Methali 27:14-27
Methali 27:14-27 Biblia Habari Njema (BHN)
Amwamkiaye jirani kwa kelele alfajiri, itaeleweka kwamba amemtakia laana. Mke mgomvi daima, ni sawa na tonatona ya maji siku ya mvua. Kumzuia ni sawa na kuzuia upepo, au kukamata mafuta kwa mkono. Chuma hunoa chuma, kadhalika mtu hufundishwa na wenzake. Anayeutunza mtini hula tini, anayemhudumia bwana wake ataheshimiwa. Kama uso ujionavyo wenyewe majini, ndivyo ujijuavyo mwenyewe moyoni. Kuzimu na Uharibifu kamwe havishibi, kadhalika na macho ya watu hayashibi. Ubora wa fedha au dhahabu hupimwa kwa moto, na mtu hupimwa kutokana na sifa zake. Mtwange mpumbavu katika kinu pamoja na nafaka, lakini hutafaulu kumtenganisha na upumbavu wake. Angalia vizuri hali ya mifugo yako; tunza vizuri wanyama wako. Maana utajiri haudumu milele, wala taji haidumu vizazi vyote. Baada ya kukata nyasi na kuzihifadhi, kata majani toka milimani, huku nyasi zinachipua upya. Kondoo watakupatia sufu kwa mavazi, mbuzi nao utauza na kujinunulia mashamba; watakupa maziwa ya kukutosha wewe na jamaa yako, na kwa ajili ya watumishi wako wa kike.
Methali 27:14-27 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Mtu ambarikiye mwenzake kwa sauti kuu asubuhi na mapema; Itahesabiwa kuwa ni laana kwake. Matone daima kudondoka siku ya mvua nyingi, Na mwanamke mgomvi ni sawasawa; Atakaye kumzuia huyo huuzuia upepo; Na mkono wake wa kulia hukuta mafuta. Chuma hunoa chuma; Ndivyo mtu aunoavyo uso wa rafiki yake. Yeye autunzaye mtini atakula matunda yake; Naye amhudumiaye bwana wake ataheshimiwa. Kama uso ufananavyo na uso katika maji; Kadhalika moyo wa mtu na mwenzake. Kuzimu na Uharibifu havishibi; Wala macho ya wanadamu hayashibi. Kalibu ni kwa fedha, na tanuri kwa dhahabu; Na mtu hujaribiwa kwa sifa zake. Hata ukimtwanga mpumbavu kwa mchi kinuni pamoja na ngano; Upumbavu wake hautamtoka. Fanya bidii kuijua hali ya makundi yako; Na kuwaangalia sana ng'ombe wako. Kwa maana mali haziwi za milele; Na taji je! Ladumu tangu kizazi hata kizazi? Manyasi hukatwa, na majani mabichi huchipua, Na mboga ya mlimani hukusanywa. Wana-kondoo hufaa kwa mavazi yako; Na mbuzi ni thamani ya shamba. Tena yatakuwapo maziwa ya mbuzi, Ya kukutosha kwa chakula chako, Na chakula cha watu wa nyumbani mwako, Na posho la vijakazi vyako.
Methali 27:14-27 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Mtu ambarikiye mwenzake kwa sauti kuu asubuhi na mapema; Itahesabiwa kuwa ni laana kwake. Kutona-tona daima siku ya mvua nyingi, Na mwanamke mgomvi ni sawasawa; Atakaye kumzuia huyo huuzuia upepo; Na mkono wake wa kuume hukuta mafuta. Chuma hunoa chuma; Ndivyo mtu aunoavyo uso wa rafiki yake. Yeye autunzaye mtini atakula matunda yake; Naye amhudumiaye bwana wake ataheshimiwa. Kama uso ufananavyo na uso katika maji; Kadhalika moyo wa mtu na mwenzake. Kuzimu na Uharibifu havishibi; Wala macho ya wanadamu hayashibi. Kalibu ni kwa fedha, na tanuru kwa dhahabu; Na mtu hujaribiwa kwa sifa zake. Hata ukimtwanga mpumbavu kwa mchi kinuni pamoja na ngano; Upumbavu wake hautamtoka. Fanya bidii kuijua hali ya makundi yako; Na kuwaangalia sana ng’ombe zako. Kwa maana mali haziwi za milele; Na taji je! Yadumu tangu kizazi hata kizazi? Manyasi huchukuliwa, na majani mabichi huonekana, Na maboga ya milimani hukusanyika. Wana-kondoo hufaa kwa mavazi yako; Na mbuzi ni thamani ya shamba Tena yatakuwapo maziwa ya mbuzi, Ya kukutosha kwa chakula chako, Na chakula cha watu wa nyumbani mwako, Na posho la vijakazi vyako.
Methali 27:14-27 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Mtu akimbariki jirani yake kwa sauti kuu asubuhi na mapema, itahesabiwa kuwa ni laana. Mke mgomvi ni kama matone yasiyokoma siku ya mvua. Kumzuia ni kama kuuzuia upepo, au kukamata mafuta kwa kiganja cha mkono. Kama vile chuma kinoavyo chuma, ndivyo mtu amnoavyo mwenzake. Yeye autunzaye mtini atakula tunda lake, naye amtunzaye bwana wake ataheshimiwa. Kama uso uonekanavyo kwenye maji, ndivyo hivyo moyo wa mtu humwonesha alivyo. Kuzimu na Uharibifu havishibi, wala macho ya mwanadamu hayashibi. Kalibu husafisha fedha na tanuru husafisha dhahabu, bali mtu hupimwa kwa sifa anazopewa na watu. Hata ukimtwanga mpumbavu kwenye kinu, ukimtwanga kama nafaka kwa mchi, hutauondoa upumbavu wake. Hakikisha kuwa unajua hali ya makundi yako ya kondoo na mbuzi; angalia ngʼombe wako kwa makini. Kwa kuwa utajiri haudumu milele, nalo taji halidumu vizazi vyote. Wakati majani makavu yameondolewa na mapya yamechipua, nayo majani toka milimani yamekusanywa, wana-kondoo watakupatia mavazi na mbuzi thamani ya shamba. Utakuwa na maziwa mengi ya mbuzi kukulisha wewe na jamaa yako, na kuwalisha wajakazi wako.