Methali 27:5-14
Methali 27:5-14 Biblia Habari Njema (BHN)
Afadhali mtu anayekuonya waziwazi, kuliko yule afichaye upendo. Makaripio ya rafiki yaonesha uaminifu, lakini busu la adui ni udanganyifu. Aliyeshiba hata asali huikataa, lakini kwa mwenye njaa kila kichungu ni kitamu. Mtu aliyepotea mbali na kwake, ni kama ndege aliyepotea mbali na kiota chake. Mafuta na manukato huufurahisha moyo, lakini taabu hurarua roho. Usisahau rafiki zako wala wa baba yako. Ukipatwa na janga usikimbilie kwa nduguyo; afadhali jirani aliye karibu kuliko ndugu aliye mbali. Uwe na hekima mwanangu upate kunifurahisha moyo, nami sitakosa la kumjibu yeyote anayenilaumu. Mwenye busara huona hatari akajificha, lakini mjinga hujitokeza mbele akaumia. Mtu akiahidi mbele yako kumdhamini mgeni, chukua nguo yake; mfanye awajibike kwa kuwadhamini wageni. Amwamkiaye jirani kwa kelele alfajiri, itaeleweka kwamba amemtakia laana.
Methali 27:5-14 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Lawama ya wazi ni heri, Kuliko upendo uliositirika. Majeraha utiwazo na rafiki ni ya kweli; Bali busu la adui ni udanganyifu. Nafsi iliyoshiba hukinai sega la asali; Bali nafsi yenye njaa huona kila kitu kichungu kuwa kitamu. Kama ndege aendaye huku na huko mbali na kitundu chake; Ndivyo alivyo mtu aendaye huku na huko mbali na mahali pake. Marhamu na manukato huufurahisha moyo; Kadhalika utamu wa rafiki ya mtu utokao katika kusudi la moyo wake. Usimwache rafiki yako mwenyewe, wala rafiki ya baba yako, Wala usiende nyumbani mwa ndugu yako siku ya msiba wako. Afadhali jirani aliye karibu kuliko ndugu aliye mbali. Mwanangu, uwe na hekima na kunifurahisha moyo wangu; Ili nipate kumjibu anilaumuye. Mwenye busara huyaona mabaya na kujificha; Bali wajinga huendelea mbele wakaumia. Twaa nguo yake amdhaminiye mgeni; Mtoza rehani aliye mdhamini wa malaya. Mtu ambarikiye mwenzake kwa sauti kuu asubuhi na mapema; Itahesabiwa kuwa ni laana kwake.
Methali 27:5-14 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Lawama ya wazi ni heri, Kuliko upendo uliositirika. Jeraha utiwazo na rafiki ni amini; Bali kubusu kwa adui ni kwingi sana. Nafsi iliyoshiba hukinai sega la asali; Bali nafsi yenye njaa huona kila kitu kichungu kuwa kitamu. Kama ndege aendaye huko na huko mbali na kitundu chake; Ndivyo alivyo mtu aendaye huko na huko mbali na mahali pake. Marhamu na manukato huufurahisha moyo; Kadhalika utamu wa rafiki ya mtu utokao katika kusudi la moyo wake. Usimwache rafiki yako mwenyewe, wala rafiki ya baba yako, Wala usiende nyumbani mwa ndugu yako siku ya msiba wako. Afadhali jirani aliye karibu kuliko ndugu aliye mbali. Mwanangu, uwe na hekima na kunifurahisha moyo wangu; Ili nipate kumjibu anilaumuye. Mwenye busara huyaona mabaya na kujificha; Bali wajinga huendelea mbele wakaumia. Twaa nguo yake amdhaminiye mgeni; Mtoza rehani aliye mdhamini wa malaya. Mtu ambarikiye mwenzake kwa sauti kuu asubuhi na mapema; Itahesabiwa kuwa ni laana kwake.
Methali 27:5-14 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Afadhali karipio la wazi kuliko upendo uliofichika. Majeraha kutoka kwa rafiki yaonesha uaminifu, lakini adui huzidisha busu. Yeye aliyeshiba huchukia kabisa asali, bali kwa mwenye njaa hata kile kilicho kichungu kwake ni kitamu. Kama ndege atangatangavyo mbali na kiota chake, ndivyo alivyo mtu atangatangaye mbali na nyumbani mwake. Manukato na uvumba huleta furaha moyoni, nao uzuri wa rafiki huchipuka katika ushauri wake wa uaminifu. Usimwache rafiki yako wala rafiki wa baba yako, tena usiende nyumbani mwa ndugu yako wakati umepatwa na maafa. Bora jirani wa karibu kuliko ndugu aliye mbali. Mwanangu, uwe na hekima, nawe ulete furaha moyoni mwangu, ndipo nitakapoweza kumjibu yeyote anitendaye kwa dharau. Mtu mwenye busara huona hatari na kujificha, bali mjinga huendelea mbele, naye hupata madhara. Chukua vazi la yule awekaye dhamana kwa ajili ya mgeni; lishikilie liwe dhamana kwa ajili ya mgeni. Mtu akimbariki jirani yake kwa sauti kuu asubuhi na mapema, itahesabiwa kuwa ni laana.