, Nikutafute uso wako kwa bidii, nami nimekuona. Nimetandika kitanda changu, magodoro mazuri, Kwa matandiko ya Kimisri yenye mistari. Nimetia kitanda changu manukato, Manemane na udi na mdalasini. Haya, na tushibe upendo hadi asubuhi, Tujifurahishe nafsi zetu kwa mahaba. Maana mume wangu hayumo nyumbani, Amekwenda safari ya mbali; Amechukua mfuko wa fedha mkononi; Atarudi wakati wa mwezi mpevu. Kwa maneno yake mengi na ulaini akamshawishi, Kwa ubembelezi wa midomo yake akamshinda. Huyo akafuatana naye mara hiyo, Kama vile ng'ombe aendavyo machinjoni; Au mpumbavu kuadhibiwa katika pingu; Hata mshale umchome maini; Kama ndege aendaye haraka mtegoni; Wala hajui ya kuwa ni hasara ya nafsi yake. Basi, wanangu, nisikilizeni sasa, Mkayaangalie maneno ya kinywa changu. Moyo wako usizielekee njia zake, Wala usipotee katika mapito yake. Maana amewaangusha wengi aliowajeruhi, Naam, jumla ya waliouawa naye ni wengi. Nyumba yake ni njia ya kwenda kuzimu, Hushuka mpaka vyumba vya mauti.
Methali 7:1-27 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Mwanangu, yashike maneno yangu, Na kuziweka amri zangu akiba kwako. Uzishike amri zangu ukaishi, Na sheria yangu kama mboni ya jicho lako. Zifunge katika vidole vyako; Ziandike juu ya kibao cha moyo wako. Mwambie hekima, Wewe ndiwe umbu langu; Mwite ufahamu jamaa yako mwanamke. Wapate kukulinda na malaya, Na mgeni akubembelezaye kwa maneno yake. Maana katika dirisha la nyumba yangu Nalichungulia katika shubaka yake; Nikaona katikati ya wajinga, Nikamtambua miongoni mwa vijana, Kijana mmoja asiyekuwa na akili, Akipita njiani karibu na pembe yake, Akiishika njia iendayo nyumbani kwake, Wakati wa magharibi, wakati wa jioni, Usiku wa manane, gizani. Na tazama, mwanamke akamkuta, Ana mavazi ya kikahaba, mwerevu wa moyo; Ana kelele, na ukaidi; Miguu yake haikai nyumbani mwake. Mara yu katika njia kuu, mara viwanjani, Naye huotea kwenye pembe za kila njia. Basi akamshika, akambusu, Akamwambia kwa uso usio na haya, Kwangu ziko sadaka za amani; Leo hivi nimeziondoa nadhiri zangu; Ndiyo maana nikatoka nikulaki, Nikutafute uso wako kwa bidii, nami nimekuona. Nimetandika kitanda changu, magodoro mazuri, Kwa matandiko ya Kimisri yenye mistari. Nimetia kitanda changu manukato, Manemane na udi na mdalasini. Haya, na tushibe upendo hata asubuhi, Tujifurahishe nafsi zetu kwa mahaba. Maana mume wangu hayumo nyumbani, Amekwenda safari ya mbali; Amechukua mfuko wa fedha mkononi; Atarudi wakati wa mwezi mpevu. Kwa maneno yake mengi na ulaini akamshawishi, Kwa ubembelezi wa midomo yake akamshinda. Huyo akafuatana naye mara hiyo, Kama vile ng’ombe aendavyo machinjoni; Au mpumbavu kuadhibiwa katika pingu; Hata mshale umchome maini; Kama ndege aendaye haraka mtegoni; Wala hajui ya kuwa ni hasara ya nafsi yake. Basi, wanangu, nisikilizeni sasa, Mkayaangalie maneno ya kinywa changu. Moyo wako usizielekee njia zake, Wala usipotee katika mapito yake. Maana amewaangusha wengi waliojeruhi, Naam, jumla ya waliouawa naye ni jeshi kubwa. Nyumba yake ni njia ya kwenda kuzimu, Hushuka mpaka vyumba vya mauti.
Methali 7:1-27 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Mwanangu, shika maneno yangu na kuzihifadhi amri zangu ndani yako. Shika amri zangu nawe utaishi; linda mafundisho yangu kama mboni ya jicho lako. Yafunge katika vidole vyako; yaandike katika kibao cha moyo wako. Mwambie hekima, “Wewe ni dada yangu,” uite ufahamu jamaa yako; watakuepusha na mwanamke mzinzi, kutokana na mwanamke mpotovu na maneno yake ya kubembeleza. Kwenye dirisha la nyumba yangu nilitazama nje kupitia upenyo kwenye mwimo wa dirisha. Niliona miongoni mwa wajinga, nikagundua miongoni mwa wanaume vijana, kijana asiye na akili. Alikuwa akishuka njiani karibu na pembe ya kwake, akielekea kwenye nyumba ya huyo mwanamke wakati wa machweo, jua likipungua nuru yake, giza la usiku lilipokuwa likiingia. Ndipo huyo mwanamke akatoka kumlaki, hali amevaa kama kahaba akiwa na nia ya hila. (Ni mwanamke mwenye makelele na mkaidi, miguu yake haitulii nyumbani; mara kwenye barabara za mji, mara kwenye viwanja vikubwa, kwenye kila pembe huvizia.) Huyo mwanamke alimkumbatia kijana na kumbusu, na kwa uso usio na haya akamwambia: “Nina sadaka za amani nyumbani; leo nimetimiza nadhiri zangu. Kwa hiyo nimetoka nje kukulaki; nimekutafuta na nimekupata! Nimetandika kitanda changu kwa kitani za rangi kutoka Misri. Nimetia manukato kitanda changu kwa manemane, udi na mdalasini. Njoo, tuzame katika mapenzi hadi asubuhi; tujifurahishe wenyewe kwa mapenzi! Mume wangu hayupo nyumbani; ameenda safari ya mbali. Amechukua mkoba uliojazwa fedha na hatakuwa nyumbani karibuni.” Kwa maneno laini yule mwanamke akampotosha; alimshawishi kwa maneno yake laini. Mara huyo kijana alimfuata yule mwanamke kama fahali aendaye machinjoni, kama kulungu aingiaye kwenye kitanzi, hadi mshale umchome ini lake, kama ndege anayenaswa kwenye mtego, bila kujua itamgharimu maisha yake. Sasa basi wanangu, nisikilizeni; sikilizeni kwa makini nisemalo. Usiruhusu moyo wako ugeukie njia za huyo mwanamke, wala usitangetange katika mapito yake. Aliowaangusha ni wengi; aliowachinja ni kundi kubwa. Nyumba yake ni njia kuu iendayo kaburini, ielekeayo chini kwenye vyumba vya mauti.